Habari za Punde

Azma ya SMZ Kuhakikisha hadi Kufikia Mwaka 2025 Uchumi wa Pemba Umeimarika Kama Ulivyo Unguja. Dk. Hussein Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Watendaji wa Mkoa wa Kaskazini Pemba katika mkutano wake wa majumuisho ya ziara yake kukagua Miradi ya Maendeleo katika Mkoa huo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2025 uchumi wa Pemba unaimarika kama ulivyo wa Unguja.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akitoa majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Kaskazini Pemba mara baada ya kukamilisha ziara yake hiyo huko katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua za Serikali za kuifanya Pemba kuwa eneo maalum la uwekezaji na kusema kwamba muitikio ni mzuri na tayari wameshajitokeza wengi kuja kuekeza.

Alieleza azma ya Serikali ya kujenga kiwanja cha ndege cha Pemba, mradi wa barabara ya Wete Chake pamoja na barabara ya Chake hadi Mkoani huku akieleza hatua za ujenzi wa barabara za ndani.

Rais Dk. Mwinyi aplipongeza maanadalizi mazuri ya ziara yake hiyo huku akisema kwamba maanadalizi ya ziara hiyo ni kukagua miradi ya maendeleo, miradi maalum inayotokana na ahuweni ya UVIKO-19 pamoja na kuhakikisha kwamba Ilani ya CCM inatekelezwa.

Alipongeza amani iliyopo kisiwani Pemba na kuwapongeza wananchi wa Pemba kwa hatua yao hio na kueleza kwamba kumeundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili wananchi waweze kuishi kwa amani, umoja na upendo.

Alipongeza hatua za uongozi wa Mkoa huo unavyosimamia miradi ya maendeleo katika maeneo mbali mbali ya Mkoa huo.

Rais Dk. Mwinyi alilitaka Baraza la Mji la Wete na Halmashauri ya Micheweni zijipange vizuri katika makusanyo na matumizi kwani fedha nyingi zaidi ziwekwe katika miradi ya maendeleo ili wananchi waweze kupelekewa maendeleo.

Alisema hatua hiyo inaweza kufanywa vizuri kutokana na kupungua kwa majukumu kutokana na kuondoa ugatuzi na kusisitiza kwamba Mabaraza ya Mji na Halmashauri ya Micheweni bado wanatakiwa kujikushanya vizuri kimapato.

Alisema kuwa kwa upande wa sekta ya afya, ameridhika na ujenzi wa hospitali za Wilaya ya Wete na Micheweni huku akisisitiza kwamba ni vyema hivi sasa wakajipanga vizuri katika kuhakikisha vifaa tiba vinafika kwa wakati ili viweze kufungwa na wananchi wakapata huduma, kujipanga katika ajira pamoja na kuweka mfumo bora wa kutoa huduma za afya.

Alisema kwamba haitokuwa busara kuwa na majengo mazuri lakini huduma zikawa mbovu huku akiwakumbusha kwamba majengo hayo mapya yanayojengwa yanahitaji huduma za maji, umeme na barabara zinazoelekea katika hospitali hizo pamoja na uzio huku akiwataka kupanga bajeti ya ziada.

Akieleza kuhusu fidia, Rais Dk Mwinyi alileza haja ya kuweka orodha ya madai ya fidia na kulepelekwa Wizara ya fedha kwani tayari ameshatoa maelekezo ili watu wapewe stahiki zao  na kuipa mda serikali kufanya mambo mengine.

Alieleza kuridhika kwake na ujenzi wa miradi ya skuli na kusema kwamba kasi hiyo ikiendelezwa mafanikio makubwa yatapatikana huku akiusifu Mkoa huo kwa kufanya vizuri katika masomo yao kwa mara ya tatu mfululizo.

Alisema kwamba Serikali itaendelea kufanya vizuri ili vijana nao kwa upande wao waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.

Alitumia fursa hiyo kukipongeza kikosi cha KMKM na kusema kwamba vikosi vyote vya SMZ alivyowapa kazi Unguja na Pemba vinafanya vizuri.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliiigiza Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni kuja na programu maalum ya ujenzi wa viwanja vya kisasa katika maeneo mbali mbali nchini na kusema kwamba haitoshi kuwa na skuli wakakosa sehemu za michezo.

Aliitaka Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na sekta husika ikiwemo Mkoa na Wilaya kuhakikisha inayapima maeneo ya Serikali kwani kuna maeneo mengi watu wanayavamia yakiwemo ya skuli na vituo vya afya.

Kwa upande wa sekta ya afya, Rais Dk. Mwinyi alileeza azma ya Serikali ya kujenga matangi 10 yenye lita milioni moja kwa kila moja ambapo kwa upande wa Pemba yatajengwa matangi matano na Unguja matano.

Alisisitiza haja ya kulindwa kwa miundombinu ya maji huku Serikali ikitafuta fedha za ziada ili kukamilisha zile sehemu ambazo bado hazipati maji.

Aliwataka Wakuu wa Wilaya, Mkoa na Wizara kufuatilia ujenzi wa matangi kwa kila wiki ili wajenzi waweze kutekeleza miradi hiyo kwa wakati na kuwataka wakandarasi kukabidhi matangi hayo mwezi Disemba kama walivyoahidi.

Aliipongeza benki ya CRDB kwa kufungua tawi la benki hiyo huko Wete Mkoa wa Kaskani Pemba huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa na benki hiyo baada ya makubaliano na Serikali kwa kuzifikisha vyema fedha za UVIKO-19 kwa wajasiriamali kwa utaratibu mzuri kama ilivyoagizwa na serikali.

Alieleza hatua ambayo inatakiwa ya kuzalisha zaidi umeme kwani umeme ulioko hivi sasa kisiwani humo ni mdogo hasa ikizingatiwa kwamba maendeleo yanaimarika kila uchao.

Rais Dk. Mwinyi alieleza uwamuzi wake sambamba na kuweka mkazo maalum wa kuwapekeea maendeleo wananchi wa visiwani.

Akitoa mfano kwa kisiwa cha Kojani na Tumbatu, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba tayari amezitaka Wizara husika zikiwemo Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Wizara ya Habari pamoja na wizara nyenginezo kuhakikisha zinawapelekea huduma husika katika visiwa hivyo.

Kwa ujula, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuridhika kutokana na maeneo yote aliyopita na kueleza kwamba Mkuu wa Mkoa pamoja na Wakuu wa Wilaya bado kazi wanayo kutokana na uchapakazi wao mzuri.

Mapema Rais Dk. Mwinyi aliweka jiqwe la Msingi katika hospitali ya Wilaya ya Micheweni pamoja na kufika uwanja wa Shaame Matta kwa kukagua shughuli za wajasiriamali waliopatiwa Mkopo wa fedha za UVIKO-19 na kupokea maoni ya wajasiriamali na hatimae kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na wanachi wakiwemo wajasiriamali katika uwanja huo, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Serikali imeeanza kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wajasiriamali zikiwemo elimu, mitaji, dhana na mazingira mazuri ya kufanya biashara zao na kusema kwamba Ilani ya uchaguzi imetekelezwa kwa vitendo.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano.

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.