Habari za Punde

Waziri Dkt.Mabula Aadhimisha Miaka Sitini ya Kuzaliwa Kuchangisha Milioni 41.6 za Masomo.

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dkt Angeline Mabula (wa pili kushoto) akiwa ameshika bilauri ya Mvinyo wakati wa kuadhimisha miaka sitini na kuzaliwa kwake jijini Dodoma tarehe 6 Mei 2022. Kushoto ni Askofu wa Jimbo la Mtwara Titus Mdoe na Kulia ni aliyekuwa katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Queen Mlozi.

Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara Titus Mdoe akizungumza wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka sitini ya kuzaliwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dkt Angeline Mabula jijini Dodoma.

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameadhimisha miaka sitini ya kuzaliwa kwake kwa kuchangisha fedha shilingi milioni 41,616,500/- za kugharamia masomo kwa wanafunzi wenye uhitaji.

Aidha, ameitaka jamii kuangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi wenye uwezo wa kimasomo lakini wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo za kifedha.

Maadhimisho hayo yamefanyika 6 Mei 2022 mkoani Dodoma kwa Waziri Dkt Mabula kushiriki Misa Takatifu kwenye Kanisa la Parokia ya Kiwanja cha Ndege na kufuatiwa na chakula cha hisani kilichofanyika Hoteli ya ST Gasper.

‘’Tukiwa na utaratibu wa kuasaidia basi tutakuwa tumewasaidia wanafunzi wengi wenye uwezo wa kimasomo lakini wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifedha’’ alisema Dkt Mabula.

Alisema, lengo la kuitumia siku yake ya kutimiza miaka sitini ya kuzaliwa kwake kuchangisha fedha ni kutaka kuwanufaisha wanafunzi kwenye taaluma mbalimbali na kutaka kila mtu kutoa michango kulingana na alivyoguswa.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara Titus Mdoe alimsifu Dkt Mabula kwa uamuzi wake wa kutoa shukurani kwa Mungu kwa zawadi ya uhai aliyoipata kufikisha miaka 60 sambamba na uamuzi wa kuchangisha fedha za kusaidia masomo jambo alilolieleza kuwa ni uamuzi wa busara.

‘’Mama ana jambo lake naye ni mpenzi wa masikini wa roho na mali ndiyo maana umechagua kuwasaidia masikini, vijana wanaokosa pesa za ada lakini umeamua kushiriki kutafuta pesa za kuwasaidia’’ alisema Askofu Mdoe.

Askofu Mdoe alibainisha kuwa, wapo vijana wengi waliopo vijijini lakini wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na hali ya wazazi wao jambo lililomsukuma Waziri Dkt Mabula kuja na wazo la kuchangisha fedha wakati wa misa ya kusheherekea kutimiza miaka sitini ya kuzaliwa.

Baadhi ya wanafunzi walionufaika na mfuko huo wa kichungaji walieleza kuwa, mfuko huo umekuwa ukitoa fursa za kimasomo kwa wale wanafunzi wanaotoka familia za kimasikini.

Thomas Kichenje anayesoma Stashada ya Utawala wa Biashara Chuo cha STeMMUCo Mtwara alisema, bila ya ufadhili wa mfuko wa kichungaji asingekuwa chuoni hapo kwani baada ya kuomba vyuo kadhaa alikosa ufadhili.

Mwanafunzi mwingine Frank Kiwanga anayesomea masomo ya sheria chuo cha SAUT Mtwara alieleza kuwa, alikosa mkopo wa elimu ya juu mara nne lakini kupitia msaada wa mfuko wa kichungaji ameweza kusoma shahada hiyo.

Maadhimisho ya kutimiza miaka 60 ya kuzaliwa Dkt Mabula kwa kuchangisha fedha yamefanyika pia katika mikoa ya Mbeya, Mwanza na Mtwara. Uchangiaji wa mfuko huo unafanyika kwa wananchi kununua kadi za kuchangia, udhamini wa wanafunzi, mchango wa hisani kupitia chakula ambapo fedha zinazochangwa hutumika kulipia gharama za Bweni,  Ada , Bima pamoja na Mafunzo ya Vitendo.

 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dkt Angeline Mabula (wa tatu kushoto) akiongoza zoezi la kula keki wakati wa kuadhimisha miaka sitini ya kuzaliwa kwake jijini Dodoma
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dkt Angeline Mabula (wa tatu kushoto) na viongozi wengine wakinyanyua bilauri yenye mvinyo wakati wa kuadhimisha miaka sitini ya kuzaliwa kwake jijini Dodoma
aibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Ridhiwani Kikwete (Katikati), Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Allan Kijazi (Kulia) wakifurahia jambo wakati wa kuadhimisha miaka sitini na kuzaliwa Dkt Angeline Mabula jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Ridhiwani Kikwete akitetea jambo na Waziri wake Dkt Angeline Mabula wakati wa kuadhimisha miaka sitini na kuzaliwa Dkt Mabula jijini Dodoma
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Isimani mkoani Iringa Mhe. William Lukuvi akizungumza wakati kuadhimisha miaka sitini na kuzaliwa Mhe.Dkt Angeline Mabula jijini Dodoma
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati kuadhimisha miaka sitini na kuzaliwa kwake jijini Dodoma tarehe 6 Mei 2022. Kushoto ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara Titus Mdoe.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dkt Angeline Mabula (Kulia), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama (kushoto) na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Queen Mlozi wakiwa kwenye Misa Takatifu Parokia ya Kiwanja cha Ndege Dodoma wakati wa kuadhimisha kutimiza miaka sitini ya kuzaliwa Dkt Mabula

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.