Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Majaliwa Amekutana na Ujumbe wa Wafanyabiashara Kutoka Falme ya SaudiArabia * Awaeleza mikakati ya Tanzania katika kuvutia wawekezaji. * Awakaribisha kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati

 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini ili kuendelea kuwavutia wawekezaji.

Ameyasema hayo leo,  (Jumatano 12 Februari 2025) alipokutana na Ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka Falme ya Saidi Arabia, Katika Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu magogoni jijini Dar es Salaam.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema uhusiano baina ya Tanzania na Saudi Arabia umeendelea kuimarika na kufungua fursa kwa wawekezaji kutoka Saudi Arabia kuwa na wigo wa kuwekeza nchini Tanzania hususan katika sekta za nishati, Kilimo, Viwanda, Mifugo Utalii na biashara.

 

Aidha, amesema Tanzania imeendelea kunufaika na fursa ya kusafirisha bidhaa za mazao na mifugo kwenda nchini Saudi Arabia jambo ambalo limeendelea kukuza uchumi wa nchi.

 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji hao kuwekeza katika sekta ya nishati ili kuongeza nguvu katika kampeni ya nishati safi ya kupikia iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

"Serikali yetu imeweka mkazo katika kufikia malengo ya kuwawezesha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na kuepukana na matumizi ya nishati zisozo rafiki kwa mazingira, Nchi yetu bado ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya nishati. Ninawakaribisha sana." 

 

Kwa Upande Wake, Rais wa Chemba ya  Biashara wa Falme  ya Saudi Arabia, Mheshimiwa  Hassan Bin Moejeb Al Huwaizi, amesema yeye pamoja na Ujumbe wake wanaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwavutia wawekezaji hususan kutoka Nchini Saudi Arabia.

 

Mkutano huo pia uliudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Naibu Waziri Uchukuzi, David Kihenzile, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida pamoja na Maofisa mbalimbali wa Wizara ya Mambo ya Nje.

 

Ujumbe huo wa Wafanyabiashara ulioongozwa na Rais wa Chemba ya Bishara ya Falme  ya Saudi Arabia, Mheshimiwa  Hassan Bin Moejeb Al Huwaizi uko katika ziara ya siku mbili Nchini Tanzania ambapo pamoja na mambo Mengine pia wamekutana na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania na kujadili mashirikiano ya kibiashara baina wafanyabiashara wa Nchi hizo.

 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATANO, FEBRUARI 12, 2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.