Habari za Punde

HESLB YAFAFANUA TAARIFA POTOFU MITANDAONI

Na Mwandishi Wetu, HESLB Dar Es Salaam 19.10. 2020

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefafanua kuhusu taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusiana na utaratibu wa kupata majibu ya maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2020/2021.


Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu (Oktoba 19, 2020) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema HESLB bado haijatoa orodha ya wanafunzi waliopangiwa mkopo na kuwa kwa sasa, kazi ya uchambuzi wa maombi ya mkopo yaliyowasilishwa inaendelea.

Badru amesema taarifa hizo zisizo sahihi zinazosambaa mitandaoni zinawaelekeza waombaji mikopo kupakua mfumo (application) katika simu zao utakaowawezesha kuona orodha ya wanafunzi waliopangiwa mkopo kwa mwaka 2020/2021.

“Taarifa rasmi kuhusu HESLB, zikiwemo zinazohusu wanafunzi wanaopangiwa mkopo zitatolewa kuanzia Novemba 10, 2020 kupitia akaunti walizotumia kuomba mkopo inayofahamika kama SIPA – Student’s Individual Permanent Account,’’ amesema Badru katika taarifa yake.

Badru ameongeza kuwa taarifa kuhusu wanafunzi waliopangiwa mikopo pia zitatolewa kupitia vyombo vya habari, tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) na mitandao ya kijamii ya HESLB ambayo ni twitter, instagram na facebook kwa jina la ‘HESLB Tanzania’.

Serikali imetenga kiasi cha Tsh Bilioni 464 katika mwaka wa masomo 2020/2021, zinazotarajia kusomesha jumla ya wanafunzi 145,000 wakiwemo wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 91,000 wanaoendelea na masomo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.