Habari za Punde

RC Mjini Magharibi azitaka taasisi za Serikali kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Idrissa Kitwana Mustafa akizungumza na Waandishi wa Habari katika mafunzo ya kushajihisha masuala ya Amani, Utangamano na Utamaduni wa kupokea maoni mbadala baada ya Uchaguzi Mkuu, (kushoto) ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Zanzibar Abdallah Mfaume. hafla iliyofanyika Ukumbi wa Kitengo cha Uzazi shirikishi Kidongo Chekundu Unguja.


Na Maryam Kidiko / Mwashungi Tahir -  Maelezo.        23/12/2020.

 

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mhe Idrissa Kitwana Mustafa amezitaka taasisi za serikali kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari katika kutoa taarifa ili kuibua matatizo yanayoikabili jamii na kuyapatia ufumbuzi.

Ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya waandishi wa habari juu ya  kushajiisha masuala ya amani,utangamano na utamaduni wa kupokea maoni mbadala  baada ya uchaguzi mkuu huko Ukumbi wa Kitengo cha Uzazi Shirikishi,Kidongo Chekundu Unguja.

Alisema kuficha taarifa na kutoeleza ukweli kwa jamii hupelekea kuwepo uvumi na kujenga dhana potofu na kutokuwa na imani kwa viongozi wao.

Aidha alisema wananchi wanahitaji kupata taarifa zilizosahihi za matukio yanayotokea sehemu mbali mbali ya maendeleo, kiuchumi na kisiasa kwa lengo la kuleta ufanisi na kuendelea kuwa na amani nchini.

Mkuu wa Mkoa huyo amewataka waandshi kufahamu mafanikio, maendeleo na ujenzi wa amani ya taifa lolote duniani yanahitaji zaidi utolewaji wa taarifa kupitia vyombo vya habari bila ya kutoka nje ya maadili ya kazi.

Hata hivyo amewataka watendaji wa vyombo hivyo kutochoka kuibua vikwazo vinavyowakabili wananchi na kuvifanyia kazi pamoja na kuyasemea yanayotekelezwa na serikali ili wananchi kuyafahamu.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Mwandishi Mwandamizi Ali Sultan alisisitiza waandishi kuacha ushabiki wa mambo yasiyo na faida kwa jamii pamoja na kuvilinda vyanzo vyao vya habari ili kuepuka kuvunja amani katika fani hiyo.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na klabu ya waandishi wa habari zanzibar zpc kwa ufadhili wa Internews.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.