JESHI la Polisi Zanzibar limesema tokea kuwepo kwa sera ya Polisi Jamii katika maeneo mbali mbali ya Mjini, limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya uhalifu, hasa katika matukio ya uvunjaji na wizi.
Hayo aliyasema Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa, katika mkutano wake na wananchi wa Shehia za Kwaaliato na Kwahani, pamoja na vikundi vya Polisi Jamii vya Shehia hizo, uliofanyika Kwahani Uwanja wa Farasi.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za Jeshi hilo kwa upande wa wilaya ya Mjini, kwa mwezi wa Januari wamepokea kesi tatu za uvunjaji na moja ya wizi kwa mwezi wa Februari, hali ambayo imepunguza matukio hayo ikilinganishwa na miezi iliyopita.
Alisema hali hiyo imetokana na nguvu za pamoja za wananchi kuamua kuanzisha ulinzi wa Polisi Jamii wenye lengo la kupunguza uhalifu na kero zinazowakabili katika maeneo yao.
Alisema sera ya Polisi Jamii ni ushirikishwaji wa wananchi kwa kusaidiana na Polisi katika ulinzi kwa kuondosha matatizo mbali mbali ya uhalifu yanayowakabili, ili jamii iweze kuishi kwa salama pamoja na mali zao.
"Bila ya wananchi Polisi hawawezi kufanya kazi zao, na ndiyo maana Polisi imeamua kwa makusudi kuanzisha sera hii ili iweze kushirikiana na wananchi kwa kuwafichua wahalifu, ambao wao ndio wajuzi wakubwa wa kuwatambua wakaazi wenzao katika maeneo yao", alisema Kamishna Mussa.
Akiyataja baadhi ya maeneo yaliyopiga hatua kubwa ya katika suala hilo ni Kwaalinato, Mji Mkongwe pamoja na Mkele ambayo amlieleza kuwa, wahalifu wengi wameyakimbia kutokana na kukabiliwa na wakati mgumu wa kisheria zinazochukuliwa na Polisi Jamii katika maeneo hayo.
"Sote ni mashahidi, maeneo hayo yalikuwa yanaongoza kwa uhalifu, lakini hivi sasa huwezi kuamini kwa jinsi yalivyotulia, unaweza kupita usiku wa manane ukiwa na vitu vya thamani bila ya kubughudiwa, hali hiyo imetokana na ulinzi wa Polisi jamii, ambao umeweza kudhibiti uhalifu kwa kiasi kukubwa katika maeneo hayo", alifahamisha.
Hivyo ametoa wito kwa viongozi wakuu wa majimbo wakiwemo Wabunge, