Habari za Punde

Maulidi ya Kusherehekea Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) Madrasatul Swifatu Nabawiyyatil Karima Kilimani kwa Msolopa Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhaj Hemed Suleiman Abdulla akishiriki katika kuitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi baada ya kumalizika kwa Maulidi ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtumu Muhammad (SAW) yalioandaliwa na Madrasatu Swifatu Nabawiyyatil Karima (Kwa Msolopa) Kilimani Jijini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akitoa salam kwa niaba ya Rais wa zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi  Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Hafla ya kusherehekea Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) iliyoandaliwa na Madrasatu Swifatu Nabawiyyatil Karima (Kwa Msolopa) Kilimani Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepongeza juhudi zinazofanywa na Madrasatu Swifatu Nabawiyyatil Karima (kwa Msolopa)  katika kuzalisha wasomi wanaoendeleza Elimu ya Dini ya Kiislamu Nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza hayo katika Salamu zilizotolewa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla katika Hafla ya kusherehekea Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) iliyoandaliwa na Madrasatu Swifatu Nabawiyyatil Karima (Kwa Msolopa) Kilimani Jijini Zanzibar.

Ameeleza kuwa Elimu inayotolewa Chuoni hapo inaakisi Mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwa kuwafundisha Vijana Tabia njema jambo ambalo litasaidia kurejesha Mila na Tamaduni za Uislamu.

Amesema Uislamu umeweka wazi namna bora ya kuishi Duniani kuhusu masuala ya Ibada na  Malezi bora jambo ambalo kila Muumini akisimamia misingi ya Dini atafanikiwa Duniani na Akhera.

Alhajj Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Kitabu kitukufu cha Qur-ani pamoja na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) zimeeleza namna bora ya kuishi ambapo Muumini akishikamana navyo watawalea watoto katika makuzi mazuri.

Aidha Mhe. Rais Dkt. Mwinyi amesema makuzi mazuri yatapelekea kupunguza matendo maovu yanayokithiri Nchini ambayo yanaipa sifa mbaya Zanzibar.

Sambamba na hayo amewakumbusha walimu wa Madrasa hiyo kutovunjika moyo kwa changamoto wanazokumbana nazo wanaposomesha vijana na kuwataka kuukuza umoja wao ili kuiendeleza Madrasa hiyo iweze kutoa zaidi vipaji vitakavyoendeleza Uislamu Zanzibar.

Nae Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar  Zubeir Bin Aly amewakumbusha waumini wa Dini ya Kiislamu kuwa maendeleo mengi Duniani yamechangiwa na Uislamu na kuwataka waislamu kuzidi kusoma ili kuendana na maendeleo ya Dunia ya sasa.

Aidha ameeleza kuwa wapo wanazuoni wengi waliokuwa na fani tofauti ambao walikuwa ni tegemezi kwa zama zao akimtolea Mfano Shekh Ibnu Syna ambae alikuwa Daktari Mkubwa aliesaidia jamii yake kwa zama alizoishi.

Akisoma Risala ya Madrasa hiyo Sheikh Omar Ahmed Mcheju ameeleza kuwa Madrasa hiyo tokea kuasisiwa kwake imekuwa ikitoa Elimu mbali mbali za Dini ikiwemo Qur-ani, Fiqhi, Hadithi na  fani mbali mbali.

Vile vile,  amesema walimu wa Madrasa hiyo wamekuwa wakijitolea kusomesha licha ya changamoto wanazokumbana nazo hasa kukosa sehemu ya kujipatia Rizki na kuziomba Mamlaka husika kuwasaidia Walimu hao kwa kuwafundisha  ujasiriamali pamoja na kuwawezesha ili kujikwamua kiuchumi.


Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

25/12/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.