Habari za Punde

Hutuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akiwasilisha hutuba ya Bajeti ya fedha ya Ofisi yake kwa Mwaka wa fedha 2022-2023. 

Jumla ya Shilingi za Kitanzania 67,368,924,250 zimeombwa kuidhinishwa kwa matumizi ya Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa Mwaka wa fedha 2022/2023.

Akisoma Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha fedha hizo kwa ajili ya Matumizi ya Ofisi. 

 

Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imepangiwa kukusanya mapato ya Jumla ya Shilingi za Kitanzania 92,826,495.

 

Katika Hotuba hiyo Mhe. Hemed ameeleza Mipango ya Serikali katika Sekta mbali mbali ikiwemo Afya, Elimu, maji safi na Salama, uwezeshaji Wananchi kiuchumi n.k.

 

Akigusia suala la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Serikali imeshaanzisha Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar na kueleza kuwa uanzishwaji wa Wakala huyo kutapelekea Uratibu mzuri na wa uhakika wa masuala ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. 

 

"Bila Shaka uanzishwaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar kutapelekea Uratibu Mzuri zaidi na wa uhakika wa masuala ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikiwa ni pamoja na masuala ya mafunzo na upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa Wajasiriamali na Wafanyabiashara pamoja na upatikanaji wa masoko kwa bidhaa wanazozalisha au huduma wanazotoa" Mhe. Hemed.

 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo katika kutekeleza malengo iliojowekea na amechukua fursa hiyo kuwashukuru wadau hao katika kuunga mkono shughuli za maendeleo nchini. 

 

Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa mashirika ya kitaifa na kimataifa ili yaendelee kufanya kazi zao kwa usalama na Amani.

 

Aidha Mhe. Hemed ameendelea kuwaasa wafanyabishara kuendelea kuuza bidhaa zao kwa bei nafuu kama zilivyoelekezwa na Mamlaka za Serikali ili kuwapa nafuu wananchi hasa katika kipindi hichi na kuzingatia ukusanyaji wa mapato pamoja na faida kwa wafanyabiashara.

 

Na.Abdulrahim Khamis

Ofisi ya makamu wa pili wa Rais wa zanzibar.

27/04/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.