Habari za Punde

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) wateketeza tani 20 za Dawa

 Wafanyakazi wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar wakishusha shehena ya dawa katika Shehia ya Kikungwi kwa ajili ya kuharibiwa baada ya kubainika hazikufuata taratibu za utengenezaji.
Baadhi ya boksi za dawa zilizokosa viwango vya utengenezaji zilizoingizwa nchini na Unguja Pharmacy zikisubiri kuangamizwa katika shehia ya Kikungwi Mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi ya boksi za dawa zilizokosa viwango vya utengenezaji zilizoingizwa nchini na Unguja Pharmacy zikisubiri kuangamizwa katika shehia ya Kikungwi Mkoa wa Kusini Unguja.


Bulldoza la Idara ya Mawasiliano likiharibu dawa katika Shehia ya Kikungwi Mkoa wa Kusini Unguja zilizoingizwa nchini na Unguja Pharmacy zikiwa hazina viwango vinavyokidhi kwa matumizi.

Baadhi ya maafisa wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar wakisimamia uangamizwaji wa shehena ya dawa katika Shehia ya Kikungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Picha na Makame Mshenga.


Na Ramadhani Ali – Maelezo                     14.03.2021


Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi  Zanzibar (ZFDA) wameteketeza tani 20 za Dawa za aina mbali mbali zilizobainika kutengenezwa kinyume na utaratibu zilizoingizwa nchini na Unguja Pharmacy.


Dawa hizo zilikutwa katika ghala lake iliyopo Mwanakwerekwe baada ya wasamaria wema kutoa taarifa ya kuwepo dawa hizo Ofisi ya Chakula Dawa na Zanzibar.


Mkaguzi Mkuu wa Dawa wa ZFDA Mwadini Ahmada Mwadini amesema shehena hiyo ya dawa kutoka nchini India hazikuonesha Kampuni iliyotengeneza jambo ambalo ni kinyume kwa mujibu wa taratibu na sheria za utengenezaji wa bidhaa hiyo.


Alieleza kuwa dawa hizo ambazo zilikuwa zimeanza kusambazwa kwenye maduka mbali mbali hazina uwezo wa kutibu na zinaweza kusababisha athari za afya kwa watumiaji.


Kazi ya kuangamiza dawa hizo feki ilifanyika katika Shehia ya Kikungwi chini ya usimamizi wa maafisa wa Mazingira katika kuhakikisha inafanyika kwa umakini bila kuathiri walioendesha zoezi hilo na wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo.


Mkaguzi Mkuu wa Dawa wa ZFDA Mwadini Ahmada Mwadini aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa Tanuri maalumu la kuchomea bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu na zilizopitwa na wakati ili kuepusha athari zinazoweza kutokea wakati wa kufanya kazi hiyo sehemu zisizo rasmi.


Mkuu wa Divisheni ya ufuatiliaji na Operesheni za Kimazingira Subira Thabit amesema kabla ya kufanyika zoezi la kuangamiza bidhaa, hasa dawa, tahadhari kubwa inahitajika na hutoa miongozo kabla ya kuuanza zoezi la aina hiyo katika kuepusha athari za uchafuzi wa mazingira.


Mbali na kuangamiza shehena hiyo kubwa ya dawa, taratibu nyengine zinaendelea kuchukuliwa na ZFDA kwa mmiliki wa Unguja Pharmacy ili kutoa fundisho kwao na wafanyabiashara wengine wanye tabia ya kufanya vitendo vya udanganyifu wa kuingiza bidhaa zisizokuwa na viwango na zilizopitwa na wakati. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.