Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe Simai Mohammed Said alipofika kwa Mchina kupokea msaada wa madawati yaliyotolewa na Mfanyabiashara Khaled Al Khaudi
Sehemu ya madawati yaliyopokelewa na Waziri leo hii
Na Mwandishi wetu
Zaidi ya madawati 1500 yenye thamani ya shilingi 240,000.000 yametolewa na mfanya biashara Khaled Al-Khaudi kutoka Abudhabi UAE kwa lengo la kupunguza tatizo la madawati nchini.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema upatikanaji wa madawati kutaisaidia sana Wizara yake katika kuondokana na tatizo la vikalio katika Skuli zake.
Akizungumza wakati alipofika kuangalia msaada huo pamoja na Meza za maabara huko kwa mchina, Mhe Simai amesema Serikali ya awamu iliyopita imefanya kazi kubwa ya kununua madawati ambapo zaidi ya madawati Elfu 44 yamenunuliwa kwa Skuli za Sekondari na zaidi ya madawati elfu 11 kwa ajili ya Skuli za Msingi.
Amesema anaimani kuwa msaada huo walioupata kwa awamu ya kwanza utasaidia kupunguza tatizo la madawati na kuhakikisha watoto wote wanapata vikalio katika Skuli zao.
Amesema mbali na madawati hayo pia kuna awamu nyengine itafuata huku akiwaomba wafanya biashara wengine na wadau wengine na wanaoishi nje ya nchi kusaidia sekta ya Elimu kwani michango yao wanaithamini katika kuleta maendeleo ya elimu nchini.
Nae mratibu wa madawadi hayo kutoka kwa mdhamini khaled, Bibi Sabine Emmerich amesema msaada huo umetolewa kwa kulenga kuwafikia zaidi Wanafunzi wa Skuli za Nungwi pamoja na Skuli za karibu zenye mahitaji kwa kuhakikisha walimu wanafanya kazi yao vizuri na Wanafuzi nao waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Amesema endapo msaada huo utatumika kama ulivyokusudiwa Mr.Khaled ambae ni mdhamini wa Madawati hayo ataendelea kusaidia zaidi ili kuleta maendeleo katika Elimu
No comments:
Post a Comment