Habari za Punde

Waislamu Wametakiwa Kukumbushana na Kuhamasishana Watu wenye Uwezo Kutoa Sadaka.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi wa Kijiji cha Chaani Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mweupe Chaani
WANANCHI wa Kijiji cha Chaani Mkoa wa Kusini Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akitowa nasaha zake kwa Wananchi baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mweupe Chaani
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi AlhajDk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi sadaka ya Tende Mwananchi wa Kijiji cha Chaani, baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mweupe Chaani Mkoa wa Kusini Unguja 

WANANCHI wa Kijiji cha Chaani Mkoa wa Kusini Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj.Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akizungumza na kuwasalimia Wananchi baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mweupe Chaani Unguja.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kaab (kulia kwa Rais) baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mweupe Chaani Mkoa wa Kusini Unguja na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud na Sheikh.Rashid Mazrui

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka waislamu kuendelea kukumbushana na kuwahamasisha watu wenye uwezo; kutoa sadaka zao kwa watu wenye uwezo duni.

Alhaj Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika salamu zake kwa waislamu walioshiriki katika Ibada ya Sala ya Ijumaa, iliofanyika katika Msikiti Mweupe Chaani Kubwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Akizungumza na waumini hao, Alhaj Mwinyi alisema kwa niaba yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, anatoa shukurani kwa wananchi   wote wa Zanzibar  waliotoa misaada mbali mbali kwa waislamu wenye uwezo mdogo katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, wakiwemo Sheikh Ariff na Sheikh Rashid Mazrui kutoka taasisi ya Miraj Tanzania  ambao walishiriki katika ibada hiyo.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alitoa shukurani za dhati kwa wananchi wa Sehiya ya Chaani kubwa kutokana na dua waliyomuombea ili aweze kuwa na afya njema na kutekeleza vyema majukumu yake ya kitaifa.

Alitumia fursa hiyo  kumuomba Mwenyezi Mungu kutakabal funga za waja wake.                                 

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume, aliwataka wananchi wa shehiya ya Chaani Kubwa kuendelea kumuombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Mwinyi, ili aweze kiutekeleza vyema majukumu yake akiwa mwenye afya njema.

Sheikh Arrif kutoka taasisi ya Miraj Tanzania aliwaomba wananchi wa Shehiya ya Chaani Kubwa na Zanzibar kwa ujumla, kumuombea Dua Alhaj Dk. Mwinyi ili aweze kuwatumikia waislamu na wananchi wote wa Zanzibar.

Mapema, Khatibu katikasala hiyo ya  Ijumaa, Sheikh Abdulghafour Abdulrahim  aliwakumbusha waislamu umuhimu wa kuendelea kutekeleza vyema ibada katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kama alivyofanya Mtume Muhammad (SAW), sambamba na kusafisha nyoyo zao.

Alisema saumu ni darasa linalowafunza waislamu , ambapo miongoni mwa mafunzo yaliomo  ni usiku wa Lailat Qadr.

Katika ibada hiyo ya sala ya Ijumaa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alikabidhi sadaka kwa waislamu walioshirki  katika ibada hiyo.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.