Habari za Punde

Watendaji wa Vituo Vya Upigaji Kura Zanzibar Wapatiwa Mafunzo na ZEC.

Na,JaalaMakame Haji - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC inaendelea na utoaji wa mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wote wa Unguja na Pemba watakaosimamia kazi zoezi la upigishaji kura linalotarajiwa kufanyika tarehe 28 mwezi huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Mjini Bi.Safia Iddi Muhammadi na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi “B” Ndg. Ali Rashid Suluh walisema mafunzo hayo yana lengo la kuwaandaa watendaji hao ili waweze kusimamia vyema jukumu la kitaifa la  kutoa huduma kwa wananchi watakaofika vituoni kwa lengo la kupiga kura.

Walisema katika kufikia malengo hayo Tume ya Uchaguzi imewataka watendaji hao kuifanya kazi hiyo kwa uadilifi ,uaminifu na umakini wa hali ya juu pamoja na kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo bila ya utashi wa chama chochote cha siasa.

Mapema akifungua mafunzo hayo kituo cha Wilaya ya Magharibi “B” Mkuu wa kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura, habari na Mawasiliano ya umma Ndg.Juma Msanifu Sheha na katika kituo cha Wilaya ya Mjini Afisa mwandamizi mstaafu wa Tume hiyo Ndg. Juma Haji Ussi walisema Tume imewaamini kufanya kazi hiyo hivyo ni vyema wakatumia busara na uvumilivu utakaosaidia kuondosha malalamiko baina yao.

Ndugu Msanifu amewataka watendaji hao kutoa huduma nzuri kwa watu wenye mahitaji maalum wakiwemo wazee, wajawazito, wanaonyonyosha na Watu wenye ulemavu wa aina zote wanapofika vituoni kwa kuwahudumia bila hata kupanga foleni.

Nao Watendaji wa vituo vya kupigia kura wamewahakikishia wananchi kuwa watasimamia na kuendesha zoezi la upigaji kura katika hali ya amani na utulivu.

Wakizungumza wakati wakiendelea kupatiwa mafunzo ya kiutendaji katika maeneo mbali mbali ya Wilaya za Unguja wamesema watatoa huduma nzuri kwa wananchi kutokana na maandalizi mazuri yaliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya  Zanzibar.

Wameeleza kuwa,  hatua muhimu wametakiwa kuifanya kazi hiyo kwa ushirikiano wa hali ya juu ili kuwasaidia kufanikisha zoezi hilo na kwa kuzingatia zaidi hali za watu wenye mahitaji maalum

Akifafanua mambo muhimu wanayopaswa kuyazingatia watendaji hao msaidizi msimamizi wa uchaguzi jimbo la Tumbatu Ndg. Ali Darweshi Chande alisema kila mtendaji anajukumu la kufahamu wajibu wake na jukumu alilonalo hasa kwa wale wakuu wa vituo (PO)

Mafunzo hayo yanatarajiwa kukamilika tarehe 25 Oktoba, 2020 kwa watendaji wote wa vituo 1412 vya Unguja na Pemba na kujiandaa kwa kazi ya Upigishaji wa Kura wa tarehe 27 na 28 Oktoba,2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.