Na A K Simai
Hivi karibuni Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein alizungumza
na Waandishi wa habari, Wahariri pamoja na wananchi katika utaratibu wake
aliojiwekea wa kila miezi mitatu.
Katika hotuba yake aligusia
mambo mengi sana yanayohusu taifa pamoja na machafuko ya karibuni yaliyoleta
uharibifu wa mali na kuvunjika kwa amani.
Kilichonisukuma kuandika
makala hii ni Suala muhimu aliloulizwa na mwandishi wa siku nyingi wa ITV, Farouk
Karim, kuhusu mikataba ya ujenzi wa jengo la uwanja mpya wa ndege kwamba sivyo
ilivyokusudiwa je ni kweli?
Dk Shein alikiri kwamba
ujenzi umesimama ila ni Serikali iliyoingilia kati na kuusimamisha kutokana na
kujitokeza kwa mambo mengi ya kimsingi kama kutojulikana kwa michoro serikalini
pamoja na mapungufu mengine kwa kutokuwepo kwa taa, eneo la kusafiria na
kuondekea abiria, eneo la VIP kuwepo ndani na pia kutokuwepo na eneo la
kuongeza jengo ikihitajika hivyo kwa siku zijazo. Na la msingi ni Air Bridges
zilizowekwa zilikuwa na uwezo wa kupokea Ndege ndogo za aina Boeing 737 wakati
tayari Airport inapokea ndege kubwa za Boeing 767, 777 na 747 pia Airbus 320 na
380. Hivyo zingelishindwa kuegesha katika Air bridges hizi na isingekuwa
muwafaka kwa siku zijazo.
Dk Shein alisisitiza kwamba
ujenzi utaendelea karibuni baada ya kuwekana sawa katika mapungufu
yaliyojitokeza.
Ikumbukwe kwamba hii ni mara
ya pili kwa jengo hili kusitishwa na kwa sababu kama alizozielezea Dk Shein
mpaka wakandarasi wakataka kufanya marekebisho ya mkataba na malipo ili kuweza
kukabiliana na gharama mpya
zilizojitokeza baada ya marekebisho ya ujenzi huo. Tayari Ujumbe wa Serikali ya
Zanzibar umeshakwenda China mara mbili kuzungumza na Serikali ya China
kuhusiana na Variations au mabadiliko yanayohitajika.
Ujenzi umesimama kwa
zaidi ya miezi miwili sasa.
Ujenzi wa jengo jipya la abiria katika
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar
wa Abeid Amani Karume ambao unafanywa na kampuni kutoka China ya Beijing
Engineering Construction kwa mkopo wa US$ 70.4 milioni kutoka Exim Bank ya
China. Tayari tunaambiwa gharama hizi zimeshaongezeka na mwenye dhamana ya
kulipa mkopo huu wa riba ni mimi na wewe kama walipa kodi kupitia Serikali.
Dk Shein alifanya ziara kutembelea
ujenzi wa jengo hili tarehe 08 Desemba 2011 kujionea maendeleo ya ujenzi.
Suala wakati Mheshimiwa Rais
alipotembelea jengo hili alishauriwa vyema au mapungufu haya yalikuwa bado
kujulikana?
Maneno kama haya
yalikaririwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alipozungumza na
wanahabari tarehe 28/02/2012 ambayo yalikuwa yakifafanuwa maendeleo ya ujenzi.
Pia hapa hatukutanabahishwa kwamba tayari kumeshaonekana matatizo katika ramani
ya jengo lile ambazo zinahitaji kurekebishwa (Variations).
Mmoja katika wachangiaji wa
mada hii katika moja ya mitandao jamii (Mzalendo.net) aliwahi kusema Mradi wa
ujenzi hupimwa kwa kutumia vigezo vitatu vikubwa:
Ujenzi
kumaliza kwa wakati.
Kwa jinsi
ya matatizo ambayo tayari yameshajitokeza kusimamishwa ujenzi huu mara mbili
tuna uhakika hautomalizika kwa wakati Desemba 2013.
