Mgombea wa Uwakilishi Jimbo la Kiwani ndugu Hemed Suleiman Abdulla amesema endapo atapewa ridhaa ya kuwa kiongozi ndani ya jimbo hilo atahakikisha huduma zote muhimu za kijamii zinapatikana kwa wakati.
Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokutana na wajasiriamali na wenye vikundi vya ushirika katika vijiji vya Mtangani, Mihogoni na Kiwani Sokoni kwa lengo la kusikiliza changamoto zao pamoja na kujiombea kura yeye na wagombea wa Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa zanzibar, Mbunge na madiwani wa wadi ya Kendwa na Mwambe.
Amesema anatambua kuwa kuna baadhi ya vijiji jimboni humo havijafikiwa na huduma ya majisafi na salama pamoja na nishati ya umeme hivyo atakapokuwa mwakilishi wa Jimbo hilo atahakikisha kila kijiji kinafikiwa na huduma hizo.
Akizungumzia suala la ulipwaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa miundombinu ya barabara nakuathirika kwa majumba na vipando vyao amesema suala hilo analifuatilia na kuwaahidi kuwa kila anaestahiki kulipwa fidia atalipwa kulingana na utaratibu uliopangwa.
Ndugu Hemed amewaahidi wanachama wa CCM na wananchi wa Jimbo la Kiwani kuwa wavuvi na wakulima wa mwani watapewa kipaombele kwa kupatiwa vifaa vya kisasa vya kufanyiwa kazi pamoja na kutafutiwa masoko ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuuziaa bidhaa zao ili waweze kujikwamua kimaisha.
Amewaahidi wajasiriamali na wenye vikundi vya ushirika kukinyamazisha kilio chao cha muda mrefu kwa kuwapatia elimu na taaluma juu ya ujasiriamali pamoja na kuwapatia mitaji kwa ajili ya kuendeleza na kukuza mitaji na biashara zao.
Mgombea huyo wa uwakilishi wa jimbo la kiwani amesema malalamiko yaliyowasilishwa na wazee juu ya kukatwa kwa pencheni zao ameyachukua na anaahidi kuyafuatilia na kupatiwa ufumbuzi kama ilivyo adhma ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Mwinyi ya kupunguza changamoto mbali mbali za wazee.
Akizungumzia sekta ya michezo ndugu Hemed amesema kwa kushirikiana na viongozi wenzake wataliangalia kwa upeo mkubwa suala la michezo jimboni humo kwa kujengwa viwanja viwanja vya michezo vya kisasa ambavyo vitatoa fursa kwa wanamichezo na vijana wa jimbo la kiwani kupata sehemu salama za kufanyia mazoezi na mashindani mbali mbali.
Amewahakikishi wananchi wa Mtangani na Kiwani kwa ujumla kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na usalama jambo la msingi ni kuhakikisha wanafuata sheria, taratibu na miongozo yote iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ili kuweza kuidumisha amani iliyopo nchini katika kipindi chote cha uchaguzi na hata baada ya ichaguzi.
Kwa upande wake Mgombea wa Ubunge Jimbo la Kiwani ndugu Hija Hassan Hija amesema endapo watachaguliwa kuwa viongozi jimboni humo watahakikisha ujenzi wa ukuta pembezoni mwa bahari kijijini hapo ili kuwakinga wananchi na madhara yanayoweza kusababishwa na kujaa kwa maji ya bahari.
Ndugu hija amesema kupatikana kwa maendeleo kunachangiwa na uwepo wa amani na utulivu nchini hivyo amewaasa wananchi wa Mtangani kutokubali kutumika kuwa chanzo cha uchafuzi wa amani kwa maslahi ya watu wachache.
Nae mgombea wa udiwani wadi ya Kendwa ndugu Ali Bakari Ali amewataka wananchi wa Jimbo la Kiwani kushirikiana pamoja katika kuijenga kiwani yenye maendeleo.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 23 / 09 / 2025
No comments:
Post a Comment