Habari za Punde

CDE.Mbeto - Akipogenza Kikosi Maalum cha KMKM kwa Kukamata Shehena ya Mchele wa Magendo

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis pamoja na Makamanda wa Kikosi cha KMKM,wakizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya jahazi juu ya tukio la Kikosi cha KMKM kukamata Mchele wa magendo, huko katika Bandari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis pamoja na Makamanda wa Kikosi cha KMKM,wakizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya jahazi juu ya tukio la Kikosi cha KMKM kukamata Mchele wa magendo, huko katika Bandari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Kikosi Maalum cha KMKM Commodore Azani Msigiri Hassan, wakiwa katika maeneo ya bandari ya Mkokotoni mara baada ya kukagua jahazi lililokamata na bidhaa za magendo ya mchele uliokuwa ukisafirishwa kwenda Mkoani Tanga.

(Picha na Abeid Machano-Afisi Kuu ya CCM Zanzibar).

Na Is-haka Omar - Zanzibar.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndg.Khamis Mbeto Khamis,amekishauri Kikosi Maalum cha kuzuia magendo (KMKM) kuongeza nguvu katika kudhibiti vitendo vya uhalifu baharini vikiwemo usafirishaji wa bidhaa za vyakula na rasilimali zingine kwa njia ya magendo.

Rai ameitoa katika ziara yake ya kukagua Jahazi lenye shehena ya magendo ya mifuko ya mchele lililokamatwa jana na Kikosi hicho karibu na cha   Kisiwa kidogo cha Tumbatu Zanzibar.

Ndg. Mbeto alikitaka kikosi hicho kujiimarisha zaidi kwa kufanya doria za mara kwa mara na kuimarisha kitengo chake cha kiintelijensia ili kupata taarifa sahihi za uhalifu na kuzifanyia kazi kwa haraka.

Kupitia ziara hiyo Katibu huyo wa Kamati Maalum ya NEC Ndg. Mbeto, alikipongeza Kikosi hicho kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kukamata jahazi hilo lililokuwa na shehena kubwa ya mchele ambao ni zaidi ya mifuko 130 iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea Mkoani Tanga.

Alisema Zanzibar kwa sasa ipo katika changamoto ya kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula hasa Mchele wakati kuna baadhi ya wafanyabisha wachache kwa kuendekeza tamaa wanasafirisha bidhii hizo kwa njia ya magendo nje ya Zanzibar.

Kupitia ziara hiyo alikisihi kikosi kwenda mbali zaidi kwa kushughulikia vitendo vyote vya uhalifu vinavyofanyika baharini vikiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya,karafuu,mazao ya baharini na rasilimali zingine zinazosafirishwa kimagendo.

 Mbeto alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi kwa sasa kipo kazini kuhakikisha kinafuatilia kwa kina utekelezaji wa Ilani yake ya mwaka 2020/2025, hivyo hakitoweza kuvumilia vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watu wachake.

Katika maelezo yake Mbeto, aliiomba mamlaka inayohusika na kudhibiti wafanyabishara wanaokwepa kodi za nchini za kujihusisha na vitendo vya uhalifu kuchukuliwa hatua za kisheria.

“ Nachukua nafasi hii kuwambia wananchi kuwa bidhaa za vyakula nchini zipo lakini kuna kundi la baadhi ya wafanyabishara wanahujumu Serikali kwa kusafirisha bidhaa hizo nje ya Zanzibar ikiwemo Tanga,Kenya na Msumbiji”, Alisema Mbeto.

Alitoa wito kwa wafanyabisha nchini kufuata sheria na kuwaonea huruma wananchi ambao ndio wanaoumia zaidi kutokana na kushindwa kumudu bei ya vyakula pale inapopandishwa bila utaratibu.

Pamoja na hayo Katibu Mbeto, alisema CCM itashirikiana na taasisi zote za umma na binafsi ili kuhakikisha ili kuhakikisha wananchi waliotoa ridhaa ya kuongoza Dola wanaondokana na changamoto na kupata maendeleo endelevu.

Naye Mkuu wa Kikosi hicho cha KMKM Zanzibar Commodore Azana Msigiri Hassan, aliahidi kupambana kikamilifu na baadhi ya watu wanaofanya uhalifu katika maeneo yote ya bahari.

Alisema atakuwa mstari wa mbele kulala baharini akiwasaka watu wanaofanya biashara za magendo ambazo ni kinyume cha sharia za nchi na wanaikosesha serikali mapato.

“Nakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na sisi katika haya mapambano yanayotokana na maelekezo ya Mkuu wa Kikosi chetu ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Hivi vitendo vya magendo vinatekelezwa na watu wachache ambao ni sehemmu ya wananchi hivyo natumia nafasi hii kuwaonya waache magendo na watafute shughuli halali kwani tutakayemkamata hatoweza kukwepa mkono wa sheria.”, alisema Commodore Msigiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni za KMKM Kanda ya Kaskazini Unguja kamanda Ame Rashid Masema, alisema wamepata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa jahazi hilo lenye jina la ‘Bora imani’ lilikuwa na bidhaa za magendo mifuko 130 pamoja na watu wanne.

Siku za hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Dk. Hussein Ali Mwinyi aliingilia kati tatizo la kupanda kwa bei ya vyakula nchini ambapo Chama Cha Mapinduzi nacho kilichukua hatua ya kukagua maeneo ya maghala ya chakula pamoja na bandarini na kuwataka wafanyabiashara kuwa waadilifu na kupunguza bei za bidhaa hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.