Quality ya ujenzi kufikia ile iliyotarajiwa
Hili nalo
pia ni tatizo hasa kwa wanaoshuhudia ujenzi huu wameonesha mashaka na kampuni
iliyopewa dhamana ya kujenga kama ina uwezo na Project kubwa za aina hii. Sijui
kama utafiti ulifanyika kabla kuona kazi za kampuni hii ilizozifanya sehemu
nyengine duniani kujiridhisha au yalikuwa ni makubaliano ya kimkataba kwa kuwa
waliotoa Mkopo ni Benki ya Kichina.
Mradi
kumaliza kwa kutumia gharama zilizopangwa awali (within budget)
Tayari
gharama zimeshaongezeka na kama marekebisho mengine yatapitishwa gharama hii
zitapanda tena na bado hatujui kwamba tunaweza kuona mapungfu mengine siku za
mbele yatakayohitajia marekebisho.
Kwa hatuwa iliyofikia jengo jipya la uwanja wa ndege wa Zanzibar, hakuna
anaeweza kusema kigezo chochote kati ya hivyo nilivyovitaja kimefikiwa,
kitafikiwa, au hakitofikiwa.
Kimsingi mazingira ya utiaji
mkataba Jengo hili na mfumo wa utendaji wake umeniwacha na maswali mengi kuliko
majibu.
1
Ni timu gani iliyokuwemo katika kuandaa plan
ya jengo hili ni watu waliokuwa na uzoefu kwenye aviation au ni watu wa
kuokoteza tu?
2
Hakukuwa na consultancy wakati wa kuandaa
plan yenyewe na hakukuwa na kureview kuangalia kama kila kinachohitajika katika
Airport ya kile kimewekwa?
3
Tulikurupuka katika kuingia mkataba huu ambao
kwa sasa utaweza kutuingiza kwenye janga zito la deni lenye kuongezeka kwa riba
pamoja na kuongezeka kwa gharama?
4
Kutakuwa na hatua zozote za kinidhamu au
kuwajibika kwa waliotuingiza katika balaa hili au kulikuwa na mazingira ya ten
percent?
Jengine ambalo bado
linaniwacha na maswali kadhaa na mtaniwia radhi kwa kujiuliza mwenyewe ni
kwamba jengo hili lilitarajiwa kumalizika Desemba 2013 na kuanza kazi mapema
2014.
Mpaka hivi sasa hakuna
mpangilio wa kuwafundisha na kuwapa mafunzo (training na inductions) wafanyakazi
watakaofanya kazi katika jengo hili ambalo ninaamini litakuwa na vifaa vya
kisasa wakati tuna mwaka mmoja tu na nusu kabla ya kufunguliwa kwake (kama
litamalizika katika muda uliopangwa). Wanatarajiwa wafanyakazi waliopo katika
jengo la zamani ( Terminal 1) kuhamishiwa huko wakati Jengo hili pia litatumika
kwa domestic flights.
Nimesema hivyo kwa sababu
katika bajeti ya mwaka huu ya Mamlaka, hakukuwekwa fungu litakaloombwa katika
bajeti ili litumike katika mafunzo ya kuwapika vijana wetu ambao tunawatarajia
kuwatwisha majukumu ya kuisimamia Airport yetu iweze kufanya kazi kwa ufanisi
na kitaalamu. Na pia hakuna fungu la kuajiri wafanyakazi wengine ambao
watahitajika kwa kuongezeka majukumu.
Wakati
akizindua Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege, Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Hamad Masoud Hamad alisisitiza bila ya
kuwepo kwa wafanyakazi wenye taaluma katika mamlaka hiyo haitoweza kuwa na sifa
za kimataifa za kuwahudumia wageni wanaoingia na kutoka katika Viwanja vya
ndege vya Zanzibar.
Aidha
waziri huyo aliwaasa wafanyakazi hao kujenga uaminifu katika utendaji wa kazi
zao kwani vitendo vya udokozi vinaweza kupoteza haiba ya uwanja huo.
Aliongeza kuwa kumfanyia kitendo kibaya mgeni mmoja
kunaweza kupoteza wageni wengi jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma malengo
yaliyokusudiwa.
Sijui nasaha hizi za Waziri zimechukuliwa vipi na
Bodi kwani uwepo wa ushindani katika usafiri wa Anga kwa nchi za Afrika
Mashariki ni mkubwa mno. Hivyo kila nchi hutakiwa kujipanga vyema kabla ya
kuingia katika ushindani huu ambao kwa nchi nyengine tayari wana uzoefu wa
kutosha.
