Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende na kujadili fursa za uwekezaji na uwezeshaji wa miradi ya mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo
yaliyofanyika katika leo Jumanne (Oktoba 10, 2023), katika Ofisi ndogo za Ofisi
ya Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo aliipongeza juhudi za benki
hiyo katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi hapa nchini.
Dkt. Jafo amesema mapambano
ya uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi yanahitaji
juhudi za pamoja baina ya serikali na wadau na kutokana na umuhimu huo Serikali
imeendelea ushirikiano na wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi za kifedha ili kuibua fursa za uwezeshaji na uwekezaji wa miradi ya mazingira nchini.
Akitolea mfano Waziri Jafo amesema Serikali imeandaa
kanuni na mwongozo kuhusu biashara ya kaboni ikiwa ni mkakati wa kuboresha usimamizi mzuri
wa miradi ya biashara ya kaboni inayotekelezwa nchini, na kuzitaka taasisi za
kifedha kujitokeza katika kuziwezesha mitaji kwa kampuni mbalimbali ya
Watanzania.
“Utekelezaji
wa biashara ya kaboni utachangia kupunguza gesijoto na hatimaye kupunguza athari za
mabadiliko ya tabianchi na pia kuchangia katika utunzaji endelevu ya mazingira na kuleta
maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wetu..Jukumu hili linahitaji mshikamano
wa wadau wote” amesema Dkt. Jafo.
Aidha Dkt. Jafo ameiomba benki hiyo kuweka mpango na
mikakati Madhubuti ya uwekezaji katika nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa
mazingira kwani nishati isiyo
salama kwa matumizi ikiwemo kuni na mkaa imekuwa na
madhara kwa afya kwa watumiaaji na kuharibu mazingira.
“Serikali imendaa rasimu ya Dira ya Taifa ya Matumizi ya
Nishati Safi ya kupikia 2033…Tunaendelea kuwahimiza wadau ikiwemo taasisi za kifedha
kujitokeza na kuwekeza katika miradi ya uzalishaji wa bidhaa na nishati safi ya kupikia na
hivyo kurahisisha upatikanaji wake kwa Watanzania” amesema Dkt Jafo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji
Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Bw. Herman Kasekende amemhakikishia Waziri
Jafo kuwa Benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha
utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi.
Akitolea mfano Kasekende amesema Benki ya Standard
Chartered tayari imeandaa andiko la miradi ya uwekezaji wa mazingira na mabadiliko
ya nchi ikiwa ni hatua mahsusi ya kuunga mkono juhudi za serikali katika
kuwashirikisha wadau kuibua miradi uhifadhi wa mazingira na uhimilivu wa mabadiliko
ya tabianchi.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia
jamii ya Watanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia
uwekezaji wa miradi…Tutatoa mitaji kwa makampuni ya Watanzania yatakayoanzisha
miradi ya biashara ya kaboni” amesema Kasekende.
Aidha Kasekende amesema Benki hiyo pia imeanzisha kampeni maalum ya upandaji miti ambapo katika msimu wa mvua uliopita taasisi hiyo ilipanda miti imepanda miti 2000 na msimu ujao wa mvua imepanga kupanda miti 10,000 katika maeneo mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment