Na Jaala Makame Haji -
ZEC
TUME
ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), imewataka maofisa na maofisa
wasaidizi wa uchaguzi Unguja, kuhakikisha wanazingatia matakwa ya katiba,
Sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji mstaafu
wa rufaa Mbarouk Salim Mbarouk, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa
maofisa hao katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Alisema
pamoja na baadhi ya maofisa hao kuwa na uzoefu katika kuendesha uchaguzi lakini
wanatakiwa kuzingatia maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi
hizo za uchaguzi kwa mazoea.
Aidha,
alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za
kufuatwa na kuzingatia kwani hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi
kuwa mzuri wenye ufanisi na kuondoa malalamiko au vurugu wakati wote wa
mchakato wa uchaguzi.
Makamo
huyo, alisema Nec imewaamini kuwateuwa kwa sababu wanao uwezo wa kufanya kazi
hiyo hivyo ni jambo la muhimu kujiamini na kujitambua kwamba wanapaswa
kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi, kanuni zake na maadili ya
Uchaguzi.
Hata
hivyo, alibainisha kuwa kwa mujibu wa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 74 (6) tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu
uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na wabunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
na madiwani kwa Tanzania bara.
"Tume
imewateuwa nyinyi kwa mujibu wa sheria na kuzingatia utendaji na uzoefu wenu
katika masuala ya Uchaguzi," alisema.
Hivyo
aliwasisitiza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yao ni muhimu kuzishirikisha
vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika masuala ambayo yanastahili
kushirikishwa.
Sambamba
na hayo alisema ni muhimu kuyajua na kuyatambua vyema maeneo yao wanayofanyia
kazi ikiwemo miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura.
Aliwasisitiza
kuzingatia mafunzo watakayopewa na kutosita kutoa uzoefu wa usimamizi wao ili
iwe ni somo kwao wote katika utekelezaji wa jukumu hilo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Sheria NEC, Emmanuel Kawisha, alisema chini
ya kanuni ya 16 (1) (b) na (3) ya kanuni za uchaguzi wa Rais na wabunge 2020 na
kanuni ya 14 (1) (b) na (3) ya kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa
msimamizi yoyote hatotakiwa kuwa mfuasi wa chama chochote cha siasa na kufanya
hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya uchaguzi.
Hivyo
aliwasisitiza maofisa hao kuhakikisha hawavai sare za chama wala kushabikia
chama chochote cha siasa kuanzia sasa na yoyote atakaebainika kufanya hivyo
atavuliwa cheo chake na kupewa mtu mwengine atakaeweza kutunza kiapo cha
uchaguzi.
Alisema
kwa mujibu wa kifungu cha 89 a na b cha sheria ya uchaguzi mtendaji au
msimamizi yoyote atakaesababisha uchaguzi kuharibika basi atatozwa faini ya
shilingi 1,000,000 au miaka miwili jela au vyote viwili kwa pamoja.
Mbali
na hayo aliwasihi kutunza siri za kiapo kwa kuzingatia katiba na sheria ya
uchaguzi.
Hata
hivyo alisema kuna makosa ambayo yanafanywa na watendaji wa uchaguzi wakati wa
uchaguzi ikiwemo usimamizi hafifu wa maofisa katika vituo vya kupigia kura na
kukosa umakini katika kuchagua watendaji mbalimbali wa uchaguzi.
Mkurugenzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar, Hamidu Mwanga, aliwaomba maofisa hao
kuimarisha mahusiano ya karibu katika kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika
kwa urahisi Oktoba 28 mwaka huu.
Katika
Mkutano huo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo mambo muhimu ya kuzingatia
katika kutoa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi, majukumu ya watendaji wa
uchaguzi na mambo muhimu ya kuzingatia, uteuzi wa wagombea na wajibu na majumu
ya watendaji wa vituo na mawakala wa vyama vya siasa.
No comments:
Post a Comment