Airport ni sehemu ambayo
kila kitu kinatakiwa kiende kwa wakati uliopangwa tokea kutua na kuondoka kwa
ndege, huduma pamoja na vitendea kazi. Kukitokea kuharibika chochote basi
kitaathiri safari nzima za ndege na kuchelewa na hivyo kuleta usumbufu kwa
wasafiri, kuhatarisha usalama wa abiria pamoja na ndege na Mamlaka kuweza
kutozwa faini na mashirika ya Ndege na hatimaye kuacha kuutumia Uwanja kwa
kukosa ufanisi.
Tunatahadharisha haya si kwa
kumchongea mtu bali kwa yaliyotokea huko nyuma wakati wa kununulia kwa Jenereta
la kutumika Uwanja wa ndege ambalo hadi sasa halijaanza kutumika wala
kujaribiwa hadi muda wake wa dhamana (warrant umemalizika) na pesa nyingi za
walipa kodi kutumika mpaka kamati teule ya Baraza la Wawakilishi kutaka hatua
za kinidhamu zichukuliwe kwa baadhi ya watendaji.
Pia tunauliza Serikali Je
ina mpango wowote wa kuwawajibisha wale wote tuliowapa dhamana ya kusimamia
mradi huu kwa kutuingiza katika mazonge na magharibi ya roho kwani kama
utaalamu wao na uzoefu wao ungelitumika vyema tusingejikuta katika hali ya
kupapurana na wakandarasi wakati wachawi ni sisi wenyewe.
Tusingejikuta katika hali
mpaka Rais wa Nchi yetu anaingilia kati suala hili na katika dhana ya kujenga
utawala bora ni sera ya uwajibikaji kutekelezwa kikamilifu kwa kila aliyekwenda
kinyume na malengo au maafikiano na dhamana alizokabidhiwa basi ima wahusika
wawajibike au wawajibishwe na Serikali na hii ni moja ya changamoto ambayo Bodi
ya Mamlaka ya viwanja vya Ndege itapaswa kukabiliana nayo bila ya kuoneana
muhali au kutazamana kwa jicho la huruma.
Tarehe 12/04/2012 wakatii
ikizinduliwa Bodi ya Mamlaka ya Uwanja wa Ndege, Mwenyekiti wa Bodi, Abdulghani
Msoma aliahidi kuwa watafanya kazi kwa uzalendo kwa
ajili ya maendeleo ya mamlaka hiyo.
“Hakuna maendeleo bila ya changamoto na nipo tayari kukabiliana na changamoto
hizo kwa hali na mali bila ya kujali maslahi yoyote” alisema Msoma.
Hii ni changamoto Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi, tunakusikiliza.
4 Comments
Ahsante sana ndugu yangu AK Simai kwa makala yako ya kizalendo, inayolenga kujenga Z'bar bora; yenye uwajibikaji na maendeleo.
ReplyDeleteUkweli ni kwamba hapa, tuna matatizo mengi ya namna hii, eneo uliloligusia ni moja tu kati ya maeneo mengi yenye matatizo hayo.
Nadhani Z'bar imebaki sehemu pekee hapa Afr. Mashariki na kati ambapo viongozi wanaoshindwa kuwajibika hawajiuzulu wala kuchukuliwa hatua za kinidhamu au kisheria.
Baya zaidi ni kwamba wakati haya yanatokea, hakuna hata mwandishi mmoja mzalendo anaeweza kuwaeleza wananchi wakayaelewa.
Inasikitisha kuona hadi hii leo kuna wazenji wengi ukiwaambia kwamba inayotumika ni kodi yangu na yako hata hawakuelewi.
Hata wale wanaodai wamesoma, mada kama hizi za kuwazindua watu hawachangii, badala yake wanachangia mambo ya ushabik na kutwambia kua matatizo yetu yote yanatokana na MUUNGANO.
Ndugu yangu usichoke kutuelimisha, endelea kuwa 'objective' naamini mwisho watu watakuelewa na kukufuatilia kwa karibu na hatimae kuwa miongoni mwa 'heroes' wa mabadiliko Z'bar!
