Habari za Punde

DK. KARUME ATABIRI UPINZANI KUANGUKA KATIKA UCHAGUZI HUU.

Akumbusha kampeni nyumba kwa nyumba ziendelee
Asema mafanikio sekta za kijamii ni kilelezo cha mafanikio ya Z'bar

Na Mwantanga Ame

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume amevitaka vyama vya Upinzani vitarajie kutoka kapa na ushindi kubakia kwa Dk. Ali Mohammed Shein, kwa Zanzibar na Rais Kikwete kwa Tanzania Bara.

Dk Karume alieleza hayo, jana wakati akifungua tawi la CCM jimbo la Kiembe samaki liliopo Mbweni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema upinzani utarajie kuanguka vibaya kwenye uchaguzi huo, huku wagombea wa Chama cha Mapinduzi wataibuka na ushindi mkubwa.

Kutokana na hali hiyo Dk. Karume aliwataka wananchi na wanachama wa CCM kuitumia nafasi yao hivi sasa kuanza kazi ya kupita nyumba hadi nyumba kuomba kura ili kukiwezesha Chama hicho kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi Mkuu ujao.

Wakimaliza kazi hiyo Dk. Karume aliwataka wanachama hao kuondoa hofu na kutembea kifua mbele kuelezea mafanikio ya ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005/ 2010 kwani imeweza kuifanya CCM kuwa na kila sababu za kujivunia maendeleo yaliopatikana katika kipindi hicho.

Alisema hilo walifanye kwa vile zipo sababu za msingi katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake zimejionesha kwa kuwaletea maendeleo makubwa wananchi wa Zanzibar chini ya CCM, na vyama vya upinzani havina uwezo wa kuyafikia.

Akichanganua maendeleo hayo, alisema ni yale yaliojionesha katika sekta ya Afya kuimarishwa huduma za kinga na tiba, huku sekta ya elimu ikiwawezesha watoto wote wa Zanzibar kupata nafasi za kusoma na kuongezeka kwa skuli za sekondari pamoja na kuanzishwa kwa vyuo vikuu.

Eneo jengine ambalo amelitaja kuwa la mafanikio ni Sekta ya umeme ambapo tayari imeimarika kwa Unguja na Pemba, vikiwemo visiwa vidogo vidogo ambapo karibuni serikali inatarajia kuzindua rasmi mradi wa umeme katika kisiwa cha Tumbatu.

Alisema mradi huo unatarajiwa kufunguliwa Oktoba 22, mwaka huu ambapo itavifanya visiwa vidogo vyenye huduma ya umeme kufikia vitatu kikiwemo cha Uzi, na Kojani huku vikiwa vimebakia cha Makoongwe, Kisiwa Panza na Fundo ambavyo vitapelekewa huduma hiyo na na serikali ya CCM.

Akitaja huduma nyengine ambazo zimewezwa kuimarishwa katika miaka 10 yakuwepo kwake madarakani ni pamoja na mtandao wa mawasiliano, ujenzi wa barabara ambapo aliwahakikishia bara bara ya Bumbwini na Mwera zitamalizwa karibuni.

Kuhusu kilimo, alisema kwa asilimia kubwa aliweza kukimarisha kwa kuanzisha kilimo cha Umwagiliaji maji ikiwa ni chimbuko la wazo la Chama cha Mapinduzi katika ilani yake ya 2005.

Kutokana na mafanikio hayo, Dk. Karume alisema kuwa kazi kubwa ambayo wanachama wa CCM wanapaswa kuiona kwa umuhimu wake ni kuyatumia matawi ya chama kwani ndio yatayoweza kuwa chachu ya maendeleo ya nchi kwa vile humo ndimo huanza mipango yake.

Alisema kuwa Chama cha mapinduzi kimekuwa kikithamini matawi ya Chama tangu utawala wa ASP kwani ndio yaliyoweza kuiletea neema Zanzibar kwa vile wananchi waliweza kukaa na kupanga mambo mbali mbali ya maendeleo.

Dk.Karume alisema maendeleo ya 2010 ni chimbuko la ilani yake iliopangwa katika matawi ya CCM na kama imewezekana kuleta mafanikio iweje washindwe kuyatumia matawi hayo ili ilani ya 2015, isiweze kupata mafanikio.

Dk Karume aliahidi kutoa ushirikiano na wanachama wa Jimbo hilo kutoa misaada mbali mbali itayolifanya tawi hilo kuwa la kisasa ili kuweza kufanyika shughuli za wanachama wa jimbo hilo.

Mapema Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini, Ramadhani Abdalla Ali, alimpongeza Rais Karume kwa jitihada zake za kufufua chama kwa kujenga matawi ya Chama na maskani sehemu mbali mbali ambayo yameweza kuinua uhai wa chama.

Akiyataja matawi na maskani hizo kuwa ni Mwembe Kisonge, Rahaleo, Kachorora na maeneo mengine ya Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.