Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali imetoa rai kwa mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu kuzingatia matumizi salama ya kemikali wakati wa kuhudumia vifaa hivyo ili kuepuka kusambaa angani kwa kemikali au gesi hizo na kusababisha uharibifu wa tabaka la ozoni au ongezeko la joto duniani.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira
Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Kamilembe Mutasa wakati
akifungua mafunzo kuhusu utekelezaji wa Itifaki ya Montreal
inayohusu Kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni leo
Mei 06, 2024 jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa
mafundi hao kuhusu matakwa ya itifaki hiyo ambapo
wanasayansi walivumbua kemikali hizo mwanzoni mwa miaka
ya 1970 ambazo hujipenyeza angani na kumong’onyoa tabaka
la hewa ya ozoni kwa kuruhusu mionzi au miale ya jua kufika
katika uso wa dunia na kusababisha madhara kwa afya ya
binadamu na
mazingira.
Bi. Kemilembe ametaja madhara hayo kuwa ni magonjwa ya
saratani ya ngozi, uharibifu wa macho unaosababisha upofu
na athari kwa ukuaji wa mimea na viumbe hai wengine.
Amesema kemikali zinazoharibu tabaka hilo zinatumika
katika majokofu na viyoyozi, vifaa vya kuzima moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku na kilimo cha maua na hifadhi ya nafaka katika maghala.
Kutokana na changamoto hiyo, Bi. Kemielembe amesema
juhudi zimeendelea kufanyika tangu mwaka 1985 baina ya
Serikali kitaifa na kimataifa kukubaliana kuanzisha Mkataba
wa Vienna na Hifadhi ya Tabaka la Ozoni na hatimaye Itifaki
ya Montreal kuhusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa
Tabaka la Ozoni ambapo shabaha yake kuu ni kusitisha
utengenezaji na utumiaji wa kemikali zinazomong’onyoa
Tabaka la Ozoni.
Ameongeza kuwa Itifaki ya Montreal imekuwa ikifanyiwa
marekebisho mbalimbali kutokana na tafiti zinazoainisha
kemikali mbalimbali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni au
kuwa na athari zingine za kimazingira kama kusababisha
ongezeko la joto duniani.
Hivyo, mafunzo hayo yanayohusu njia bora za kuhudumia
vifaa ikiwemo majokofu na viyoyozi pasipo kuathiri mazingira
yanatolewa na Mtaalamu wa Kimataifa wa viyoyozi na
majokofu kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa la Mazingira
(UNEP) Bw. Freeborn Taruvinga kwa kushirikiana na
wakufunzi kutoka Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi
(FETA), Bagamoyo Mhandisi Goodluck Rulagora pamoja na
Bw. Said Mziwanda koka kutoka Chuo cha Mafunzo ya Elimu
ya Ufundi Stadi (VETA) Chang’ombe, jijini Dar es Salaam
chini ya shughuli wezeshi ya kujenga uwezo wa kitaasisi katika kutekeleza Itifaki ya Montreal inayotekelezwa na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
No comments:
Post a Comment