Habari za Punde

ZIPA Yasaini Mkataba wa Makubaliano na Benki ya Uwekezaji ya Ufaransa (BPI)

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano kati ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Benki ya Uwekezaji ya Ufaransa (BPI)  kunadhihirisha utayari wa kushirikiana katika kukuza na kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo nchini.

Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya kutiliana saini mkataba wa ushirikiano kati ya  Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Benki ya Uwekezaji ya Ufaransa (BPI) France iliyofanyika katika Ukumbui wa Hoteli ya  New Amani Hoteli Zanzibar.

Amesema makubaliano hayo ya kimkakati yatapelekea kukuza ushirikiano wa kiuchumi, kubadilishana mifumo ya uchumi na biashara sambamba na  kupeana fursa za uwekezaji kati ya Zanzibar na Ufaransa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ushirikiano huo unalenga zaidi katika uwekezaji wa kifedha na kufungua milango katika kupeana taaluma, kubadilishana uzoefu wa kufanya kazi ambao utawaogezea uwezo wataalamu wa ndani.

Aidha, Mhe.Hemed amesema ushirikiano kati ya ZIPA na BPI FRANCE hautawanufaisha wawekezaji wa Kimataifa Pekee bali utawawezesha wafanyabiashara wa ndani kupata vifaa muhimu vya uzalishaji ambavyo vitasaidia biashara zao kukuwa na kujipanga katika soko la Kimataifa. 

Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali imekuwa ikiweka mazingira rafiki ya biashara ikiamini kuwa uchumi unakuwa na kufanikiwa kwa kushirikiana na kufanya Uvumbuzi wa kitaaluma ambapo kupitia makubalino hayo  yanadhihirisha utayari wa kufanya kazi kwa pamoja yatakayoleta matokeo chanya katika suala zima la uwekezaji na ukuwaji wa uchumi nchini.

Akizungumza kwa niaba ya ya Waziri wa Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Mhe. Ali Suleiman Ameir amesema kupitia utiaji wa saini kwa mkataba huo wa kufanya kazi kwa mashirikiano kati ya ZIPA na BPI France kutajenga nguzo Imara kwa kuweka mikakati madhubuti ya  ukuwaji wa uchumi wa Zanzibar. 

Amesema BPI imejipanga kuisaidia Zanzibar kukuza uchumi wake kupitia sekta mbali mbali ili kuweza kufikia malengo yake ya kuwa na maendeleo endelevu katika Sekta ya Uchumi na Biashara. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar ndugu. Saleh Saad Mohamed amesema uwekwaji wa saini wa mkataba huo wa mashirikiano kati ya BPI France na ZIPA yatasaidia kukuwa kwa maendeleo ya uchumi Zanzibar na sambamba na kukuwa kwa kipato cha mtu mmoja mmoja. 

Saleh amesema kuwepo kwa makubaliano hayo yataleta mabadiliko chanya katika biashara na uchumi ambapo Taasisi binafsi zitaweza kukuza uchumi wao pamoja na kuongezeka kwa ajira zitakazosaidia kukuwa kwa  uchumi wa Zanzibar. 

Nae Balozi mkaazi wa Ufaransa nchini Tanzania bibi Anne-Sophie Ave amesema makubaliano yao kati ya BPI France na ZIPA yamelenga kushirikiana katika Ukuwaji kwa uchumi wa Zanzibar ambapo BPI imejipanga katika sekta ya Mafuta na Gesi, Viwanda, Miundombinu, Utalii na Sekta nyenginezo.


Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Tarehe 10.04.2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.