Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Akizundua Mpango wa Utalii kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akionesha kitabu cha Muongozo wa mchango wa Utalii katika Pato la Taifa mara baada ya kuuzindua mchango huo katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Jijini Zanzibar.

Waziri wa Utalii na Mambo ya kale Mhe. Simai Mohamed Said akieleza namna mchango wa Utalii katika Pato la Taifa katika hafla ya uzinduzi wa mchango huo uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Jijini Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitoa nasaha zake kwa Viongozi na Wadau mbali mbali wa utalii wakati wa uzinduzi wa mchango wa utalii katika Pato la Taifa- Zanzibar  hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Na.Abdulrahim Khamis

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kwa dhati kuiendeleza Sekta ya Utalii na kuongeza thamani na ubora ili kuendelea kukuza uchumi wa Nchi.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza hayo kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katka hafla ya uzinduzi wa mchango wa utalii katika pato la Taifa Zanzibar iliyofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa ndege Jijini Zanzibar.

 

Amesema Serikali ya Awamu ya Nane ina jukumu la Kuendeleza vivutio mbali mbali vya kitalii hasa kupitia uchumi wa Buluu ambapo rasilimali za bahari zitatumika ipasavyo kwa ajili ya kuendeleza Sekta hiyo ikijumuisha ujenzi wa Mahoteli na mikahawa.

 

"Msisitizo Mkubwa wa Serikali ni kuendeleza Uchumi wa Buluu Hii itajumuisha Ujenzi wa Mahoteli na Mikahawa na tutatumia Fukwe na bahari kwa ajili ya michezo ya Utalii kama vile soka ka Fulwell na resi za Ngalawa"

 

Aidha Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa uzinduzi wa zana hiyo inaonesha wazi jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyothamini na kuiendeleza Sekta ya Utalii kwa kuwa ndio Uti wa mgongo wa Uchumi wa Zanzibar.

Pia Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameleza kuwa uwepo wa utoaji wa takwimu sahihi katika Sekta mbali mbali za Kiuchumi itasaidia kufikia malengo ambayo Serikali imejiwekea ili kuweza kuendana na Maendeleo endelevu.

 

Aidha ameeleza kuwa Nchi nyingi zinazoendelea na hasa zilizo kusini mwa Janga la Sahara kuna tatizo la utoaji wa Takwimu Sahihi jambo ambalo linasababisha uzorotaji wa maendeleo katika sekta mbali mbali.

 

Sambamba na hayo Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Kamisheni ya Utalii na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu na Taasisi nyengine kuendeleza tafiti zao katika utengenezaji wa Mifumo kwa lengo la kupata mchango halisi wa Utalii Zanzibar.

 

 Aidha ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inaziwezesha Taasisi husika ili kuweza kuhakikisha mahitaji ya uendelezaji wa Mfumo huo yanapatikana kwa wakati.

 

Nae Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Simai Mohamed Said ameeleza kuwa Mfumo huo ulianzishwa na Shirika la Utalii Duniani kwa lengo la kupata Takwimu sahihi za kitalii ili kusaidia kupima pato la Utalii.

 

Mhe. Simai ameeleza kuwa kazi kubwa ya Zana hiyo ni kuchambua kwa undani nyanja zote za mahitaji ya Utalii ikiwemo bidhaa na huduma zinazohusiana na Shughuli za wageni.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Bwana Rahim Bhaloo ameeleza kuwa zana hiyo itasaidia kuzalisha ajira kwa wananchi na wawekezaji na kupelekea Serikali kuweza kufikia malengo iliyojipangia.


Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

06/05/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.