Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia, ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab (kushoto) akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika jijini Windhoek, Namibia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023. Kulia, ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Namibia, Balozi Penda Naanda.
Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma
Rajab (wa pili kutoka kushoto walioketi), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa
Namibia, Balozi Penda Naanda (watatu kutoka kushoto walioketi), Balozi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Dkt. Modestus Kipilimba
(wa kwanza koshoto walioketi), Balozi wa Jamhuri ya Namibia nchini Tanzania,
Mhe. Lebius Tobius katika picha ya pamoja na Makatibu Wakuu na Maafisa
Waandamizi wa Serikali ya Tanzania na Namibia wakati wa Mkutano wa Tatu wa Tume
ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia, ngazi ya Maafisa
Waandamizi unaofanyika jijini Windhoek, Namibia.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Jamhuri ya Namibia zimesisitiza kuweka mikakati imara ya ushirikiano
itakayoimarisha mfumo wa utendaji kazi kwa lengo la kukuza na kuendeleza
Diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya nchi hizo pamoja na watu wake.
Msisitizo huo umetolewa katika hafla ya ufunguzi wa
Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) kati ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Namibia unaofanyika Jijini Windhoek, Namibia
kuanzia tarehe 8 hadi 10 Machi 2023.
Akifungua mkutano huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye pia ni kiongozi wa
ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa JCC kati ya Tanzania na Namibia
kwa Ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab ameeleza kuwa Tanzania
itaendelea kuweka mikakati imara ya ushirikiano na kukuza uchumi kati yake na
Namibia ili kuuenzi ushirikiano wa kidugu na kihistoria uliopo baina ya nchi
hizo.
Balozi Fatma ameongeza kuwa ushirikiano huo
uliasisiwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na waasisi
wa mataifa hayo mawili, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Namibia,
Hayati Dkt. Samuel Daniel Nujoma.
“Ni matumaini yangu mkutano huu utatuwezesha
kusaini makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya anga ili kurahisisha uwepo
wa safari za moja kwa moja baina ya nchi zetu na kuwezesha uendeshaji wa
shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu” alisema Balozi Fatma.
Vilevile, Balozi Fatma alieleza kuwa kupitia fursa ya majadiliano ya mkutano huo Tanzania na Namibia zitafungua maeneo mapya ya ushirikiano ambapo, kwa upande wa Tanzania tayari imewasilisha mapendekezo ya makubaliano ya ushirikiano kwa Namibia katika sekta za ulinzi, biashara na uwekezaji, nishati na majadiliano ya kisiasa na diplomasia ambazo makubaliano yakikamilika zitarasimishwa na kusainiwa katika mkutano wa ngazi ya Mawaziri utaofanyika tarehe 10 Machi 2023 jijini Windhoek, Namibia.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje
wa Namibia ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza katika mkutano huo, Balozi Penda
Naandi ameeleza kuwa takwimu za biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na
Namibia bado ni ndogo, hivyo mkutano huo utaweka mikakati madhubuti ya
kuhakikisha ushirikiano huo unaleta maendeleo ya kiuchumi na kuinua maisha ya
wananchi wa pande zote mbili.
“Nchi zetu zinashirikiana katika sekta za kiuchumi
ambazo zinatuwezesha kuingia kwenye soko la ushindani katika Eneo Huru la
Biashara Afrika (AfCFTA) na kuinua uchumi wa kikanda pamoja na kufikia malengo
ya maendeleo endelevu kwa watu wake” alisema Balozi Naanda.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utapitia,
kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala
mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa pili uliofanyika
mwezi Desemba 2019 Jijini Dar es salaam, Tanzania.
Tanzania na Namibia zinashirikiana katika sekta za
Diplomasia, Siasa, Ulinzi, Uvuvi na Rasiliamali za Bahari, Kilimo, Maji,
Maendeleo ya Miji, Madini, Nishati, Biashara, Uwekezaji, Mazingira, Utalii na
Maliasili, usafiri, Afya, Utamaduni na Elimu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.
No comments:
Post a Comment