Habari za Punde

Katibu Mkuu WHVUUM awapongeza Vijana waliotembeza Mwenge.

Na.Takdir Suweid

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi Fatma Hamad Rajab amewapongeza Vijana kwa kuonyesha Uzalendo wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa.

Ameyasema hayo wakati Vijana wa Zanzibar walioshiriki kukimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu,  walipofika Ofisini kwake Migombani kumtembelea.

Amesema Vijana hao wameiwakilisha vyema Zanzibar katika Tunu hiyo ya Taifa.

Aidha amewataka kuyafanyia kazi Mafunzo walioyapata katika Mwenge ikiwemo kutunza siri ili kuendelea kuwa Vijana bora na Wazalendo wa Nchi yao.

Hata hivyo amewataka kufanya kazi kwa bidii, kushikamana na kuwa na Maadili mema katika utendaji wa kazi zao na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana Bw. Shaibu Muhammed Ibrahim na Afisa Mdhamini Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo  Bw. Mfamau Lila Mfamau wamesema Vijana hao wamefanya kazi ngumu na Uzalendo wa hali ya juu.

Hata hivyo wamesema mafanikio hayo yaliopatikana yanatokana na Umahiri, Ujasiri na Umakini wa Mkufunzi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa kutoka Zanzibar Bw. Mussa Muhammed Ngomambo.

Nao Vijana walioshiriki kukimbiza Mwenge huo, kutoka Zanzibar Bw. Ramadhan Makame Khamis kutoka Mkoa wa Kusini Pemba na Nusaibat Hafidh Ahmed kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi wameipongeza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kuwaamini na kuwapatia fursa hiyo muhimu kwa Faida yao na Taifa kwa Ujumla.

Aidha wamesema kazi hiyo ilikuwa ngumu lakini wameweza kuifanya kwa urahisi kutokana na mashirikiano walioyapata kutoka kwa Viongozi wa Wizara zote mbili za Tanzania zinazohusiana na Vijana.

Mwenge wa Uhuru mwaka 2024, umezinduliwa tarehe 2/4/2024 Mkoani Kilimanjaro na kufikia kilele chake tarehe 14/10/2024 Mkoani Mwanza ambapo Kauli mbiyu ilikuwa Tunza Mazingira, Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa endelevu.

Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano,

WHVUUM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.