Habari za Punde

kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana ili kuwaepusha na mimba za umri mdogo

Na Maulid Yussuf. WMJJWW ZANZIBAR .

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana ili kuwaepusha na mimba za umri mdogo pamoja na maambukizi ya maradhi mbalimbali.

Akizungumza katika sherehe ya siku ya Hedhi Salama Duniani, iliyoadhimishwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya WAJAMAMA na Taasisi ya Maisha bora Foundation, huko Mbweni Unguja, amesema afya ya uzazi kwa wasichana ni muhimu kwani inawasaidia kujitambua na kuepukana na vishawishi.

Amesema siku ya Hedhi salama ni siku muhimu kwani inasaidia katika kupeana elimu juu ya  namna ya matumizi bora ya taulo za kike pamoja na namna ya  kujisafisha kwa wasichana na akina mama.

Aidha amewataka Wanafunzi walioshirik8 maadhimisho hayo na kupewa elimu kutambua kuwa suala la hedhi ni hali ya kawaida kwa mwanamke na ni suala la kimaumbile kwani hata katika dini limetajwa, hivyo amewataka kutokuwa na huzuni na kujiamini kwa kusoma kwa bidii ili watimize ndoto zao.

Pia amewataka kujitambua na kuridhika na hali walizokuwa nazo kwani kuna baadhibya wanaume wanaweza kuwarubuni kwa kuwapa pesa za kununulia taulo za kike ili waweze kuwadhalilisha hali ambayo itawasababishia kupoteza utu wao.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJAMAMA Ndugu Nafisa Jidawi Amewataka kutambua kuwa wanapopatwa na siku zao za hedhi hawatakiwi kupata maumivu hivyo  ikiwatokea hali hiyo wanatakiwa kuonana na wataalamu wa afya ili waweze kupatiwa matibabu ya haraka.

Kwa upande wake Ndugu Fatma Fungo Kutoka Taasisi ya Maisha Bora Foundation  amesema Takwimu zinaonesha kuwa siku 48 wasichana wengi wanakosa kuwepo skuli kutokana na kupata maumivu wakati wa  hedhi, ambapo  hali hiyo inapelekea kuwepo  utoro  Skuli, kudhoofika kwa afya na afya ya uzazi kuathirika, hivyo amesema kuna umuhimu wa kutafuta ufumbuzi  ili kuweza kupunguza changamoto hizo.

Akitoa elimu juu ya hedhi salama kwa Wanafunzi hao, Msaidizi Miradi Kutoka Jumuiya ya WAJAMAMA ndugu Yusra Ameir Haji amesema wanapokuwa na taula za kike salama wataweza kuwa na viongozi wazuri wa baadae kwa kuweza kujisomea vizuri na  kutumiza malengo yao.

Aidha ameomba kuangaliwa vyema suala la sera  ya kodi katika punguzwa ushuru au  kuondoshwa kabisa kwenye bidhaa za taula za kike kwani wasichana wengi wazazi wao wanashindwa kumudu kutokana na gharama na hivyo kukosa masomo yao kwa kubaki nyumbani.

Nao Wanafunzi na Walimu wa Skuli ya Sekondari Potoa  wa kidatu cha pili walioshiriki katika maadhimisho hayo wameelezea changamoto zao wakati wanapopata hedhi wakiwa Skuli wamesema wengi wao wanapata maumivu makali na hivyo kuwafanya kurudi nyumbani.

Hivyo wameoimba Serikali kuwapatia daktari maalumu ili kuwasaidia wanapopatwa na hedhi na maumivu makali ili kuwapunguzia kukosa masomo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.