Habari za Punde

Bandari ya Tanga imetajwa kuwa ya pili kwa upokeaji na usafirishaji Mafuta, ikiongozwa na Dar es salaam


Na Hamida Kamchalla, PANGANI.

MKOA wa Tanga umetajwa kushika namba mbili kwa upokeaji na usafirishaji wa mizigo hasa ya mafuta kupitia bandari ambayo pindi itakapokwisha itakuwa chachu ya maendeleo ya mkoa na ni kubwa na yakisasa baada ya Dar es salaam.

Akiwahutubia wananchi wilayani Pangani, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alisema mradi mkubwa wa bandari ya Tanga utakwenda kubadilisha uchumi na kuufanya mkoa kuwa wa kisasa huku akiwataka wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya nchi.

Suluhu alieleza kwamba sambamba na bandari hiyo kuja kuleta mapinduzi ya kibiashara na uchumi, wilaya hiyo pia ina rasilimali ambazo maeneo mengine hakuna hivyo kuwaasa wananchi kuzitumia vizuri ili kujiletea maendeleo pamoja na kujivunia kwa utunzaji mzuri wa rasilimali hizo.

"Bandari ya Tanga sasa hivi inajengwa vizimba na vifaa vya kupokelea mizigo, nataka niwaambie bandari ile ikafanye mkoa huu kuwa wa pili kwa kupokea mizigo ya mafuta, magari na mengineyo atakayotumika upande wa kaskazini wa nchi yetu, lakini mbali na mafuta pia itahudumia meli tofauti tofauti zitazotumika kuteremsha au kubeba bidhaa zitakazokwenda maeneo mengine" alisema.

Hata hivyo alisema mbali na hilo kuna matengenezo makubwa ya uwanja wa ndege ili kuufanya uwe unahudumia masaa 24 na mkubwa utakaupa hadhi mkoa wa Tanga.

"Kwahiyo niseme hongereni sana Tanga kwenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji mko vizuri, na tumeuangalia vizuri tukijua kwamba ni mkoa wa uwekezaji, viwanda vingi viko hapa, jana nimeweka mawe ya msingi na kuzindua viwanda kadhaa katika wilaya za Handeni na Korogwe vya kuchakata mazao ya kilimo" alisema.

"Ni imani yangu kwamba kwa viwanda vilivyopo na mwongozo nitakaouzindua keshokutwa, Tanga itaendelea kuwa mkoa wa viwanda na biashara kama ilivyokuwa zamani, lakini ukiacha hayo pia huu ni mkoa wa utalii, kwahiyo hatuna budi kujenga mabarabara ili utalii na viwanda uweze kupaisha uchumi katika mkoa huu" aliongeza.

Aidha alisema bahari iliyopo mjini hapo ni kielelezo tosha cha kuifanya Pangani kuendana na uchumi wa bluu ambao uko kimkakati Zanzibar, kikubwa alisisitiza kuleta miradi zaidi na kuleta mwendeleo yatakayoibadilisha wilaya hiyo na kuwa ya kitalii.

Alieleza pia kuhusu ujenzi wa miundombinu na kwamba barabara inayoendelea kuchongwa kutoka Tanga- Pangani hadi Bagamoyo nao ni moja ya chanzo kitakachochangia kuiweka juu isitoshe aliwaasa pia kuitunza ili wapate manufaa ndani ya wilaya.

"Fedha tulizozileta zimehudumia barabara ile kwa kiwango cha changarawe nasasa ni nzuri, kwahiyo niwapongeze wakazi wa Pangani na halmashauri yenu kwa kazi nzuri mliyoifanya ya ujenzi wa miundombinu" alibainisha.

Suluhu alisema wakati leo ikiwa ni uzonduzi wa wiki ya maji, akizindua miradi kadhaa ikiwemo ya maji mkoani Tanga akiwa kwenye ziara ya kikazi na kusisitiza wananchi kuilinda ili kuisaidia serikali katika kutimiza majukumu yake.

Sambamba na hayo pia aliwasisitiza wananchi kujikita zaidi kwenye kilimo cha mkonge ambacho kipo kimkakati kwakua zao hilo ndilo linalobeba taswira ya mkoa na tayari wakulima kadhaa wa ndani wameshaanza kilimo hicho kinachopewa kipaumbele.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.