Salma Said, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein amekuwa akisitasita kuwaapisha majaji wanne aliowateua Novemba 29 mwaka huu kufuatia barua aliyoandikiwa na Chama Cha Mawakili Zanzibar (ZLS) juu ya uteuzi huo kutozingatia taratibu.
Kusita huko kwa Dk Shein kuwaapisha tangu awateue kunaelezwa kuwa kunatokana na utata wa kisheria uliopo kutokana na majaji hao kutoiva vya kutosha katika taaluma ya sheria na kwa mujibu wa sheria tume ya utumishi ilipaswa kukaa kuidhinisha majina hayo jambo ambalo halikufanywa kwa baadhi ya majaji walioteuliwa.
Baadhi ya mawakili wakiongozwa na rais wa chama cha mawakili Zanzibar, Yahya Khamis Hamad waliosaini barua ya kumpinga Dk Shein juu ya uteuzi wa majaji hao ambao kwa mujibu wa maelezo yao hawana sifa zinazowafanya wawe majaji wa mahakama kuu.
Rais wa Zanzibar kwa mamlaka aliyopewa alifanya uteuzi wa majaji wanne wa Mahakama Kuu pamoja na Mwenyekiti wa Mahkama ya Ardhi ambaye ni Haroub Sheikh Pandu, na majaji wanne wa mahakama kuu akiwemo Abdul-hakim Ameir Issa, Fatma Hamid Mahmoud, Mkusa Isaac Sepetu, na Rabia Hussein Mohammed.
Chama hicho kilisema uteuzi huo, ulikuwa unatumia mamlaka aliyopewa rais na Katiba ya Zanzibar, 1984 kifungu cha 94(2) na (3) ambapo Chama cha Mawakili hakina mashaka na uteuzi wa Abdul-hakim Ameir Issa, wala uteuzi wa Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi, Haroub Shehe Pandu.
Chama hicho kilisema kuwa mashaka yapo kwa Fatma ambaye ni mtoto wake Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mkusa Isaac Sepetu na Rabia Hussein Mohammed ambao wote watatu wanadaiwa kutokuwa na sifa zinazostahiki kuteuliwa nafasi hiyo.
Juzi Disemba tatu usiku Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud aliitisha kikao cha tume ya utumishi ambacho anadaiwa kuwa hakikupitisha jina moja la jaji aliyeteuliwa na mawakili hao ili wajadiliane, lakini kikao hicho kilishindwa kufanyika baada ya kupokea barua nyengine kutoka chama cha mawakilishi kusema kwamba kikao kitakachofanyika hakitokuwa halali kwa mujibu wa sheria kwa kuwa wajumbe wa kikao hicho hawakutimia.
Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na katibu wa chama cha mawakili, Salim Mkonje iliyotumwa kwa rais wa Zanzibar ya Desemba tatu mwaka huu, ambayo tayari saini ya rais inaonesha ameshaipokea ilisema kwamba wakili Awadh Ali Said ambaye alikuwa mjumbe wa tume ya uajiri anayetokana na chama hicho katika vipindi viwili vimekwisha tokea septemba 17 mwaka huu hivyo hawezi kuwa mjumbe tena hadi hapo atakapoteuliwa tena.
Mbali na mjumbe huyo, lakini pia Jaji Mshibe Ali Bakari naye muda wake umekwisha kwa mujibu wa sheria ya tume hiyo No 13 ya mwaka 2003 koramu ni wajumbe watano kifungu cha 9(2).
“Kufuatia kikwazo hiki, wakili Awadh alifahamishwa na katibu wa tume ya uajiri ya mahakama asihudhurie kikao cha leo 3 Desemba jana usiku” ilisema barua hiyo kutoka kwa mawakili. Na kuongeza kwamba.
“Kwa sababu wajumbe waliokuwepo walikuwa sita hivyo kupungua kwa wajumbe wawili kunapelekea tume isiweze kufanya maamuzi kama sheria inavyotaka kwani yatakuwa batili kwa kukosekana koram,” alisema barua hiyo.
Aidha chama hicho kimeitisha kikao chake jana kuteuwa jina la wakili ambaye atakiwakilisha chama hicho na kulipeleka kwa rais ili ateuliwe kuingia katika kikao hicho ikiwa pamoja na wajumbe wengine ambao sheria inasema tume hiyo iwe na wajumbe wanane akiwemo jaji mkuu, mwanasheria mkuu na mwenyekiti wa tume ya utumishi, na kadhi mkuu
Hii habari ya Salma naona ina mushkel. Inaonekana kama kwamba imeandikwa na mtu ambae sio mwandishi wa habari makini. Kichwa cha habari halilingani na habari yenyewe. au ni katika kuuza magazeti? Mwandishi hakutoa ushahidi wowote unaoelezea kuwa Raisi anasitasita. Kwa mfano nilitegemea muandishi aseme kuwa kulingana na sheria fulani raisi alipaswa kuwaapisha majaji baada ya siku mbili au tatu. Lakini hakusema hilo. Sasa ushahidi wa kuwa raisi anasitasita uko wapi?
ReplyDeleteMdau.
Simtetei Salma, ila nadhani ni mwendelezo wa habari hii ambao imekuwa kwenye public interest na hasa wengi kutaka kujua next move ya Mr President baada ya mawakili kutoa petition yao.
ReplyDeleteTitle hii ipo kwenye gazeti la Mtanzania ama mwenyewe Salma kichwa cha habari alichokipa ni "Dk Shein Kuwaapisha Majaji Kesho?" Sasa sijui twende na mawazo ya mhariri au ya mwandishi mwenyewe