Habari za Punde

Haki za Binadamu na Biashara Zajadiliwa

Naibu Mwakilishi UNDP Zanzibar Godfrey Nyamrunda akitoa salamu za shirika hilo wakati wa mkutano wa kujadili mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara uliowashirikisha watendaji mbalimbali wa SMT na SMZ uliofanyika Ukumbi wa Takwimu Mazizini Zanzibar.

Na.Idara ya Maelezo Zanzibar.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema pamoja na uwepo wa sheria, sera , mipango mbalimbali na ushirikiano thabiti miongoni mwa wadau lakini bado kuna changamoto za utekelezaji wa haki za binaadamu katika sekta ya uwekezaji na biashara nchini.

Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar, Kubingwa Mashaka Simba, alieleza hayo wakati akifungua mkutano ulioshirikisha wadau wa SMT na SMZ wenye lengo la kujadili mchakato wa kuandaa mpango kazi wa haki za binaadamu na biashara uliofanyika katika ukumbi wa Takwimu Mazizini.

Alisema changamoto kubwa ya utekelezaji wa haki za binaadamu katika shughuli za biashara zinatokana na ufahamu mdogo wa masuala hayo miongoni mwa wadau na kutokuwepo kwa uratibu wa pamoja wa masuala ya haki za binaadamu na biashara inayosababishwa na kutokuwepo kwa mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara.

Alidha alisema serikali kupitia Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Mei 6 mwaka 2022 ilikutana na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala bora kujadili kuhusu mkakati wa kuondoa changamoto hizo katika shughuli za uwekezaji na biashara ambapo wazo la kuwepo kwa mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara lilijadiliwa.

“Tume ya Haki za binaadamu na Uwatala bora na Wizara ya Shetia na Katiba Tanzania bara zilipewa ridhaa ya kuanzisha na kuongoza mchakato wa kuandaa mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara,” alisema.

Alisema serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha haki za binaadamu, zinalindwa, zinatetewa na kuhifadhiwa katika utekelezaji wa shughuli za uwekezaji na biashara.

Katibu alisema ukuaji wa shughuli za uwekezaji na biashara unaenda sambamba na mahusiano baina ya uwekezaji, biashara na utekelezaji wa haki za binaadamu.

Alisema mara nyingi shughuli za biashara na uwekezaji zimekuwa zikilaumiwa kusababisha uvunjwaji wa haki za biaadamu.

“Uvunjwaji wa haki za binaadamu unaolalamikiwa zaidi katika sekta ya utalii hasa haki za kazi na viwango vya ajira,fidia isiyo ya haki kwa watu wanaochukuliwa ardhi zao kwa ajili ya shughuli za uwekezaji, kunyanganywa vifaa vya uvuvi na vyombo vya dola wakati wa operesheni baharini, ukiritimba katika upatikanaji wa vibali vya uwekezaji na mengineyo,” alisema.

Alibainisha kuwa serikali imefanya jitihada kubwa kuvutia wawekezaji na shughuli za biashara na uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi kutokana na shughuli za biashara na uwekezaji hususan sekta ya utalii, usafirishaji, uvuvi na biashara kwa ujumla.

Aidha alisema jitihada nyengine hizo ni pamoja na kuanzisha Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na kutunga sheria ya taasisi hiyo namba 14 ya mwaka 2018.

Katibu Kubingwa alisema pia serikali imeandaa muongozo wa uwekezaji wa mwaka 2023 na sera mbalimbali za maendeleo ikiwemo sera ya ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi (Public- Private Partnership Policy),Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na sera ya Uchumi wa Buluu.

Alifahamisha kuwa ili kuhakikisha sheria, sera na mipango hiyo inateklezwa kwa ufanisi serikali inafanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa haki za binaadamu ikiwemo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vya siasa, vyama vya wafanyakazi, jumuiya ya wafanyabiashara jamii na tume ya haki za binaadamu na utawala bora.