ASANTE NDUGU SIMAI KWA KUTUELEWESHA WAPI TUMEFIKA WENGI TULIKUWA HATUJUWI KINAENDELEA NINI NA WAPI TUMEFIKA?NATUMAI WAHUSIKA WATAIPATA MADA YAKO ILI TUWEZE KUSONGA MBELE TUACHANE NA UZEMBE,PIA HAWA WAFANYAKAZI WA KIWANJA HICHO CHA KISAUNI WANAITIA HASARA SANA ZANZIBAR TENA KWA MAKUSUDI KAMA UNAVYOJUWA TUPO WAZANZIBAR WENGI NJE YA NCHI NA KILA MWAKA JUNE,JULY ASILIMIA 80 HUWA TUNAKUJA NYUMBANI CHA KUSHANGAZA TUKISHUKA DAR-ES-SALAAM HATUPATI USUMBUFU WOWOTE TUNASHUKA TUNACHUKUA VISA BILA TAABU UNATOKA BILA MASHWALI WALA KERO LAKINI UKISHUKA KISAUNI UTAJUTA WANAKUFANYA KAMA MHALIFU KWA MASWALI MENGI UNAZULIWA KUTOKA WANAZUIYA PASSPORT MPAKA UPATE MWENYEJI AKUTOE KWA HALI HIYO SOTE TUMEAAMUA KUSHUKIA DAR KUKIMBIA USUMBUFU SASA KIASI GANI SERIKALI YA ZNZ INAKOSA?HILI NDIO SWALI LA KUJIULIZA MAANA KWA MFANO FAMILY MOJA TU YENYE BABA MAMA NA WATOTO 5 TUNALIPA $300 ZA KIMAREKANI SASA UKIPATA WAZANZIBAR WOTE WAKISHUKA HAPO KISAUNI SERIKALI YA ZNZ ITAINGIZA KIASI GANI KWA AJILI YA VISA?MAANA ASILIMIA 90 TUNAOISHI NJE TUNA PASSPORT ZA KIGENI KWA HIYO TUNALAZIMIKA KULIPA VISA $50 ZA KIMAREKANI KILA MTU HATA MTOTO MCHANGA WENGELITIZAMA HILI ILI HIZI PESA TUJE KULIPA KISAUNI KUENDELEZA MAENDELEO YA ZNZ HAITOWEZEKANA KAMA UKISHUKA UMECHOKA NA SAFARI HALAFU MTU ANULETEA USUMBUFU NA MASWALI YASIYO NA MSINGI WOWOTE.
ReplyDeleteUnaona kazi...hiyoo?
ReplyDeleteKumbe uchumi tunao tunaukalia!
Na mimi naamini, kuna wazenji wengi zaidi wenye paspoti za kigeni kuliko hata ndugu zetu wa Bara kutokana na maafa ya 1995-2000.
Nyinyi akina CALYPSO tupeni data hizo, tuwabane wawakilishi wajue maswali ya kuuliza Barazani badala ya kulala na kugonga meza!
Mimi nataka ifikie pahala mtu akitaka kugombea ubunge au uwakilishi afikirie kwanza ugumu wa kazi kuliko hata malipo yake!
Nataka mara hii tuone bajeti ya wizara ya mawasiliano ikizuiwa mpaka pale wahusika wa kashfa hii watakapochukuliwa hatua!
"TUJIANGALIE WENYEWE KWANZA KABLA YA KULAUMU WENGINE"
Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki Tanzania!
Ndugu yangu nakuomba utufanyie pia ihsan ya kutuletea makala zinazohusiana na uchumi hata kama wewe sio 'economist' kwa uwezo unaouonesha, naamini unaweza hata kuwaomba wachumi kama vile Dr. Moh'd Hafidh wakakupa data ili uweze kutufunua macho.
ReplyDeleteJamani Z'bar tupo gizani! utadhani watu hawakusoma, tunaambiwa tu tunategemea utalii na kilimo lkn. hatuambiwi ni kilimo cha nini au kinatoa asilimia ngapi?
Wengine akina Ustadh Farid(mwamsho) wanatwambia zanzibar ni tajiri na hakuna kisiwa maskini lkn hawasemi ni kwa vipi.
Najua takwimu zipo, lkn sisi wengine tunahitaji tufafanuliwe kwa karibu, najua tunakukwaza lkn. jitahidi 'you are the only hope'