Habari za Punde

AGENDA ZA MABEBERU FURSA KWA WATANZANIA



Na MWANDISHI WETU   
Agenda nyingi za Mabeberu wa ndani  na nje ya nchi hakika ni fursa ya kipekee kwa Watanzania kujua jinsi ya kukabiliana nazo, kupambana nazo kwa njia sahihi ambayo inawanufaisha na kutengeneza kipato kwa ajili ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja , familia na Taifa kwa ujumla.

Tanzania nchi huru iliyopata uhuru wake tarehe 09 Desemba mwaka 1961 ina kila sababu ya kuona imekomaa kiasi gani na kamwe sio nchi ya kubabaishwa na mabeberu wanaoimezea mate kila kukicha. Mabeberu wanasahau kuwa Tanzania Taifa lililobarikiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuwa na Amani, Utulivu na Mshikamano wa watu wake kitu ambacho kinaonewa wivu na mataifa ya ndani ya Bara la Afrika na duniani kote.

Tanzania kwa asili ni Taifa  kiongozi wengine wanafuata katika masuala mbalimbali ya kimataifa na taifa ambapo yanaanzia nyumbani, lakini upende usipende yanahusisha dunia bila kutarajiwa na wale wanaoionea kijicho nchi yetu. Tanzania imepewa  heshima Duniani katika rpoti ya nchi zenye Amani zaidi duniani mwaka 2020, Tanzania imetambulika kuwa moja ya nchi zenye amani zaidi duniani huku ikishika nafasi ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki

Wakati Mabeberu wa nchi wanapopanga mbinu za kuiharibu, kuivuruga, kubomoa ustawi wa nchi yetu na kuiondoa Amani tuliyonayo, ili wapate fursa ya kunyonya rasilimali zetu na kudhalilisha utu wetu,  Watanzania  wako macho hawadanganyiki ila  wanapata fursa ya kutafuta njia ya kuhimili vishindo vyao kwa  kuchapa kazi kwa bidii, kujineemesha na kujinufaisha kwa rasilimali alizowajalia Mwenyezi Mungu .

Mfano hai ni wakati muafaka huu wa uchaguzi wapo wanaotaka kujipenyeza kuhakikisha mwanya huu wa kufanya uchaguzi unakuwa ndio wakati muafaka wa kubomoa Taifa la Tanzania lakini wamechelewa badala yake ndio kwanza kila kukicha Watanzania wanamilila mola wao wapite salama kwa amani na kuhakikisha Umoja, Utul;ivu na Mshikamano unawaumbua wale wote wanaodhani ni wakati sahihi kujipenyeza.

Aidha, zama za ujima za kupewa shanga, nguo na pesa na kuuza watu wetu, kuwadhalilisha na kuwapa viongozi wetu matoi na vitu ambavyo havina thamani kama utu wa binadamu, umepitwa na wakati kwa kuwa misingi iliyojengwa na waasisi wetu hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shekh Abeid Amani Karume imejengwa kwa zege la chuma ambalo kulivunja haiwezekani.

Akihutubia Kongamano la Maombi Maalum  ya Dua na Sala kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu 2020 lililofanyika Uwanja wa Jamhuri  Mkoa wa Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema “ Tanzania ni nchi huru ambayo kila Mtanzania anapaswa kujivunia kuwa yuko huru na ana haki ya kuheshimiwa utu wake na utamaduni wa Watanzania daima utadumishwa hatutaki kuletewa mila na desturi zinazoharibu umoja wetu”.

Mzee Butiku amesema “Maneno haya matatu yakizingatiwa  ya Amani, Umoja na Maendeleo yetu wote yanayotokana na juhudi zetu sisi wenyewe.  

Aidha, ameongeza na amesema “Kwa nini nipo hapa katika umri huu wa miaka 82 ni kushirikiana na nyinyi wote na Mheshimiwa Rais wetu nikiwa bado najisikia mwenye nguvu na kukumbushana kuhusu umuhimu wa jambo hili Amani ya Taifa letu,  Umoja ya Taifa letu na Maendeleo ya Watanzania katika Taifa lao, umuhimu wa uongozi bora wa Taifa letu na jinsi ya kupata uongozi na viongozi bora kupitia mchakato wa uchaguzi ulio huru, haki na unaotoa matumaini” amesisitiza Mzee Butiku.

