Habari za Punde

Balozi Seif awasilisha taarifa ya Serikali juu ya tekelezaji wa Ilani ya Mapinduzi Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha Taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi mbele ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika katika Ukumbu wa Jakaya Kikwete Mjini Dodoma.
 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa wakiendelea na Kikao chao cha kumpendekeza Dr. John Pombe Magufuli aendelee kugombea nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi chengine cha Miaka Mitano.
 Mteule wa Chama cha Mapinduzi atakayepeperusha bendera ya Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao Dr. Hussein Ali Hassan Mwinyi akitoa shukrani baada ya kukabidhiwa kijiti hicho kuelekea uchaguzi mkuu huo.
  Msanii wa Kizazi Kipya wa Muziki wa Bongo Fleva King Ali Kiba pamoja na wasanii wenzake wakitoa burdani kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Mjini Dodoma.
 Mke wa Rais Mstaafu wa Tanzania Mama Siti Mwinyi na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein wakishangiria matukio mbali mbali yaliyofanyika ndani ya ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.
Waziri Mkuu Mstaafu Wa Tanzania Mh. Eduward Ngonyai Lowasa akitoa salamu kwa Wastaafu wenzake kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Mjini Dodoma  uliowateuwa Dr. John Pombe Magufuli Kupeperusha Bendera ya CCM kwa upande wa Muungano na Dr. Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar Kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Picha na – OMPR – ZNZ.
NA Othman Khamis, OMPR
Hatua za kuimarisha Uchumi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  zimeleta mafanikio makubwa katika kasi ya ukuaji wa Uchumi na Maendeleo uliochangiwa zaidi na uwepo wa hali ya Amani na Utulivu hapa Nchini.
Akiwasilisha Taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi mbele ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa Mjini Dodoma, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hatua hiyo, imeiwezesha Serikali kutekeleza Mipango yake ya Maendeleo kwa kutumia fedha zake yenyewe za mapato inazokusanya, kwa kiasi kikubwa.
Balozi Seif amezipongeza Taasisi zinazosimamia ukusanyaji wa mapato kama vile Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuweza kuyatekeleza kwa ufanisi majukumu yao na kuweza kufikia mafanikio ya kuridhisha katika kipindi  cha Miaka Kumi inayomalizika sasa.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2019, Pato la Taifa limekua kutoka thamani ya Shilingi Bilioni 1,768 mwaka 2010 hadi kufikia thamani ya Shilingi Bilioni 3,078 mwaka 2019.
Balozi Seif alieleza kwamba ongezeko hilo ni sawa na mara 1.74 zaidi ya wakati wa Awamu ya Saba inaingia madarakani ambapo kasi ya ukuaji wa uchumi imepanda kutoka asilimia 4.3% mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.0% mwaka 2019. 
Mtendaji huyo Mkuu wa Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar alieleza kwamba Pato la Mwananchi Mmoja Mmoja nalo limeongezeka kutoka Shilingi  Laki 942,000 sawa na Dola za Marekani Mia 675 mwaka 2010, hadi kufikia Shilingi Milioni 2,549,000 sawa na Dola Elfu  1,114 mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko kubwa lililofikia sawa na asilimia Mia 170.59%.
Alifahamisha kwamba mfumko wa bei umeshuka kasi yake kutoka asilimia 14.7% mwaka 2011 hadi asilimia 2.9% mwaka 2019 hali iliyoleta faraja kwa wananchi kuweza kupata bidhaa muhimu kwa bei ya kuridhisha wakati Serikali kwa upande wake imefanikiwa kuongeza mapato mwaka hadi mwaka. 
Balozi Seif alibainisha kwamba Mapato ya ndani yalifikia Shilingi Bilioni 748.9 hadi  mwaka  2019/2020, ikilinganishwa na jumla ya shilingi Bilioni 181.1 zilizokusanywa mwaka 2010/2011, hali iliyopunguza utegemezi wa bajeti kutoka wastani wa asilimia 30.2%  mwaka 2010/2011 na kufikia wastani wa asilimia 5.7% mwaka 2018/2019.
Akizungumzia suala la miundombinu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema jitihada kubwa zimechukuliwa katika kuimarisha ujenzi wa Bara bara ambapo tayari Kilomita 129 zimeshakamilika katika Kiwango cha Lami katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Alisema hicho ni kiwango kikubwa kuwahi kujengwa katika Historia ya  Zanzibar kilichokwenda sambamba na Ujenzi wa Madaraja pamoja na kuweka Taa za Bara barani na zile za kuongozea vyombo vya  Moto.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mafanikio hayo makubwa yamekuja na kupatikana kutokana na Serikali Kuu kujikita zaidi katika ununuzi wa Vifaa na zana za kisasa za kutengenezea Bara bara kazi iliyofanywa na Wakala wa Bara bara Zanzibar.
