Na Issa Mzee - Maelezo 17/11/2021
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), ACP Ahmed Makarani amezitaka Asasi za Kiraia kuisaidia Serikali katika kutoa elimu ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa maslahi ya Taifa.
Amesema endapo wanajamii waliowengi watapatiwa elimu hiyo, lengo la Serikali la kutokomeza uhalifu huo litafanikiwa na kuisaidia Zanzibar katika kutekeleza vyema miradi ya maendeleo.
Aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Jamii, ulioshirikisha wadau mbalimbali wa Asasi za Kiraia, uliofanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzibar.
Makarani alieleza kuwa, Asasi za Kiraia zipo karibu zaidi na wanajamii hivyo zina uwezo mkubwa wa kutoa elimu na kuizuwia Rushwa pale inapotendeka, jambo ambalo litaisaidia mamlaka hiyo katika kupambana na uhalifu huo.
Aidha alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na Rushwa na uhujumu uchumi hivyo ni vyema kwa kila mwanajamii kutoa ushirikiano wa dhati kwa Mamlaka hiyo ili kuendeleza mapambano dhidi ya Rushwa kwa maslahi ya wanachi.
Akiwasilisha mada kuhusu Uzuiaji Rushwa na Nafasi ya Sekta za Jamii katika kupambana na Rushwa, Afisa Elimu kutoka ZAECA Futari Mzee Ali, alisema Asasi za kiraia ziwe mstari wa mbele katika kutoa taarifa sahihi za rushwa na uhujumu uchumi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka na mamlaka husika.
Alisema mikataba mbalimbali ya kimataifa inazitaka asasi za kiraia zishirikishwe katika mapambano dhidi ya rushwa, kutokana na umuhimu mkubwa wa kusaidia katika upatikanaji wa taarifa sahihi na kuwa karibu zaidi na wajamii.
Hata hivyo, alisema ipo haja kwa kila Asasi ya kiraia kumlinda mtoaji taarifa ili kuhakikisha usalama wake, kwa lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya Rushwa.
Wakitoa maoni baadhi ya washiriki katika mkutano huo wamesema ipo haja ya utoaji wa elimu ya rushwa kwa kila mwanachi ikiwemo rushwa ya ngono, pamoja na kuondoa dhana potofu ya kuwaona wajinga baadhi ya watumishi wasiochukuwa Rushwa wakati wa kutoa huduma.
No comments:
Post a Comment