Habari za Punde

Wizara ya Afya Zanzibar Yazindua Mkakati wa Miaka Mitano wa Digitali ya Afya

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akizindua mkakati wa kidigitali wa Afya katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Verde, Mtoni Mjini Zanzibar.
Baadhi ya waalikwa waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa kidigitali wa Afya ulifanyika Hoteli ya Verde, Zanzibar.
Afisa tathmini na ufuatiliaji kitengo cha Malaria Zanzibar Mohamed Haji akimpa maelezo Waziri wa Afya Hamad Rashid namna wanafofanya kazi kwakutumia mfumo wa kidigitali, alipotembelea banda lamaonyesho wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Kidijitali wa Afya.
Waziri wa Afya Hamad Rashid (katikati) katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni waliohudhuria uzinduzi wa mkakati wa kidigitali wa Afya.
Picha na Makame Mshenga. 
Na Ramadhani Ali – Maelezo                  10.9.2020
Waziri wa Afya Mhe.Hamad Rashid Mohamed ameshauri kuanzishwa somo la Teknolojia ya Kidijitali kuanzia skuli za msingi ili kuzalisha wanasayansi watakaomudu mifumo ya sasa ya utendaji kazi.
Waziri Hamad ameeleza hayo wakati akizindua Mkakati wa miaka mitano wa Kidijitali wa Afya katika Hoteli ya Verde Mtoni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema mfumo wa Teknolojia ya Kidijitali, unaotumika duniani kote hivi sasa, unahitaji vijana wenye upeo mkubwa katika fani hiyo  na maandalizi ya mapema ni jambo la msingi badala ya kusibiri kusoma ngazi ya elimu ya juu.
Alisisitiza kuwa matumizi ya Teknolojia yamekua yakiongezeka na kuhusisha sekta zote muhimu katika kuharakisha maendeleo ya nchi.
Waziri wa Afya amesema kuzinduliwa kwa Mkakati wa Afya wa Kidijitali Zanzibar ni hatua mpya ya maendeleo kwa upande wa huduma za afya ambapo itarahisisha utendaji kazi katika maeneo mbali mbali.
Hata hivyo amewataka madaktari na wahudumu wengine wa afya kuongeza taaluma ya matumizi ya Teknolojia ya Kidijitali ili kuongeza ufanisi katika kazi zao za kila siku.        
Waziri Hamad Rashid alisisitiza kuwa huduma za afya za kidijitali zinamchango  mkubwa katika utoaji na upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii na kupunguza gharama kwa Serikali na wagonjwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla  alisema matumizi ya kidijitali katika utoaji wa huduma za afya umeanza zamani katika baadhi ya hospitali hasa katika kuimarisha huduma za uchunguzi pamoja na shughuli za utawala.
 Katika taarifa yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema Mkakati wa Kidigitali wa afya uliozinduliwa utakaounganisha mawasiliano katika Hospitali na vituo vya afya utaleta mapinduzi makubwa katika kutoa  huduma za afya.
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya duniani (WHO) Dkt. Ghirmay Andemichael Mkakati wa Kidijitali wa Afya ni nyenzo muhimu katika kufanikisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Alisema mawasiliano ya moja kwa moja kutoka kituo kimoja kwenda kituo chengine na taarifa za mara kwa mara zitasaidia kupunguza matumizi makubwa ya rasilimali za nchi.
Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Wizara ya Afya Mohamed Habib alisema mfumo huo wa Kijiditali wa afya utawawezesha madaktari bingwa walipo Hospitali ya rufaa Mnazimmoja kusaidia wagonjwa waliopo vituo vyengine kwa kuwasiliana moja kwa moja na watendaji wa waliopo vituoni humo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.