Habari za Punde

Tigo Zantel Yazitundua Kituo cha Huduma kwa Wateja Amani Zanzibar

Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar Mhe. Mahmoud Mohammed Mussa akikata utepe kukizindua Kituo cha Huduma kwa WSateja cha Tigo Zantel Amani  Zanzibar Wilaya ya Mjini Unguja leo 24-1-2024 na (kushoto kwake) Mkurugenzi Huduma kwa Wateja Tigo Zantel Mwangazza Matotola , uzunduzi huo uliofanyika Amani Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar.

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mohammed Mussa, ameitaka kampuni ya Tigo Zantel kudhibiti matumizi mabaya ya mawasiliano kwa wateja wao ili waweze kusaidia maendeleo ya nchi yao.

Kauli hiyo aliitoa wakati akizindua kituo cha huduma kwa wateja Tigo Zantel Amani.

Alisema mawasiliano ni silaha kwani watumiaji wa mtandao huo wakiweza kutumia vibaya njia ya mawasiliano kwa kutoa taarifa za uongo basi yanawaweza kusababisha mitihani katika nchi ikiwemo machafuko.

Aidha lisema serikali inakuwa makini sana katika Mawasiliano kwani nchini Misri waliwahi kupata mitihani kwa sababu ya mawasiliano yaliyopelekea kupotea kwa kiongozi mkubwa katika nchi.

Meya Mahmoud alisema dhamana hiyo ya kuhimili na kudhibiti mambo kama hayo yapo kwao hivyo ni lazima kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kudhibiti jambo hilo.

"Kwenye wateja 1,500,000 ambao mnao muhakikishe mnakwenda nao vizuri hususan katika eneo la usalama wa Nchi na tukifanya hivyo tutasaidia sana maendeleo ya nchi yetu kukua zaidi," alisisitiza.

Hata hivyo, alibainisha kwamba katika mawasiliano pia biashara zinafanyika huko lakini malengo makuu ya serikali yoyote duniani ni kukusanya mapato lakini upo ujanja unaoendelea kutumika kupitia mitandao kwa watu kufanya biashara kupitia mitandao hiyo lakini serikali haipati faida na biashara hiyo inayofanyika.

Alisema wakati umefika sasa kwa kampuni hiyo kufanya kazi karibu na serikali ili kuona biashara popote itakapofanyika kupitia mtandao wa simu basi serikali inafaidika kwa kupata mapato.

Aidha alipongeza Tigo Zantel kwa kazi nzuri wanayoifanya na anaamini wataendelea kuongeza wateja kutokana na mipango na mikakati mizuri waliyojiwekea. 

Alisema makampuni ya simu mengi yaliyokuwepo katika jamii ya wananchi wa Tanzania milioni 60 Tigo Zantel ipo karibu ya kupata wateja milioni 20 sio kazi ndogo bali ni kazi kubwa.

Mbali na hayo, aliwasisitiza kufanya mambo yao kwa mujibu wa taratibu walizokubaliana na serikali ipo tayari wakati wote kuwasaidia kuhakikisha kampuni hiyo inakuwa zaidi kwani kampuni ya Zantel ndio ya kwanza kuanzishwa Zanzibar na inakuwa namba moja na kampuni nyengine zinafuatia nyuma.

Naye Mkurugenzi Huduma kwa wateja Tigo Zantel, Mwangaza Matotola, alisema kituo hicho kimeboreshwa kwa lengo la kutoa huduma ya daraja la dunia, kubadilika kulingana na mabadiliko ya kidijitali, na kuweka viwango vipya vya kuridhisha wateja wake zaidi ya milioni 1.5 wanaojumuisha Zanzibar na Pemba.

Alibainisha kuwa mafanikio hayo ni dhamira njema ya kampuni hiyo inayoendana na muungano wenye mafanikio na uwekezaji mkubwa walioweka ya kudumisha azma yake ya kuwapa wateja huduma nzuri.

Alisema kituo hicho kitafanya kazi muda wote masaa 24 kwa kuwahudumia wateja kuhakikisha wanatatuliwa changamoto zao kwa haraka.

Hata hivyo, alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa na teknolojia ya 5G yenye haraka zaidi (1Gbps) hapa Zanzibar, na kufanya marekebisho ya 4G kote Tanzania Bara na Zanzibar hivyo kituo hicho kitaongeza zaidi uzoefu, ushindani, na kuharakisha mabadiliko ya uchumi wa kidigitali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.