Habari za Punde

Serikali Yasisitiza Watu Wenye Ulemavu Wasinyanyapaliwe.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAZIRI wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye  Ulemavu, Jenista Mhagama amewataka wananchi kuacha tabia ya kuwanyanyapaa watu wenye Ulemavu badala yake kuwafanya wawe jumuishi katika maswala yote ya kila siku.

Waziri Mhagama aliyasema hayo juzi kwa niaba ya Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa, jijini Tanga kwenye maadhimisho ya watu wenye ulemavu ambayo Kitaifa yalifanyika mkoani humo katika viwanja vya Tangamano.

"Niendelee kutoa wito kwa Watanzania wote, kutowanyanyapaa wala kuwabagua watu wenye ulemavu, nao Wana haki sawa kama Watanzania wengine, nawashukuru wale wote ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuitikia wito huu na kuungana na serikali kuwafanya watu wenye ulemavu kuwa jumuishi katika maswala yote ya kila siku" alisema.

Alibainisha kwamba serikali kwa kuwajali wenye ulemavu imeendelea na itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwanza wanafunzi kuanzia ngazi ya msingi na sekondari wanapatiwa vifaa stahiki kulingana na ulemavu wao ili wapate elimu bora na kwamba vipo vitimwendo ambavyo vinatarajiwa kuanza kugaiwa kwa wanafunzi hao.

"Serikali imeendelea kutenga fedha na itaendelea kutenga fedha ili kusambaza vishikwambi vilivyopo na ambavyo vimewekwa kamusi ya lugha za alama kwa wanafunzi hao wapate elimu bora na siyo Bora elimu" alieleza Mhagama.

"Vile vile serikali itaendelea kugawa vitimwendo vipatavyo 1403 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo kwa shule za sekondari na msingi, vitimwendo hivyo vitawasaidia wanafunzi wetu kuweza kujongea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine na kupata elimu katika maeneo mbalimbali" aliongeza.

Naye mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alisema zoezi la utambuzi linaendelea ili kujua idadi kamili ya watu wenye ulemavu ambapo alifafanua kwamba kukamilika kwa zoezi hilo itasaidia kuelekeza huduma za msingi kwa watu wenye ulemavu kupitia Halmashauri na ngazi nyingine.

"Mkoa wa Tanga unakadiriwa kuwa na jumla ya watu wenye ulemavu 6300, ambao wanaume ni 3400 na wanawake 2900, kati ya hao walemavu wa viungo ni  2177, wenye ulemavu wa ngozi ni 930, wasioona 844 na walemavu wenye matatizo ya kusikia ni 1500" alifafanua.

"Zoezi la utambuzi linaendelea ili kupata takeimu sahihi, na halisi ya kila aina ya ulemavu na mahitaji yao, na kukamilika kwa zoezi hili kutatuwezesha kuelekeza huduma za msingi kwa wanajamii wenzetu hawa kupitia Halmashauri, taasisi zingine pamoja na serikali ya Mkoa na serikali kuu" alisema.

Kwa upande wao walemavu hao walieleza kwamba bado wana changamoto ya kutoshirikishwa kikamilifu katika ngazi za maamuzi, kuanzia ngazi za chini kwenda juu lakini pia huduma wanazopata haziwanufaishi moja kwa moja kundi la wenye ulemavu.

Aidha walisema kuwa endapo watakuwa kwenye nafasi za uongozi bila kubaguliwa itachangia kuongeza uelewa ndani ya jamii na kuona kwamba wanaweza na kuongeza kuwa bado kuna unyanyapaa na mtazamo hasi kwa wenye ulemavu katika jamii nyingi na hali hiyo inapelekea vitendo ambavyo haviridhishi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.