Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Ireland Ikulu leo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikiliza Mgeni wake  Balozi wa Jamhuri ya Ireland Nchini Tanzania Bibi.Mary O'Neill  wakati wa mazungumzo yao alipofika Ikulu jijini Zanzibar leo kujitambulisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na  Mgeni wake Balozi wa Jamhuri ya Ireland Nchini Tanzania Bibi.Mary O'Neill  alipofika kujitambulisha Ikulu jijini Zanzibar .
 Balozi wa Jamhuri ya Ireland Nchini Tanzania Bibi.Mary O'Neill  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na Mgeni wake  Balozi wa  baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika leo Ikulu jijini Zanzibar pamoja na kujitambulisha.[Picha na Ikulu] 08/11/2021.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania kwa kuahidi kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi katika kuimarisha sekta zake za maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania Bi Mary O’Neil aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya pande mbili hizo, na kuupongeza utayari wa Jamhuri ya Ireland kuahidi kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua za Jamhuri ya Ireland ya kuahidi kuwawezesha wanawake kutasaidia kwa kiasi kikubwa hasa kwa upande wa wanawake wanaojishughulisha na shughuli za kimaendeleo wakiwemo wakulima wa mwani ambao kwa upande wao wamekuwa na changamoto ya kukosa soko la bidhaa yao hiyo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza hatua ya nchi hiyo kutoa nafasi za masomo nchini humo na kusisitiza haja ya kuendeleza na kuongezwa zaidi hatua hiyo ili Wazanzibari walio wengi waweze kupata nafasi za masomo mbali mbali nchini humo.

Aliongeza kuwa katika eneo la utalii, ambapo Balozi O’Neil aliahidi kwa nchi yake kwamba atahakikisha anakuwa balozi wa kuitangaza na kuutangaza utalii wa Zanzibar nchini mwake, alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kwani hivi sasa wawekezaji katika sekta hiyo wamekuwa wakija Zanzibar na kuekeza kwa kasi sambamba na kuongezeka kwa watalii kufuatia kupungua kwa janga la UVIKO 19 duniani.

Alieleza kuwa suala zima la uhifadhi wa mazingira hasa katika bahari nalo limepewa kipaumbele zaidi na Serikali ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia uharibifu wa mazingira huku akieleza kwamba licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi na athari zake lakini bado hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa kuzibiti hali hiyo.

Kwa upande wa Uchumi wa Buluu, Rais Dk. Miwnyi alimueleza Balozi huyo hatua na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Nane huku akieleza kwamba Jamhuri ya Ireland inasababu kadhaa za kuunga mkono hatua hizo hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imeweza kupiga hatua kupitia Dira hiyo.

Nae Balozi Bi Mary O’Neil  alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya Jamhuri ya Ireland ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono hatua za kuwawezesha wanawake, nafasi za masomo, mazingira ya upatikanaji wa haki kwa jamii, sekta ya utalii,  mabadiliko ya tabia nchi, uchumi wa buluu na sekta nyenginezo.

Balozi O’Neil alieleza jinsi Jamhuri ya Ireland ilivyokuwa na nafasi nzuri ya kuuunga mkono Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya Uchumi wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi hiyo ni kutokana na nchi hiyo kuwa na mazingira yanayofanana na Zanzibar sambamba na kuitekeleza kwa vitendo Dira hiyo nchini humo.

Kitengo cha Habari.

Ikulu Zanzibar. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.