Habari za Punde

Wafanyabiashara Zanzibar Watakiwa Kufuata Bei Elekezi.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wafanyabiashara mbali mbali alipokutana nao Ofisini kwake Vuga na kuwataka kutopandisha bei za bidhaa hasa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka                        Wafanyabiashara Nchini kuisaidia Serikali katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa   Ramadhani kwa kuhakikisha Chakula kinapatikana cha kutosha.                                                                           

Mhe. Hemed ameeleza hayo alipokutana na wafanyabiashara Ofisini kwake Vuga Zanzibar.

Amesema jukumu la Serikali ni kuhakikisha Chakula kinakuwepo kipindi chote ikiwemo kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kueleza kuwa SMZ inafarijika kuona Wafanyabiashara hao wanaisaidia Serikali katika upatikanaji wa Chakula Nchini.

Mhe. Hemed amesema kuwa hadi sasa hakuna viashiria vyovyote vya upungufu wa Chakula Nchini hatua ambayo Serikali  inamatumaini makubwa kwa wananchi wake kupata huduma hiyo bila ya changamoto yoyote.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wafanyabiashara hao kuhakikisha wanauza Biashara kwa kufuata bei elekezi na kukemea tabia ya baadhi ya Wafanyabiashara ambao hupandisha bei katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

"Baadhi ya Wafanyabiashara hutaka kutumia fursa hii kupata faida kubwa kwa maana ya kupandisha bei bila ya kujali kuwa mwananchi wa chini ndie anaeumia" Mhe. Hemed

Mhe Hemed amesema Wafanyabiashara hao ni vyema kusimamia makubaliano na Taasisi husika juu ya bei za Bidhaa ili kutomsumbua mwananchi anaetafuta huduma muhimu za vyakula.

"Kwa bidhaa zilizotolewa bei elekezi basi ikiwezekana kushusha ama kufuata bei hizo, hili ni faida kwenu na kwa wananchi’’ Alisema Mhe. Hemed .

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwashukuru Wafanyabiashara Nchini kwa kuisaidia Serikali katika kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu hasa ya chakula ili wananchi kuweza kupata huduma hizo za msingi na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwapata mashirikiano ili waweze kufanya biashara zao kwa utulivu bila ya usumbufu wowote.

Akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiashara wenzake Ndugu Said Nassir Nassor Bopar ameeleza kufurahishwa kwao kwa kitendo cha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwaita na kujadiliana nao kuhusu uwepo wa vyakula katika vipindi vyote hasa kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Aidha amewashauri Wafanyabiashara wenzake kutopandisha biashara kiholela hasa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa nia ya kupata faida kubwa zaidi na kuwasihi kuendelea kufanya biashara zao kwa mujibu wa makubaliano na Serikali.

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

16/03/2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.