Nawakumbusha waasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Shekh Abeid Amani Karume  tunakumbuka walivyohangaika kujitolea na kuhatarisha maisha yao katika kuweka misingi, taratibu za uongozi wa nchi wakitanguliza  watu waliokuwepo wakati huo na watakaokuja baadaye wakazingatia usawa wa watu hao, heshima ya watu hao, demokrasia  yao na haki zao wote bila ubaguzi wowote. Misingi hiyo ya usawa bila ubaguzi wa aina yeyote heshima kwa watu wote, haki sawa kwa watu wote, mbele ya sheria na katika fani za aina mbalimbali na kutochanganya siasa na imani za dini zetu ndio iliyotujengea Amani, Umoja, na maendeleo kwa watu wote.

Tukubali tukatae kama anavyosema Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli kuwa vita ya uchumi ni ngumu kwani inakuwa na vikwazo vingi kutoka kwa mabeberu hawafurahii maendeleo ya Tanzania, Watanzania muwe macho na watu wasioitakia mema Tanzania.

Mabeberu wamekuja na agenda zao na kufanya hila mbalimbali za kuhujumu uchumi wakidhani wanawakomoa Watanzania matokeo kuna mafanikio mengi sana ndani ya miaka mitano ambayo inaishangaza dunia. Kwanza Tanzania kuingia Uchumi wa Kati kabla ya makusudio ya kufika mwaka 2025 ni maajabu yaliyoiduwaza dunia hususan mabeberu wanaoimezea mate nchi ya Tanzania.

Ushindi wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile, reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Umeme la Nyerere, ilikuwa na pingamizi kutoka kwa bwana wakubwa wanaoshikilia dunia, Ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na ununuzi wa ndege 11, Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA), Ujenzi wa hospitali za Mkoa, Wilaya na uboreshaji na vituo vya Afya na ujenzi wa vituo vipya  ujenzi wa miundombinu ya barabara  kuunganisha mikoa, wilaya na vijiji, Upanuzi wa Bandari zetu Bahari ya Hindi na Maziwa, ununuzi wa meli mpya na vivuko vya kisasa  na  ukamilishaji wa miradi ya maji hakika  ni maajabu mengine ambayo mabeberu hawataki kusikia.

Hivi karibuni Tanzania imedhihirisha haina utani na wahujumu uchumi kwa kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana nao ili kubadilisha mtazamo wa vizazi vijavyo kuwa uhujumu uchumi ni kitu kibaya na sio utamaduni wa Mtanzania. Zaidi ya watuhumiwa 467 wa uhujumu uchumi wamefikishwa kwenye  vyombo vya sheria  na kukiri makosa yao kwa kurejesha fedha za umma bilioni 107 walizozifuja na mali kadhaa.

Aidha, zaidi ya magari 130 ambayo yamefanya makosa mbalimbali hususan ya uhujumu uchumi, uhalifu wa dawa za kulevya, ubebaji wa wahamiaji haramu na mengineyo yamesababisha  magari hayo kutaifishwa na kupewa Serikali na Taasisi za Umma zenye mahitaji ya magari kwa manufaa ya Watanzania.

Hivyo, majangili wa nyara za Serikali  na wahujumu wa mali zetu za asili kama wanyama pori, pembe za ndovu, madini, misitu (magogo) na samaki. Mabeberu wanaoiba ubunifu wa Watanzania na kutangaza vitu vingi vya Tanzania kuwa ni vyao hakika wameumbuka kwa kuwa sasa kila kilicho chetu tunakijua na tunakitangaza ni cha Tanzania.

Pia, kuna makongamano, shangwe ya vijana na majukwaa mengi yaliyofanyika katika kuwapa elimu makundi mbalimbali kama vile vijana, wanawake, walemavu na wasanii kabla ya kuanza kampeni yamewapa mwanga Watanzania wa kufanya biashara ndani ya makongamano na mikutano husika na kuhakikisha wanaufaika kiuchumi, ambapo hili ni pigo kwa mabeberu ambao wanafurahia wakiona wananchi wanakosa fursa za kufanya biashara na kusahau kampeni zinaanza ndio watafanya biashara sana na kunufaika kiuchumi.

