
Zanzibar imelazimisha sare ya kutokufungana na Mabingwa watetezi Uganda na hivyo kuingia katika Robo fainali baada ya kupata pointi nne katika mechi zake tatu ilizocheza.
Katika mechi ya kwanza ilifanikiwa kuilaza Burundi goli 4-0 kisha kufungwa kwa taabu na Kili boys 1-0 na hatimaye kuwabana vilivyo mabingwa watetezi na kutoka sare 0-0.
Uganda iliwapumzisha wachezaji wake muhimu kama Goli kipa Hamza Muonge na wachezaji Stephen Bengo , Dan Wangaluka, Simon Serunkuma , Geoffry Massa na Bonny Wayenje.
Zanzibar itabidi wajilaumu wenyewe kwa kuweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini wakashindwa kuweka mpira kimiani mwa Uganda Cranes. Nafasi za wazi zilipotezwa na Abdul Halim Humoud, Abdullah Seif na Othman Omar.
Golikipa wa akiba Mohamed Abdalla nae alikuwa na kazi pevu kupangua hatari za washambuliaji kama kina Patrick Ochan anaechezea Soka ya kulipwa St George ya Ethiopia na Petr Senyonjo.
Ni hatua nzuri kufika Robo Fainali na tuiombee dua timu yetu iweze kuvuka kikwazo kinachofuata na kuturudishia raha ya kulitwaa Kombe la Chalenji kwani mara ya kwanza na ya mwisho kulitwaa ni 1995 takriban miaka kumi na nne iliyopita.
No comments:
Post a Comment