Habari za Punde

SMZ Yaanda Sheria Mpya ya Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar. - Mhe. Othman.



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Junuiya ya ZAYEDESA Mama Shadya Karume (kulia kwake) na (kushoto kwake ) Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum na Wafanyakazi wa Zayedesa na wa Wizara yake. wakati wa ziara yake kutembelea Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema vita dhidi ya dawa za kulevya ni sugu, inayohitaji juhudi za pamoja ili kuokoa nguvukazi ya taifa na uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo katika ziara yake ya kutembelea taasisi mbali mbali kikiwemo Kituo cha Kubadilisha Tabia kwa Watumiaji wa Dawa za Kulevya, Kidimni Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema licha ya kuwa tatizo la dawa za kulevya nchini, kama ilivyo kwingineko ulimwenguni, ni suala mtambuka, kulikabili kwake kunahitaji nguvu na mikakati imara ya pamoja, ikizingatiwa kwamba katika mapambano hayo yapo machungu ambayo baadaye yatageuka kuwa matamu na hatimaye mafanikio kwa umma.

“Tunahitaji mpango wa kitaifa katika kupambana na suala hili ambalo ni sugu sana ili kila mmoja aweze kutekeleza wajibu wake”, amesema Mheshimiwa Othman.

Aidha ameeleza azma ya sasa ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar, kuifanyia marekebisho Sheria ya Dawa za Kulevya na hatimaye kuiwasilisha katika Kikao kijacho cha Baraza la Wawakilishi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Kanali Burhan Zubeir Nassor, ametaja udhaifu katika mfumo wa uendeshaji kesi, vyombo vinavyojihusisha na usambazaji wa mihadarati, baa na baadhi ya hoteli, na ukosefu wa vifaa zikiwemo mashine za uchunguzi, kuwa miongoni mwa changamoto zinazodhoofisha vita dhidi ya dawa za kulevya hapa nchini.

Mheshimiwa Othman katika ziara hiyo ametembelea kituo cha ZAPHA- PLUS kiliopo Welezo, kukagua shughuli za kuwahudumia watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI na pia kuangalia harakati za Jumuiya ya ZAYADESA inayoongozwa na Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Zanzibar, Mama Shadya Karume.

Ziara hiyo imewajumuisha pia Waziri na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dokta Saada Mkuya Salum na Dokta Omar Dadi Shajak, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Mgaharibi Unguja, Bw. Idris Kitwana Mustafa, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Bw. Msaraka na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Bi Suzane Peter Kunambi. 



Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
20/10/2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.