Habari za Punde

Mhe.Luhanga Mpina Ahoji Bungeni Anguko la Ukusanyaji Mapato Wizara ya Mifugo,Uvuvi,Maliasili na Utalii. Ashauri Uchunguzi Ufanyike Kama Kisa ni CORONA.

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni Dodoma

Na.Assenga Oscar - DODOMA

MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina ameitaka Serikali kuchunguza kwa kina sababu zilizopelekea kuwepo anguko kubwa la ukusanyaji mapato ya Serikali ya shilingi bilioni 12 kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja bilioni 495 kwenye Taasisi za TANAPA, TAWA na NCAA zilizoko Wizara ya Maliasili na Utalii ili kujiridhisha kama kweli limetokana na athari za ugonjwa wa Corona kama ilivyoelezwa.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bungeni Dodoma, Mpina ametahadharisha kuwa Corona isije ikatumika kama kichaka cha kuficha uzembe katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambayo wananchi wanayasubiria kuboresha huduma mbalimbali.

“Wakati tukipokea taarifa za kila wizara baadhi ya taasisi kushindwa kufikia malengo sababu wanaeleza ni Corona. Na mimi niseme kwamba ni kweli kabisa corona inaweza kuwa imechangia kupunguza mapato yetu lakini haiwezi kulingana na maeneo pengine ambapo waliweka lockdown wakazuia kila kitu hali zao ni mbaya zaidi na kwa hili nataka nimpongeze sana Hayati Tingatinga Dk. John Pombe Joseph Magufuli alivyotusimamia vizuri sana katika hili eneo madhara ya corona sisi hatujadhurika sana” alisema Mpina

Hivyo Mpina ameshauri Wizara ya Fedha kufuatilia kwa karibu taasisi zote za Serikali ili kujiridhisha kama sababu ya kuporomoka kwa mapato yao ni kweli ni corona maana janga hilo kipindi kama hiki mwaka jana hali ilikuwa mbaya lakini mapato yaliendelea kuwa mazuri.

“Lakini ninachotaka nitahadharishe hapa pia ni isije ikawa kinga watu wamekuwa wazembe kule kukusanya mapato ya Serikali alafu wanakuja hapa wanasema Corona na Wizara ya Fedha mnafuatilia namna gani kwenda kujiridhisha kweli sababu zinazotolewa ni za kweli, mnajiridhishaje , mnafatilia mkiambiwa corona tu mnasema ni corona kweli au kuna sababu zingine”alihoji Mpina

Mpina ametolea mfano Taaisi tatu za Wizara ya Malisiali na Utalii pamoja na Wizara ya Mifugo na Mifugo namna zilivyoanguka kimapato huku sababu kuu ikitajwa ni Corona.

“Tumeelezwa anguko kubwa sana la taasisi za TANAPA, NCAA pamoja na TAWA ambao walipanga kukusanya bilioni 584 wameweza kukusanya bilioni 89 tu katika kipindi cha kufikia mwezi wa nne kweli sasa kweli sababu ni hizo tu sababu ni corona?au zipo sababu nyingine, ukienda Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamepata anguko la bilioni 12.5 ikilinganishwa na mwaka jana kwa kipindi kama hiki je sababu ni hiyo corona kweli?au kuna sababu zingine mnaenda kufuatilia?”alihoji Mpina

Hivyo Mpina akabainisha kuwa ndio maana Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti akahoji kile kitengo cha ufuatiliaji na tathmini cha Wizara ya Fedha kinatekeleza kwa usahihi majukumu yake katika kufuatilia makusanyo ya Serikali.

“Ile Monitoring and Evaluation inayofanywa na Wizara ya Fedha ina usahihi gani katika kuhakikisha kwamba inaenda kubaini chanzo cha matatizo kinachosababisha kodi yetu kushuka” alihoji Mpina

Mbunge wa Kuteuliwa, Humphrey Polepole amesema licha ya janga la Corona kuikumba nchi yetu bado Tanzania ilikuwa na uchumi mzuri kati ya nchi 8 zinazoizunguka Tanzania hivyo kuungana na Mpina kuwa uchunguzi wa kina ufanyike ili kisingizio kisibaki kuwa ni corona

“Mheshimiwa Spika napenda kumpa taarifa mzungumzaji  ndugu yangu kwamba anachokisema kuhusu sababu zinazopelekea kuanguka kwa makusanyo tuhoji kama ni corona tu au kuna lingine kwa sababu mwaka jana mpaka mwisho wa mwaka Tanzania ndio nchi pekee ambayo ilikuwa ina uchumi chanya kati ya nchi zote 8 zinazoizunguka kwa hiyo lazima kiko kitu kingine zaidi ya Corona”amesema Polepole

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.