Habari za Punde

Dk.Mwinyi Amesisitiza Matumizi ya Mashine ya EFD Kwa Ukusanyaji wa Kodi na Kuwataka Wananchi Kudai Risiti.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Zanzibar, ikiwa ni mkutano wake wa kila mwisho wa mwezi kuzungumza na Wahariri na Waandishi wa habari,mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 31-5-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza matumizi ya mashine ya EFD katika ukusanyaji kodi, sambamba na kuwataka wananchi kudai Risiti wanapofanya manunuzi, ili kuiwezesha Serikali kukabiliana na hali ya kiuchumi.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu jijini Zanzibar, katika mkutano na Waandishi  wa Vyombo mbali mbali vya habari hapa nchini, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu wake wa kukutana na Wahariri na waandishi wa habari kila mwisho wa mwezi.

Alisema katika kukabiliana na athari zilizotokana na misukosuko ya Kiuchumi Duniani, Serikali  imelazimika kupunguza kiwango cha ushuru  pamoja na kufidia viwango vya bei za bidhaa, hivyo akabainisha umuhimu wa kukusanya kodi na kusisitiza matumizi ya mashine ZA Risiti za Kielektronik (EFD) sambamba na wananchi kudai risiti wakati wanapofanya manunuzi.

Alizitaka mamlaka zinazohusika kuchukua hatua stahiki kwa wananchi wasiolipa ushuru kupitia mashine hizo za VFB.

Aidha, alisema kuna umuhimu kwa wananchi wa Zanzibar kuongeza uzalishaji wa kilimo cha Karafuu, kwa kigezo kuwa pamoja na misukosuko ya kiuchumi Duniani, zao hilo limeBAKI kuwa na bei nzuri katika soko la Dunia (US dola 7,500 kwa tani), kiasi cha kimeiwezesha Serikali kuwalipa wakulima kiwango cha bei za kawaida.

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali imefikia uamuzi wa kuridhia kupanda kwa nauli ya Boti kutoka shilingi 25,000 hadi 30,000 (kwa usafiri wa daraja la chini) kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam kwa kuzingatia maombi ya muda mrefu ya wamiliki wa vyombo hivyo,(takriban miaka saba sasa), huku bei ya mafuta ikipanda katika kipindi hiki.

Akigusia suala la upandishaji wa mishahara kupitia sekta binafsi, Dk. Mwinyi alisema Serikali inakusudia kukaa pamoja na waajiri wa sekta hiyo ili kuona namna ya kuwapandishia mishahara wafanyakazi wao ili waweze kumudu gharama za maisha.

Kuhusiana na changamoto ya uharibifu wa mazingira unaovikabili visiwa vya Unguja na Pemba, Dk Mwinyi alisema kuna tatizo kubwa hususan katika suala la uchimbaji wa mawe, uchimbaji mchanga pamoja na ukataji mikoko na hivyo akabainisha kuwepo kwa mikakati ya kuikabili hali hiyo.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi Kisiwani Pemba ambao maeneo yao yalipimwa kwa ajili ya matengenzo ya barabara ya Chake- Wete na kubainika kutokuwa na  matatizo, kuwa watalipwa mara moja. 

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.