Mabeberu walidhani watatumia mwanya na kisingizio kuhusu ugonjwa wa  Homa Kali ya Mapafu iletwayo na virusi vya Corona na kuhakikisha wanadhoofisha uchumi na juhudi za Tanzania katika kuwaletea Watanzania maendeleo, lakini Mungu amewaacha mabeberu hao midomo wazi  kwani Tanzania ni salama zaidi na  hakuna maambukizi ya Corona.

Kwa kuwa Dunia imefahamu jinsi Tanzania  ilivyopambana na ugonjwa wa Corona na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuaamua kufuata nyayo za Tanzania  za kutowafungia watu ndani, kufungua shule, vyuo vyote Barani Afrika na kuendelea kuchukua tahadhari japo ukweli ni kwamba hawataki kumtanguliza Mungu ili  awaepushe na janga hilo.

Aidha, Taasisi ya Kimataifa inayofanya Uchunguzi kwa Serikali za Afrika, Asia ndani na nje ya mabara yao yenye Makao Makuu yake nchini Norway (Whisteblowers Investigation Worldwide- WIW) imedhihirisha kuwa mabeberu wanaifatilia na kuinyemelea Tanzania kwa kutumia hali na mali ilimradi ihakikishe  inapenyeza agenda zao za kuendelea kuinyonya na kuikandamiza Tanzania.

Kutokana na harakati mbalimbali za mabeberu Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  imepata fursa na  imefanikiwa kuokoa fedha na mali zenye jumla ya shilingi bilioni 273.38, na kutaifisha fedha taslim shilingi milioni 899 katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu  ya Tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli. Kutokana na taarifa iliyopatikana kutoka kwenye taasisi hiyo imeweza kuokoa Dola za Marekani 1,191,651 na Euro, 4,301,399.  Ikiwa ni pamoja na kuokoa nyumba nane zenye thamani ya shilingi bilioni  11.6, magari matano yenye thamani ya shilingi milioni 126 na viwanja vitano.   

Pia, TAKUKURU wameokoa Dola za Marekani milioni 55.8, Euro milioni 43, magari 75, nyumba 41, viwanja 47 na mashamba 13, vyote hivyo ni fursa kwa Watanzania  kutumia rasilimali  zilizorejeshwa kuzalisha kwa wingi  mazao,  na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mafanikio mengine ambayo ni fursa ni kuongezeka kwa kasi ya utambuzi na urejeshaji serikalini wa mali na fedha vilivyotokana na vitendo vya rushwa. Mengine yaliyofatiliwa na Taasisi hiyo ni wakwepaji wa kodi na rushwa katika madini, ambapo sasa fursa lukuki zimejitokeza kwa wachimbaji wadogo wa madini ambapo mabeberu wamepata pigo lingine kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kuwa na madini Tanzanite yenye uzito mkubwa kuliko nchi yeyote duniani kilo 9.5 na kuwavutia watalii kutoka sehemu mbalmbali duniani kuja kujionea utajiri huo.

Kama hiyo haitoshi  zaidi ya Watanzania wengi wamejiajiri katika sekta ya uchimbaji wa Madini na kujipatia riziki zao za kila siku na kufurahia rasilimali aliyowapa Mwenyezi Mungu.

Pia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika kuhakikisha Madini yanawanufaisha Watanzania  imeleta matokeo ya Kampuni ya Barrick Gold Minning kuanza kulipa fidia ya kodi ya Dola ya Marekani milioni 300 hii ni safari ndefu ya kuwapiga kikumbo mabeberu
Vita ya ufisadi imefanikiwa kuwachambua vibaraka wa mabeberu wala rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maji, afya na katika vyama vya ushirika ikiwa ni pamoja na masoko ya mazao ya kilimo (AMCOS), wakopeshaji wasiokuwa na leseni, ufuatiliaji wa mali za Serikali zilizoporwa au kuchukuliwa bila kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu wote wapo kitanzini  hawana pa kupumulia NCHI HII HAINA NAFASI KWA MABEBERU NA VIBARAKA WAO.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.