Habari za Punde

Kikosi kazi cha kutoa mapendekezo ya mageuzi ya elimu chaundwa

 Na Khadija Khamis –Maelezo  Zanzibar .20/05/2022.

Waziri wa Elimu na Mambo ya Kale Mhe Lela Muhamed Mussa amesema Wizara ya elimu imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya mageuzi ya elimu ili kuondoa changamoto za elimu nchini .

Amesema kikosi hicho kitajumuisha wataalamu tisa ambacho kitafanyakazi kwa muda wa miezi miwili na kutoa mapendekezo kupitia tafiti mbali mbali ikiwemo midahalo na makongamano jambo ambalo litasaidia kuimarisha sheria za elimu na kuondoa  changamoto zilizopo kwa kuleta mageuzi ya kielimu .

Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni , wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali kuhusiana na kipaumbele cha wizara ya elimu na mafunzo ya amali .

Aidha alisema sekta ya elimu kwa mwaka 2022/2023 imepitisha bajeti ya jumla ya Tsh . 309,815,073,000/- bajeti ambayo sawa na asilimia 16.7 ukilinganisha na bajeti ya mwaka uliopita ya jumla ya Tsh .265,549,743,000/ bajeti ambayo itasaidia Wizara kufanya mabadiliko makubwa ya sekta ya elimu kwa lengo la kutatua changamoto zitazoikabili sekta hii kwa kutekeleza mipango yanayoendana na mahitaji halisi ya nchi na wananchi wake  .

Alisema kuwa atahakikisha kuyasimamia matumizi ya fedha hizo kwa kutatua kero za wananchi kupitia kipaumbele cha wizara ya elimu kama inavyoelekeza .

Alieleza kuwa miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa ni kuajiri wafanyakazi wapya wakiwemo walimu waliojitolea kuanzia mwaka 2018 na kurudi nyuma  , kuzipatia ruzuku za fedha Skuli zote za Serikali zikiwemo za Maandalizi, Msingi na Sekondari kwa ajili ya gharama za uendeshaji .

Alifahamisha Wizara itasimamia ununuzi wa vitabu kwa ajili ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu ya maandalizi na msingi pamoja na kuwapatia mafunzo walimu wote wa maandalizi na msingi kufuatia kukamilika kwa mitaala mipya ya elimu ya maandalizi na msingi .

Vile vile Wizara ya Elimu itasimamia kuimarisha miundombinu kwa kujenga skuli 12 madarasa mapya 50 na kukamilisha madarasa 50 yalioanzishwa kwa nguvu za wananchi  kwa Unguja na Pemba ili  kupunguza msongamano wa wanafunzi  .

Alisema wizara itasimamia ujenzi wa karakana za elimu ya amali kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum  katika skuli ya elimu mjumuisho pamoja na kuendeleza programu ya lishe katika skuli za msingi 42 zilizo katika mazingira magumu

Pamoja na hayo wizara pia itatoa elimu kwa walimu wa sekondari, kujenga maabara katika skuli 10 za sekiondari kwa lengo la kuimarisha elimu ya sayansi ,kujenga vyuo vitano vya elimu ya amali, na kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu .

Hata hivyo Waziri lela amewahimiza wanafunzi na Wananchi kiujumla kutoa ushirikiano katika zoezi muhimu la  sense ya watu na makaazi linalotarajiwa kufanyika mwezi august mwaka huu wa 2022 zoezi ambalo litaiwezesha nchi kujua ya watu wake na mazingira yao wanayoishi ili iweze kuandaa mipango na mikaakati sahihi inayoandamana na mahitaji yakiwemo ya elimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.