Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Ndg.Kinana Amkumbuka Lowassa kwa Uwajibikaji na Kuunganisha Watu

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndg. Abdulrahman Kinana, akisalimiana na Mjane wa Marehemu Mama Regina Lowassa Nyumbani kwake alipoungana na wanafamilia, viongozi wanachama, Serikali na wananchi katika ibada ya Shukrani ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa Waziri Mkuu Mstaafu iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Monduli Mjini Mkoani Arusha
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndg. Abdulrahman Kinana, ameungana na wanafamilia, viongozi wanachama, Serikali na wananchi katika ibada ya Shukrani ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa Waziri Mkuu Mstaafu iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Monduli Mjini Mkoani Arusha

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Ndg. Abdulrahman Kinana, Akizungumza na wanafamilia, viongozi wa Serikali na waumini wa KKKT katika ibada ya Shukrani ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa Waziri Mkuu Mstaafu iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Monduli Mjini Mkoani Arusha, Leo marchi 24, 2024.(Picha na Fahadi Siraji)

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahmani Kinana, amesema kuwa, Waziri Mkuu Mstaafu Edwar Lowassa ni kiongozi wa mfano hususan katika uwajibikaji na kuwaunganisha Watanzania bila ya kujali imani zao.

Kinana ameyasema hayo  katika ibada ya Shukrani ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa Waziri Mkuu Mstaafu iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Monduli Mjini Mkoani Arusha, Leo marchi 24, 2024.

“Ndugu Lowassa tutamkumbuka kama kiongozi mzalendo kwa taifa hili. Alikuwa mzalendo, alikuwa mchapakazi, alikuwa mtu aliyetufundisha uwajibikaji, mtu aliyefahamika akiamua jambo lake anatimiza.

“Kuna jambo leo hii linazungumzwa hapa nchini, jambo linaitwa uwajibikaji, kama kuna darasa la uwajibikaji basi darasa hilo litakuwa Edward Ngoyayi Lowassa,” amesema.

Mbali na hilo, kinana amesema kuwa hayati Lowassa atakumbukwa kwa namna alivyowaunganisha Watanzania bila ya kujali itikadi zao.

“Baba askofu umezungumza sana  juu ya umoja wa Watanzania na ukasisitiza kwamba tofauti zetu za kiimani tofauti zetu za kikabila, za kimaeneo ziwe ni tofauti zinazotuunganisha kutufanya tuwe kitu kimoja.

“Ukaongeza kusema kwamba siku hizi kuna utamaduni mzuri zaidi unaoimarisha umoja wetu, dini zote zinashirikiana, mimi ni shahidi, ndugu Lowassa amechangia misikiti mingi sana nchini, na ni muhimu kumuogopa Mungu, kumuabudu Mungu,” ameeleza.

Amesema kinachowaunganisha Watanzania ni kushikamana, kuwa wamoja, kuwa ndugu bila ya kujali dini, vyama, itikadi wala makabila.

“Ninawaomba Watanzania wote tuendelee kushirikiana, tuendelee kuimarisha umoja na amani, ya nchi yetu kwani bila ya amani, bila ya umoja, undugu na mshikamano mambo mengine hayawezekani, kila mmoja wetu kwa imani yake tuendedelee kumtanguliza Mungu na wote tukimtanguliza Mungu nchi yetu itakuwa nchi ya baraka” ameeleza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.