Habari za Punde

MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA II

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Katika matini ya iliyotangulia nilieleza kwa kiasi shule hizi za Azania na Tambaza na baadhi ya shule za umma za Dar es Salaam na namna hali ya shule hizo zilivyokuwa na hali ya udugu na urafiki wa wanafunzi hao wakati huo.

Kwa siku ya leo naomba niutazame mgogoro mmojawapo wa Tambaza na shule ya Msingi ya Muhimbili ulisababisha ukuta wa Shule ya Msingi ya Muhimbili kuvunjwa.

Kama ramani ya Upanga ilivyo shule ya sekondari ya Tambaza inapakana na Barabara ya Umoja wa Mataifa, kwa mkono wa kushoto ukiwa unaitazama barabara hii, kuna shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) na kwa kulia ikipakana na Shule ya Msingi ya Muhimbili.

Shule ya Msingi Muhimbili wakati huo ilikuwa ni miongoni mwa shule kubwa za msingi jijini Dar es Salaam yenye wanafunzi wengi, iliyokuwa inafaulisha wanafunzi wengi kwenda sekondari za umma. Shule zingine za msingi zilizokuwa kama hii ni Mnazi Mmoja, Bunge (shule iliyojaa watoto wa wengi wa viongozi), Shule ya Msingi Mlimani, Shule ya Msingi Mchikichini, Shule ya Msingi Gerezani, Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Olympio (shule ya watoto wengi wa viongozi), Madenge, Mtoni Mtongani (Mama Mere) na zingine nyingi.

Shule hizi zilikuwa na walimu maaarufu waliokuwa wakiwafundisha vizuri wanafunzi hao hadi wakafaulu vizuri. Muhimbili walikuwa na mwalimu Ndossi, Mnazi Mmoja mwalimu Mtolela, Bunge Mwalimu Makwega , Uhuru Mchanganyiko Mwalimu Msangi na walimu wengine wengi.

Kwa hiyo wanafunzi hao waliofaulu kutoka shule hizo na shule nyingine wakifaulu walipangiwa shule hizi za kutwa na baadhi yao walipangiwa shule za bweni za Dar es Salaam mathalani Pugu na za mikoa mingine.

Wapo waliokosa nafasi hizo huku wakitafuta nafasi za kukariri tangu darasa la tano, sita au la saba.Wapo wengi waliopita kwa njia hii na walikuwa na majina tofauti na dini zao na makabila yao.Wengine waisoma shule za kulipia mathalani Kinondoni Muslimu, Thakhafa, Thakalini, Al Muntazir, Agakhan-Mzizima, Shaban Robert na zinginezo.

Kwa desturi tangu miaka mingi wanafunzi wa Tambaza walikuwa wakipita katika geti la pili la kuingilia Shule ya Msingi Muhimbili, geti hili lilikuwa na wigo wa miti na maua tu wanafunzi wa Tambaza walipita katika njia za kukimbilia mbio katika kiwanja kikubwa cha mpira wa miguu na kuingia katika eneo la Shule ya Tambaza jirani na bwalo la chakula na mabweni.

Jirani na Shule ya Muhimbili na jirani na bwalo na mabweni ya Tambaza palikuwa na viwanja vya michezo kadhaa, huku kukiwa na uwanja mkubwa wa mpira wa miguu niliyokueleza hapo juu. Uwanja huu ulikuwa una sehemu ya kukaa kama majukwa ya ngazi ambapo kwa miaka mingi wanafunzi wa Muhimbili na Tambaza walikuwa wakiutumia kucheza michezo mbalimbali kama vile mechi za madarasani, mechi za kirafiki baina ya shule na shule.

Kiwanja hiki kwa kuwa kilikuwa kikubwa na kizuri, kuna wakati hadi timu za Yanga na Simba zilikuwa zikifanya mazoezi. Binafsi nakumbuka Yanga waliwahi kufanya mazoezi nadhani mwaka 1992 na mimi nilimuona kwa mara ya kwanza Rifati Said (Mzanzibari) ambaye alikuwa Golikipa wa Yanga na Timu ya taifa wakati huo pia siku hiyo nilimuona Salumu Kabunda.

