Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Biashara ya Kusafirisha Binaadumu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wazee ,Wanawake na Watoto Bi.Mau Makame Rajab, akizungumza wakati wa hafla ya Mafunzo ya Siku moja kuhusiana na biashara haramu ya usafirishaji binaadamu.

Na.Mwandishi wetu
NAIBU Katibu Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Zanzibar Bi. Maua Makame Rajab amesema biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu haiwezi ikatokomezwa na Serikali pekee, bali kuna hitajika nguvu za pamoja ili kuweza kupambana nayo.

Maua aliyasema hayo wakati akifunguwa Mafunzo ya siku moja kuhusu kupinga biashara haramu ya usafirishaji binadamu ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya siku ya kupinga biashara hiyo duniani itakayofikia kilele chake Julai 30 Mwaka huu.

Alisema kuwa kila mmoja atambuwe kwamba anajukumu la kupambana na biashara hiyo kuanzia ngazi za familia na wadau wote, zikiwemo taasisi zisizo za Serikali na za Serikali .

"Wote tutambuwe kuwa Serikali ina dhamira ya kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa ni ya Uchumi wa viwanda na Uchumi wa kati lengo ambalo litafikiwa tu ikiwa tunarasilimali watu wenye nguvu za uzalishaji na ujuzi hasa vijana", alisema.

Hivyo alisema kuwa moja ya matokeo mabaya ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu katika nchi ni uondoaji wa rasilimali watu ambao ni wazalishaji.

Mwenyekiti wa Secretairiet ya Kuzuia na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu Adatus Magere amesema safari ya kupambana na Biashara hiyo haramu hapa  nchini ilianza miaka kadhaa iliyopita ambapo mwaka 2008 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu. 

Alisema kuwa Sheria hiyo ndiyo iliyounda kamati ya kitaifa anayoiongoza, pamoja na Sekretariati yake ambayo ilianzishwa Desemba, 2011.

"Uzoefu tuliopata katika kipindi hiki kifupi unaonesha kuwa hii ni  vita ngumu inayohitaji kujitoa na wakati mwingine inaweza kuhatarisha maisha", alisema.

Hivyo alisema  Biashara hiyo ina mtandao mkubwa wa ndani na nje ya nchi ambao ni wa uhalifu wa kimataifa na hufanya shughuli zake kwa siri na wakati mwingine huhusisha magenge ya kimataifa ya uhalifu yanayojishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya na silaha. 

Magere alisema kuwa Biashara hiyo kama isipodhibitiwa ni hatari kwa usalama wa raia wao pamoja na nchi kwa ujumla. 

"Sisi kama Kamati pamoja na Sekretarieti kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumejipanga vilivyo katika kukabiliana na biashara hii hapa nchini", alifafanua.

Hivyo alisema kuwa wanaamini kuwa Serikali pamoja wadau wengine wataendelea kuwaunga mkono katika kutimiza azma yao.

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na kamati ya Secretairiet ya kupambana na  biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu chini ya ufashili ya Shirika la kimataifa la Wahamiaji IOM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.