Alieleza kwamba uimarishaji wa usafiri wa Anga umezingatiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar na ule wa Pemba kwa kujengwa njia za kupitia ndege kutoka Mita 1,805 hadi kufikia Mita za mraba elfu 3,427.
Alisema Wahandisi wa Ujenzi hivi sasa wanakamilisha Ujenzi wa Jengo Jipya la Abiria la Terminal 3 la Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume wenye Bara bara ndefu ya kurukia Ndege kuliko Viwanja vyote vya Afrika Mashariki ambao utahudumia Abiria wapatao 1,600,000 kwa Mwaka.
Akigusia Nishati ya umeme ambayo ni muhimu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi na ustawi wa maendeleo ya wananchi Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika awamu zake mbali mbali imefanya jitihada kadhaa za kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa na huduma za nishati za umeme wa uhakika.
Alisema katika jitihada zilizoanzishwa na Awamu za Uongozi wa Serikali zilizotangulia za kusambaza na kuwafikishia wananchi huduma ya Nishati popote walipo, Serikali imeweza kuufikisha umeme katika shehia zote za Unguja na Pemba ambapo kwa sasa nishati hiyo inapatikana katika vijiji 2,882 kati ya vijiji 3,259 sawa na asilimia 88.43% vikiwemo vijiji 354 vilivyopatiwa umeme katika kipindi hichi. 
Alisema Jumla ya Visiwa vidogo vidogo vitano (5) navyo vimepatiwa huduma ya umeme ambavyo ni Kisiwa Panza, Makoongwe, Shamiani (Mwambe), Fundo na Uvinje wakati  jitihada za kuufikisha umeme katika kisiwa cha Kokota na Njau huko Pemba zilipata changamoto na kusababisha kuchelewa kidogo.
Alieleza hata hivyo, fedha kwa ajili ya kazi hio zimeshatengwa na utekelezaji wa mpango huo utaendelezwa kama Serikali ilivyoahidi na kuwanasihi wakaazi wa Visiwa vya Kokota na Njau waendelee kuwa na subira kwenye dhamira hiyo njema itakayofanikiwa. 
Alibainisha kwamba kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme yaliyojitokeza, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuwa ipo haja ya kuwa na umeme wa uhakika na tayari ishaanza kutafuta njia mbadala za kupata vyanzo vipya vya nishati ya umeme. 
Alifahamisha kwamba utafiti uliofanywa Serikali Chini ya Wataalamu wa Shirika la Umeme Zanzibar {ZECO} kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) umeonesha kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa Zanzibar kupata nishati ya umeme inayotokana na nishati ya jua. 
“ Benki ya Dunia itatuunga mkono kwa kuanzia kupata MW 35, lakini wapo wawekezaji waliojiandaa kuwekeza zaidi ya MW 70 ”. Alifafanua Mtendaji huyo Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema hivi sasa Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo na tayari limefikia hatua nzuri kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na sekta binafsi, ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo muhimu kwa ustawi na Maendeleo ya Wananchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Viongozi pamoja na Watendaji wote kwa kuendelea kuwajibika na kuwashuku Wananchi kwa ustahamilivu na imani yao kubwa kwa Chama cha Mapinduzi na Serikali zake zote mbili kwa muda wote.
Halkadhalika Balozi Seif alitoa pongezi Maalum kwa Viongozi wad INI wa Madhehebu mbali mbali Nchini ambao wanaendelea kukesha kwa kuliombea mema Taifa la Tanzania liendelee kupiga hatua kubwa ya Kimaendeleo na Kiuchumi hasa baada ya kuimarika kwa Amani Nchini kote.
Naye akiwasilisha Taarifa ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa  juu ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi mbele ya Mkutano Mkuu huo wa CCM alisema viongozi wana wajibu wa kuwashawishi Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais John Pombe Magufuli kutokana na usimamizi wake mahiri wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Kipindi cha Miaka Mitano inayomalizika.
Mh. Majaliwa alisema ushahidi uko wazi wa mafanikio makubwa ya Uchumi wa Taifa uliopelekea Tanzania kuingia katika Uchumi wa Kati wiki chache zilizopita ndani ya usimamizi wa Dr.John Pombe Magufuli.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.