Kutokana na uwanja huo kuwa mzuri na mkubwa na ukiwa jirani na Ukumbi wa Diamond Jubilee matukio kadhaa yalikuwa yakifanyika, kwa hiyo Kamati ya Shule ya Msingi Muhimbili iliamua kujenga ukuta huo kwa nguvu za wazazi kwa sababu mbalimbali ikiwamo la usalama wa watoto wao Lakini nadhani jambo kubwa zaidi nia ya kuujenga ilikuwa ni kuongeza kipato cha shule hii.

Wakati ujenzi unafanyika viongozi wa wanafunzi wa Tambaza waliweza kupatawa hadi ramani ya shule ya Tambaza kabla shule hiihaijakabidhiwa kwa serikali, wakisema kuwa uwanja huo ni mali ya Shule ya Tambaza na siyo wa Shule ya Msingi ya Muhimbili huku mkuu wa shule akisema kuwa atalifanyia kazi jambo hilo.

Kujengwa kwa ukuta huo kuliibua dhana ya kuwanyima wanafunziwa Tambaza kushiriki michezo kwani Agakhan wasingeweza kujenga shule hiyo katika eneo finyu kama lilivyobaki walisema wanafunzi hao.

Jambo hilo liliwakwaza mno walimu na wanafunzi wengi wa Tambaza hususani mwalimu wa michezo wakati huo Mwalimu Hatia.

Hayo yakiendelea, ukuta ulikuwa unajengwa na kwa kuwa wanafunzi wa Tambaza walioneshwa ramani ya asili ya eneo hilo, hali ilikuwa mbaya mno. Hapo ndipo wanafunzi hawa wa Tambaza wakajichukulia sheria mkononi na kuuvunja ukuta huo kwa kutumia baruti na vyuma vizito.

Huku hali ya taharuki ikiongezeka mno katika eneo hilo nalo Jeshi la Polisi lilisimama imara chini ya RPC Mwinyi Dadi Ally. RPC Mwinyi Dada Ally aliyekuwa mzee mmoja mrefu sana mwembamba, mweupe, mpole sana, mwenye maneno machache na aliyekuwa akipenda kusali sana katika misikiti jirani alipokuwa akiishi.

Mwisho wa siku ukuta ulijengwa na wanafunzi wa Tambaza walipokuwa wakitaka kucheza katika kiwanja hicho walipaswa kuomba kwa Mkuu wa Shule ya Muhimbili , hadi leo huku Tambaza wakibakiwa na kiwanja cha mpira wa wavu,  na eneo kidogo.

Kwa kuwa nimezungumzia suala la ramani ya shule ya Tambaza ifahamike wazi kuwa shule hii kabla ya 1967 ilikuwa ikifahamika kama H,H AGAKHAN BOYS SECONDARY SCHOOL nayo Zanaki ilikuwa H.H AGAKHAN GIRLS SECONDARY SCHOOL na ndiyo maana wanafunzi hawa ni ndugu wa urafiki wa shule hizo ni tangu siku nyingi. Wengi walidai kuwa tangu mwanzo ilikuwa nadra wanafunzi wa Tambaza kuwafanyia vurugu wanafunzi wa Zanaki.

Baada ya shule hizo kuwa za umma wapo walimu waliokuwepo tangu awali yaani tangu H.H Agakhan ambao wengine walikuwa na asili ya Uhindi na Waarabu kwa hakika walikuwa wakisimulia historia ya shule hiyo kwa miaka mingi. Ndiyo maana ramani zilipatikana na kupatiwa wanafunzi na mgogoro huo ukawa mkubwa kisa ikidaiwa kuwa kiwanja hicho kuna mtu alikitaka ili kuweza kukodisha kwa shughuli mbalimbali.

Mwanakwetu naomba kwa leo niishie hapo, kipi kitaendelea subiri matini ijayo

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.