6/recent/ticker-posts

DK KARUME KUFUNGUA MAPINDUZI CUP LEO

Azam kuivaa KISC jioni, Yanga, Mafunzo kumenyana usiku

Na Salum Vuai, Maelezo

RAIS mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, leo anatarajiwa kufungua pazia la mashindano ya kuwania Kombe la Mapinduzi katika uwanja wa Amaan.

Ingawa michuano hiyo itaanza kwa mechi mbili za kundi B, lakini ile ya usiku itakayowakutanisha mabingwa wa Tanzania Bara na Afrika Mashariki na Kati, Yanga na machampioni wa Zanzibar Mafunzo, ndiyo iliyopangwa kuwa ya uzinduzi rasmi.


Kabla ya mtanange huo unaotazamiwa kuwa wa kukata na shoka, uwanja wa Amaan utakuwa katika kibarua kigumu kuhimili maadaluga ya matajiri wa 'ice cream' Azam FC na wakongwe wa soka Zanzibar waliorudi ligi kuu msimu huu baada ya kupotea kwa miaka mingi, Kikwajuni, ambao watatoana jasho wakati wa saa 10:00 jioni.

Kwa mujibu wa Kamati ya mashindano hayo, kabla mechi ya uzinduzi, kutakuwa na burudani kadhaa zitakazopamba uwanja ikiwa ni pamoja na michezo ya sarakasi, na beni.

Kamati hiyo imewaomba mashabiki wa soka visiwani humu kujitokeza kwa wingi ili kupata burudani hiyo pamoja na kuzipa hadhi sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho kwa mechi za kundi A, ambapo mnamo saa 10:00 jioni, Miembeni United itatiana mbavuni na mabaharia wa KMKM, huku wekundu wa Msimbazi, Simba, wakipimana ubavu na Jamhuri wakati wa usiku.

Ubingwa wa ngarambe hizo unashikiliwa na Simba ya Dar es Salaam, ambayo iliutwaa kwa kuwafunga watani wao wa jadi Yanga mabao 2-0 katika mchezo wa fainali katika michuano iliyopita mwaka jana.

Tayari mashabiki wa soka katika mitaa mbalimbali ya Zanzibar wameanza kuizungumzia michuano hiyo, ambapo kila mmoja amekuwa akitabiri kwa uoni wake juu ya timu inayoweza kulibeba kombe hilo jipya.

Post a Comment

0 Comments