Habari za Punde

Umoja wa Ulaya EU kuendelea kuiunga mkono Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Mhe.Manfredo Fanti, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania Mhe Manfredo Fanti (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu) 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Umoja wa Ulaya (EU) wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu mbali mbali za maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), nchini Tanzania Manfredo Fanti akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua ya Umoja wa Ulaya (EU) ya kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha programu mbali mbali za maendeleo zitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza Sera yake ya Uchumi wa Buluu.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha Sera yake ya Uchumi wa Buluu inatekelezeka ipasavyo, hivyo, hatua za Umoja wa Ulaya (EU) kuziunga mkono juhudi hizo zitaleta mafanikio makubwa.

Aliongeza kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha utunzaji wa mazingira unapewa kipaumbele hasa uhifadhi wa mazingira ya bahari hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuyahifadhi na kutyalinda mazalio ya viumbe vya baharini.

Aidha, Rais Dk Mwinyi alieleza mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuwasaidia wakulima wa zao la mwani ambao asilimia kubwa ni wanawake ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kulisarifu zao hilo hapa hapa nchini badala ya kuliuza kama malighafi.

Alisema kuwa tayari kiwanda cha mwani kinajengwa huko Chamanangwe kisiwani Pemba, ikiwa ni miongoni mwa juhudi za kuhakikisha zao hilo linawanufaisha wakulima wake kwa kiasi kikubwa sambamba na kulipatia soko la uhakika litakalowaongezea kipato wakulima wa zao hilo.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuuimarisha Uchumi wa Buluu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo katika kuhakikisha wanapata uwezo wa kuvua kisasa na kuweza kupata pato kutokana na kutumia vifaa na nyenzo za kisasa sanjari na kuwasaidia wafugaji wa samaki.

Rais Dk. Mwinyi pia, alizungumzia suala zima la kuuimarisha Mji Mkongwe wa Zanzibar ambapo hivi sasa hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha Mji huo unaleta haiba yake ya asili huku akiupongeza Umoja huo  kwa kuunga mkono harakati za utalii katika Mji Mkongwe hasa katika Matamasha likiwemo Tamasha la Sauti za Busara.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza kiongozi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutafuta vyanzo vyengine vya nishati ya umeme hapa Zanzibar na kupongeza jinsi EU inavyounga mkono suala hilo.

Rais Dk. Mwinyi pia, alitumia fursa hiyo kuzikaribisha nchi za Umoja wa Ulaya kuja kuekeza Zanzibar kwani bado fursa kadhaa zingalipo hasa katika sekta ya uwekezaji na utalii kwa azma ile ile ya kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Buluu.

Mapema Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU),  nchini Tanzania Manfredo Fanti alimueleza Rais Dk. Mwinyi mipango na mikakati madhubuti iliyowekwa na Umoja huo katika kuisaidia Zanzibar kuimarisha na kuendeleza programu mbali mbali za maendeleo.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Fanti alipongeza juhudi zzinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi na kueleza matumaini  makubwa ya umoja huo ya kuiona Zanzibar inafunguka kimaendeleo.

Alieleza hatua zilizofikiwa na Umoja huo za kuanzisha programu za maendeleo katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa mwaka huu na kuendelea kwa mwaka ujao.

Akieleza miongoni mwa  programu hizo ni pamoja na kuhakikisha suala zima la mazingira linapewa kipaumbele hasa ikizingatiwa kwamba Umoja huo umetenga bajeti  maalum ya programu hizo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia hata kuwaendeleza wavuvi, kutunza misitu na uhifadhi wa mazingira yote ya baharini pamoja na viumbe vyake sambamba na kuendeleza hatua za kukabiliana na Tabianchi.

Pamoja na hayo, Balozi huyo alieleza azma ya Umoja huo kuunga mkono suala la jinsia kwa kuwasaidia wanawake katika kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Sambamba na hayo, Balozi  Fanti alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Umoja wa Ulaya (EU), utahakikisha unaiunga mkono Zanzibar katika nyanja zote za Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya uchumi wa Zanzibar.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.