Hivyo, aliwataka washiriki hao kutumia mkutano huo kama sehemu ya kujifunza na kujijengea uwezo kuhusu masuala ya haki za binaadamu na biashara na kushiriki kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu namna bora ya kuaanda mpango huo.

Naye, Mwenyeiti wa Tume ya Haki za binaadamu na utawala bora Tanzania bara, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, alisema mwaka 2011 muongozo wa kanuni za umoja wa mataifa wa haki za binaadamu ulioridhiwa ni nchi tisa tu za Afrika ambazo zimechukua hatua kuanzisha mchakato wa kuandaa mpango kazi wa kitaifa ikiwemo Kenya, Moroco, Liberia, Uganda, Ghana, Nigeria, Zambia, Msumbiji na Afrika Kusini.

Alisema katika nchi za Arika Mashariki nchi ya Kenya na Uganda zimeshaanza mpango huo na sasa zip katika hatua ya utekelezaji ambazo zimekuwa mfano bora kwa Tanzania katika kuanzisha mchakato wa kuandaa mpango kazi wa haki za binaadamu na biashara.

Akizungumzia baadhi ya faida za mpango huo alisema ni kuimarisha utamaduni wa kuheshimu haki za binaadamu katika shughuli za biashara, kuzuia na kupunguza vitendo vya uvunjwaji wa haki za binaadamu katika utelezaji wa shughuli za biashara na kuhamasisha maendeleo yanayozingatia haki za binaadamu.

Alisema muongozo huo wa kanuni umeweka jukumu kwa serikali kulinda haki za binaadamu, sekta ya biashara kuheshimu haki za binaadam na upatikanaji wa nafuu kwa waathirika wa uvunjwaji wa haki unaotokana na shughuli za biashara.

Mapema Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Godfrey Nyamronda, aliipongeza SMT na SMZ kuendeleza msukumo katika masuala ya haki za binaadamu na biashara nchini Tanzania.

Alisema bado kuna mengi ya kufanya katika kufikia haki za binaadamu na biashara hivyo aliiashauri serikali kuhakikisha inashirikisha wadau mbalimbali kwani mpango huo ni nguzo muhimu katika kufikia malengo 2030 na kuahidi kuwa UNDP itaendelea kushirikiana na serikali zote mbili katika michakato yote itakayopitia ili kupatikana kwa mpango huo.

Mwenyekiti Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Methew Mwaimu akizungumza katika mkutano wa kujadili mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara uliowashirikisha watendaji mbalimbali WA SMT na SMZ na kufanyika Ukumbi wa Takwimu Mazizini Zanzibar.
Katibu Kamisheni ya Utumishi wa Umma- Zanzibar Kubingwa Mashaka Simba akifungua mkutano wa wadau wa haki za Binadamu uliolenga kujadili mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara uliowashirikisha watendaji mbalimbali WA SMT na SMZ na kufanyika Ukumbi wa Takwimu Mazizini Zanzibar.
Mratibu wa miradi tume ya haki za binaadamu na  Utawala Bora Jovina mchunguzi akiwasilisha mada ya biashara na haki za binaadamu wakati wa kujadili mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara uliowashirikisha watendaji mbalimbali wa SMT na SMZ na kuifanyia Ukumbi wa Takwimu Mazizini Zanzibar.
Afisa kutoka Wizara ya kilimo umwagiliaji Mali asili na mifugo Rashid Khamis Rashid Akichangia mada katika mkutano wa kujadili mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara uliowashirikisha watendaji mbalimbali wa SMT na SMZ na kufanyika Ukumbi wa Takwimu Mazizini Zanzibar.
Wadau wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora wakiwa katika mkutano wa kujadili mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara uliowashirikisha watendaji mbalimbali wa  SMT na SMZ katika ukumbi wa Takwimu Mazizini Zanzibar.
Wadau wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora wakiwa katika mkutano wa kujadili mpango kazi wa kitaifa wa haki za binaadamu na biashara uliowashirikisha watendaji mbalimbali wa  SMT na SMZ katika ukumbi wa Takwimu Mazizini Zanzibar.
(Picha na Idara ya Maelezo Zanzibar)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.