Habari za Punde

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu CCM Taifa Mlezi wa Mkjoa wa Tanga Mhe. Hemed Suleiman Afungua Kampeni za CCM Mkoa wa Tanga

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Mlezi wa Mkoa wa Tanga Ndugu. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wana CCM na wananchi wa Mkoa wa Tanga kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili CCM iweze kushinda kwa kushindo katika uchaguzi huo.

Ameyasema hayo katika Mkutano wa Hadhara wa uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi Mkoani Tanga kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika katika Uwanja wa Ramole Wilaya ya Tanga, Mkoa wa Tanga.

Mhe. Hemed amesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu sana katika kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 hivyo amewaagiza viongozi wa chama ngazi mbali mbali kuelekeza nguvu zao katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuhakikisha wagombea wote wa CCM wanashinda kwa kishindo.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amesema ili Chama cha Mapinduzi kiendelee kushinda na kushikilia Dola ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake ndani ya chama kupambana ili kuwaonesha wapinzani ukubwa na uimara wa CCM hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema akiwa Mlezi wa Mkoa wa Tanga Kichama hayuko tayari kuona Mkoa wake ukifanya vibaya katika uchaguzi huo hivyo ni jukumu la wanachama kujitokeza kwa wingi katika kuipigia kura CCM na kuweza kushikilia nafasi ya Kwanza kwa wingi wa Kura.

Nae Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ndugu Rajab Abraham Abdalla amesema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa CCM itashinda kwa kishindo na kuendelea  kushikilia hatamu Mkoa wa Tanga kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa.

Ndugu Rajab amesema CCM imefanya mambo makubwa ya kimaendeleo ndani ya Mkoa wa Tanga ikiwemo kuendelea kusimamia suala zima la Amani na Utulivu ambayo ndio chachu ya Maendeleo yanayoletwa na CCM chini ya Raisi Dkt Samia Suluhu Hassan.

Amefahamisha kuwa Mkoa wa Tanga utaendelea kuwa ngome Imara na madhubuti ya chama Tawala na hatotokea kiongozi yoyote kutoka vyama vya upinzani kuongoza katika Mkoa wa Tanga .

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo laTanga Mjini Mhe. Ummy Ali Mwalim amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa zaidi ya Asilimia mia hivyo wanaCCM na wananchi waTanga wana kila sababu ya kuwapigia kura wagombea wote walioteuliwa na Chama cha Mapinduzi kugombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuendelea kukiweka chama hicho madarakani.

Mhe.  Ummy amesema hakuna Sekta ambayo haijapitiwa na miradi ya maendeleo chini ya Jemedari Rais Dkt. SAMIA na kutolea mfano ujenzi wa Bandari ya Tanga  ambapo meli kubwa kutoka nchi mbali mbali zinatia nanga Mkoani hapo na harakati za kiuchumi mkoani humo zinaongezeka siku hadi siku.

Akizungumza kwa niaba ya wagombea wenzake Mgombea kwa nafasi wa Mwenyekiti wa Masiwani kata ya Majengo Ndugu PAUL MAZEE MWAKA amemuhakikishia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM na Mlezi wa Mkoa wa Tanga kuwa yeye na Wagombea wenzake wamejipanga vya kutosha na kuhakikisha kuwa watashinda kwa kishindo nafasi zote zinazogombaniwa kwenye Mkoa wa Tanga.

Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR)

Leo tarehe… 20 / 11 / 2024

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.