Habari za Punde

Baraza la Manispaa Chake watakiwa kusimamia vyema mapato


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka uongozi wa  Baraza la Mji la Chake Chake Pemba ambalo limepandishwa hadhi na kuwa Baraza la Manispaa Chake Chake kuhakikisha wanasimamia vyema vyanzo na  ukusanyaji  mzuri wa mapato ili  kuweza  kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ameyasema hayo wakati akizindua Baraza la Manispaa Chake Chake Pemba katika Viwanja vya Tibirinzi  Pemba Mhe. Hemed ameipongeza Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kasi kubwa ya kuimarisha utendaji kazi katika Serikali za Mitaa na kuridhia mapendekezo ya kulipandisha hadhi Baraza la Mji Chake Chake na kuwa Baraza la Manispaa Chake Chake  Pemba kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

 Amesema kuwa matarajio ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Baraza hilo jipya litahakikisha huduma za kijamii zinakuwa bora na za ufanisi zaidi ambazo zitawaondolea usumbufu wananchi kwa kupata huduma hizo pamoja na kuandaa mipango bora ya kimkakati itakayotoa tija kwa Wananchi na Serikali kwa ujumla.

Aidha Mhe. Hemed amewasisitiza Watendaji wa Baraza la Manispaa Chake Chake kusimamia vyema makusanyo kwa kutumia mifumo ya risiti za kielektroniki, kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali watu na rasilimali fedha, kuibua Miradi mbali mbali ya maendeleo, kuimrisha usafi wa mazingira na kusimamia Amani na mshikamano katika jamii.

Amelitaka Baraza la Manispaa Chake Chake Pemba na watendaji wake kukemea vitendo vya rushwa na utumiaji mzuri wa rasilimali za Serikali, kuacha ,uhali na kutanguliza maslahi ya Taifa  ili kuwa Baraza la  mfano litakalotoa  hamasa wa ushindani wa kimaendeleo kwa kuongeza mapato Serikalini na kuzitumia fursa mbali mbali zinazopatikana katika Wilaya hiyo.

Ameutaka Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Kusini Pemba  kuwa na mipango shirikishi jamii kwa kuzishirikisha Kamati za mashauriano za Shehia na Mabaraza ya wadi, Kamati za Wilaya na Mikoa ili kupata mazingatio na ushauri katika maendeleo.

Sambamba hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa endapo Mabaraza ya Manispaa na Miji Zanzibar yatatekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Serikali za Mitaa yataleta matokeo mazuri yenye tija na kuepusha Migogoro katika jamii.

Pamoja na hayo amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuridhia Baraza la Mji la Chake Chake Chake kupandishwa hadhi na kuwa Baraza la Manispaa kumetokana na miongozo na maelekezo yake kwa watendaji wa Baraza hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Mohamed ameishukuru Serikali ya Awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuridhia kulipandisha hadhi Baraza la Manispaa Chake Chake ni  kurahisisha kasi ya upatikanaji wa maendeleo na ukuwaji wa uchumi ndani ya Mkoa huo.

Aidha amewataka watendaji wa Baraza la Manispaa Chake Chake kwa kushirikiana na wananchi  kuongeza kasi katika utendaji wao wa kazi, kuwa wabunifu wa miradi mbali mbali itakayowaongezea kipato  kitakachosaidia kukuza uchumi hasa katika Mkoa huo.                                           

Amesema mashirikiano ndio silaha katika kutimiza majukumu yetu ya kazi na kuwataka kuachana na kufanya kazi kwa utashi binafsi na kuelekeza nguvu zao katika kulitumikia Taifa.

Sambamba na hayo Mhe. Masoud amemuhakikisha makamu wa pili wa rais wa Zanzibar wizara itahakikisha inafata maelekezo na maagizo yote yanayotolewa na viongozi wakuu wa nchi katika kuwaleetea maendeleo wananchi wote  pamoja na kuifata  ilani ya chama cha mapinduzi ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba  Mhe. Mattar Zahor Massoud   amesema endapo viongozi watafanya kazi kwa pamoja hasa katika shuhuli za maendeleo na kuwataka kuachana na tabia ya kukwamisha na kuzorotesha Miradi mbali mbali ya maendeleo kwani kufanya hivyo ni kuikwamisha Serikali kwa ujumla.

Mhe. Mattar ameahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na viongozi na wananchi kwa  kufuata miongozo ya Nchi na kamwe hatokatishwa tamaa na wachache wasioitakia mema nchi yetu na amesema jitihada pekee ndio zitakazolipandisha zaidi Baraza hilo la Manispaa kuwa Jiji muda mfupi ujao.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa chake chake Ndugu Maulid Mwalim Ali  amesema kupandisha hadhi kwa baraza la manispaa la chake chake kutawajengea ari na morali wafanyakazi katika kufanya kazi kwa umakini na weledi wa hali ya juuu katika kufanikisha malengo ya serikali iliyojiwekea katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Amesema  Baraza la Manispaa Chake Chake litahakikisha linaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuimarisha usafi wa mazingira na kuendelea kutekeleza miradi mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na kuwapatia elimu zaidi  wafanyakazi ili kuleta ufanisi nzuri wa kazi.

Aidha amesema Baraza la Manispaa Chake chake  litafanyakazi kwa kasi na ufanisi zaidi ili kuhakikisha linapanda hadhi Zaidi kwa maslahi ya wanachi na Taifa kwa ujumla.

 

 Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.