Habari za Punde

Nchi ya Ujerumani na Mpango Bora wa Kuwezesha Kilimo Cha Mkonge Nchini Tanzania

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

BALOZI wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Hess amesema kuwashawishi wawekezaji wakubwa kuja nchini kuwekeza katika kilimo cha mkonge ndio mpango wa kuwawezesha wakulima wadogo wa zao hilo.

Balozi Hess aliyasema hayo jana jijini Tanga alipokutana na viongozi wa Bodi ya Mkonge kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa zilizopo kwenye kilimo cha zao hilo ambapo alieleza namna nchi yake itakavyoweza kuwasaidia wakulima hao.

Katika ziara yake hiyo alipata nafasi ya kwenda kujionea uwekezaji wa mashamba makubwa na mdogo ya mkonge ikiwa ni pamoja na kutembelea kitalu pekee cha uzalishaji wa miche ya zao hilo nchini cha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Mlingano kilichopo wilayani Muheza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge nchini Saad Kambona alielezea umuhimu wa ziara ya Balozi Hess mkoani hapa pamoja na jitihada za serikali katika kuongeza uzalishaji pamoja na kuongeza thamani katika kilimo cha zao hilo.

Kambona alibainisha kwamba wana jukumu la kuhamasisha kilimo hicho ambapo pia Bodi imepewa jukumu na serikali kuhakikisha wanaongeza uzalisha kutoka tani elfu thelathini na saba kwasasa kwenda tani laki moja na ishirini elfu kufikia mwaka 2025.

"Zipo jitihada mbalimbali zilizofanyika ikiwepo Rais kufuta hati za mashamba kule wilayani Kilosa, mkoa wa Morogoro kwa lengo la kupata ardhi kubwa kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo na wawekezaji wakubwa, na hii siyo kwa ajili ya mazao mengine tu bali hata pia kwa kilimo cha mkonge zaidi" alisema.

Kambona alisema wamepata nafasi ya kuongea na Balozi huyo na kumuomba mambo makuu matatu likiwemo kuwezeshwa kupata msaada wa kifedha kwa wakulima wadogo ili waweze kuwakopesha na kumudu kuendesha kilimo hicho.

"Sote tunafahamu kwamba kilimo bila fedha ni kitu ambacho hakiwezekani, hali ya mashamba yetu siyo nzuri sana, kwahiyo tumeomba kama tungepata uwezeshwaji toka serikali ya Ujerumani tukaitumia kuizunguusha kuwakopesha wakulima wetu wadogo wakafanya kilimo chao na baada ya kuvuna wanakatwa kidogokidogo ili pesa ile iweze kuwawezesha wakulima wengine wengi zaidi ili tuweze kuenea nchi nzima kwa fedha hiyohiyo kutoka Ujerumani" alifafanua Kambona.

Aidha alisema jambo la pili waliloomba ni eneo la uongezwaji thamani wa zao hilo ambalo limezoeleka kuzalisha nyuzi, makapeti na kamba ambapo alieleza kwamba yapo maeneo ambayo kwa Tanzania hakuna hata kiwanda kimoja, likiwemo eneo la kutengeneza sukari ya mkonge, uzalishaji wa bidhaa za vifaa vya ujenzi kama matofali na vinginevyo.

Aliongeza kuwa jambo la tatu ni kuhusu suala la mashine na tekinolojia katika kuchakata zao la mkonge kutokana na nchi hiyo kuwepo kwenye biashara hiyo kwa muda mrefu lakini pia kuhimiza aawekezaji wa kampuni za magari aina ya BMWB na Mercedes Benz ambazo zinatengeneza vifaa vya ndani ya magari hayo kwa kutumia zao la mkonge.

"Lalini poa tumeomba wenye kampuni za magari ambao wanatumia mkonge kutengeneza sehemu za ndani na mabampa, waje kuwekeza kiwanda hapa nchini kwa ajili ya kuzalisha ile bidhaa kwa ajili ya kutengeneza hivyo vitu kule kwao" alieleza.

"Au waje kufanya kilimo mkataba na wakulima wetu ili tuongeze uzalishaji wa mkonge hapa ndani halafu soko wakawa ni wao, wanakuja kupata idadi na ubora wa mkonge wanaoutaka wao, lakini hii ni baada ya wao kuwa wabia katika kilimo cha huo mkonge wenyewe, tuna maeneo makubwa sana ya kulima zao hilo" aliongeza Kambona.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.