Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk Shein Azungumzia Suala la Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi kupitia vyombo vya  Habari wa Vyombo mbali mbali vya serikali na Binafsi,kuhusu matokeo ya Utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar hafla iliyofanyika leo Ikulu Mjini Zanzibar
Waandishi wa Habari wa Vyombo mbali mbali vya serikali na Binafsi, wakimsikiliza  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi kupitia vyombo hivyo leo ,kuhusu matokeo ya Utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Zanzibar.
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali inalenga  kuhakikisha faida zitokanazo na rasilimali ya Mafuta na Gesi asilia  zinachangia katika ukuaji wa uchumi na kuwanufaisha wananchi wote bila ya ubaguzi.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, wakati alipozungumza na waandishi  kutoka vyombo mbali mbali vya habari hapa nchini.

Amesema suala la utafutaji wa mafuta na gesi asilia ni jambo linalohusu maendeleo ya Zanzibar, hivyo kamwe halitakiwi kuleta mifarakano na badala yake linapasa kuwaunganisha.

Alisema wananchi wanapaswa kujiepusha na baadhi ya watu walioamuwa kuitumia agenda hiyo kwa dhamira ya kuwagawa , jambo ambalo ni kinyume na malengo ya serikali.

Alieleza suala la mafuta na gesi asilia ni sehemu ya uchumi wa Buluu, jambo ambalo limekuwa likitekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020.

Aidha, alisema katika ushughulikia wa suala hilo, Serikali imeanzisha Mamlaka ya udhibiti na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia (ZPRA) na Kampuni ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia Zanzibar (ZPDC) kwa lengo la kuimarisha usimamaizi  na udhibiti  wa shughuli za utafutaji, uchimbaji pamoja na uendelezaji wa rasilimali hizo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa katika usshughulikiaji wa suala hilo Serikali ilisaini mkataba wa Mgawanyo wa uzalishaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia na Kampuni ya RAK Gas kutoka Ras el Khaimah, katika sherehe zilizofanyiika Ikulu Oktoba 23, 2018.

Akizungumzia  kazi za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika Kitalu cha Pemba – Zanzibar chenye ukubwa kilomita za mraba 11,068, Dk. Shein alisema zoezi hilo lilianza mwaka 2017 kabla ya kusianiwa kwa mkataba wa PSA, kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya RAK Gas, ambapo   hatimae shughuli kadhaa zilifanyika ikiwemo uchukuaji wa taarifa kwa njia ya Anga  (Full Tensor Gradiometric Survey), kazi iliyofanywa na Kampuni ya Bell Geospace kutoka Scotland.

“Kazi hiyo ilifanywa ili kuangalia uwezekano wa kuwepo kwa miamba yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia”, alisema.

Alieleza kuwa kufuatia matokeo yaliopatikana, ililazimika kufanyika uchunguzi kwa njia ya mtetemeko (2 DSeismic Survey) kupitia kampuni ya BGP ya Jamuhuri ya Watu wa China katika maeneo ya baharini,  nchi kavu pamoja na maeneo ya kina kifupi cha bahari.

Dk. Shein alibainisha kuwa matokeo ya usafirishaji wa taarifa zilizokusanywa yameonyesha kuwepo kwa sura mbili tofauti, wakati ambapo kwa upande wa Unguja taarifa za mistari zilibainisha kuwepo ubora unaoridhisha na kuonesha maeneo ya miamba yenye maumbile yanayoweza kuhifadhi mafuta na gesi asilia.

“Kwa upande wa Pemba , taarifa imeonesha taarifa zenye kiwango kidogo cha ubora kutokana na maumbile ya kijiografia ya kisiiwa hicho (gegraphical Landscape)”alisema.

Alisema kutokana na matokeo hayo, kampuni ya RAK Gas ilichukua hatua ya kuendeleza kazi za utafutaji wa taarifa za mitetemo za mafuta na gesi asilia kwa kitalu cha Pemba-Zanzibar, matokeo yalioifanya kuendeleza uchunguzi kwa njia hiyo ya mitetemo katika kina kifupi cha maji, eneo ambalo lilionesha kuwepo viashiria vya gesi asilia.

Aidha, alisema matokeo ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa njia ya Anga (full tensor Gradiometric Survey pamoja na mtetemo (2D SEIS MIC Survey yameonyesha uwezekano wa kuwepo miamba yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia.

Vile vile, alisema utafutaji wa rasilimali hiyo kwa njia ya anga, umeonyesha kuwepo uwezekano wa miamba inayoweza kuhifadhi rasilimali hiyo katika maeneo ya Makoongwe (Pemba), Tumbatu pamoja na upande wa bahari ya Mashariki mwa kisiwa cha Unguja.

Sambamba na hilo alisema utafutaji wa rasilimali hiyo kwa njia ya mtetemo umeonyesha kuwepo maeneo matano yenye uwezekano wa kuwepo rasilimali hiyo, ambayo ni eneo la Bahari liliopo baina ya Kaskazi Mashariki mwa kisiwa cha Unguja na Kusini mwa kisiwa cha Pemba, eneo la Kaskazi, Kusini na Mashariki mwa kisiwa cha Unguja, eneo la bahari ya Kaskazini Magharibi mwa Kisiwa cha Pemba pamoja na eneo la Kusini mwa Kisiwa cha Pemba.

Alisema kwa ujumla wake maeneo hayo yaeonyesha kuwepo maumbile ya miamba yenye uwezo wa kuhifadhi rasilimali hiyo yenye ujazo wa futi Trilioni 3.8, hivyo kuwepo uwezekano wa kufanikiwa kugundua rasilimali hiyo kwa silimia 30, kiwango ambacho ni kikubwa katika utafutaji kwa njia ya mtetemo.

“….kuna uwezekano wa kupanda kutoka asilimia thelathini hadi asilimia arobaini na tano baada ya kukamilika utafutaji kwa njia ya mtetemo kupitia teknolojia ya 3D.”alisema.

Alifafanua kuwa dhamira njema ya serikali ya kushughulikia suala hilo inazidi kuleta matumaini ya kuwepo uwezekano wa kugundulika hapa Zanzibar.

Hata hivyo Rais Dk. Shein aliwatanabahisha wananchi kuwa pamoja na juhudi kubwa zinazohitajika katika  kusimamia, kudhibiti na kuiendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia, mchakato huo huchukua muda mrefu usiopungua miaka sita hadi minane tangu utafiti kufanyika; kabla ha wananchi kunufaika na rasilimali hizo.

Dk. Shein aliwataka wananchi kutovunjika moyo na kuendelea kuvuta subira na kubainisha matumaini yake kuwa wataweza kunufaika na rasilimali hiyo katika siku za usoni.

Aidha, alitoa shukurani kwa Rais wa Awamu ya nne wa Serikali ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuhakikisha suala hilo linapata ufumbuzi, Rais wa Jamuhuri ya Muunganio wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar kufanikisha malengo ya ushughulikiaji wake, Mtawala wa Ras Al Khaimah Sheikh Saud Bin Saqri Al Qasimi pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Rak Gas kwa hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa suala hilo.

Mapema, akimkaribisha Rais Dk. Shein, Waziri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi “Gavu” alimpongeza kwa uongozi wake na kufanikisha mambo mbali mbali ya maendeleo. .

Katika mkutano huo, waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali

walipata fursa ya kuuliza maswali mbali mbali pamoja na kumpongeza Dk. Shein kwa uongozi wake ulioleta maendleeo makubwa hapa nchini.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.