Habari za Punde

Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar yasaini hati ya mashirikiano na Wizara Maliasili na Utalii



Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar kupitia Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale imesaini hati ya Mashirikiano na Wizara Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Makumbusho ya Taifa Tanzania kwa lengo la kuzidi kuimarisha mashirkiano ambayo yatakua na muongozo maalum utakaowezesha kukuza Utalii na Mambo ya kale nchini.

Akizungumza mara baada ya Utiaji saini, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa Tanzania Dkt. Noel Lwoga ameeleza kuwa mkataba huu utahusiana zaidi katika eneo la Makumbusho na mambo ya kale hasa katika shughuli za Uhifadhi, Utoaji wa elimu juu ya mambo ya kale Uandaaji wa matamasha na tafiti mbali mbali ndani ya nchi yetu hasa katika mambo yanayoingiliana baina ya Zanzibar na Tanzania .
Dkt. Noel amefafanua kuwa kupitia mkataba huo wa mashirikiano taasisi zote zitaweka nguvu ya pamoja kwa kuandaa Sera na Kanuni,(taratibu) za kulinda na kuhifadhi Mambo ya kale ili Umiliki na Uhalali unaohusisha masuala ya urithi ubaki kua ni wa nchi ya Tanzania .
Nae Mkurugenzi wa Makumbusho na Mambo ya Kale Nd.Maryam Mansab amefafanua kuwa kupitia mashirikiano hayo yatapanua wigo kwa wataalamu wa pande zote mbili katika Mambo ya Kale ili kubadilishana uwezo na taaluma na hatiame kufikia lengo la namna gani Tanzania inaweza kuhifadhi na kutunza Urithi huu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Hati ya Mashirkiano imesainiwa leo tarehe 25/10/2023 na kushuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Dkt. Amina Ameir Issa katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.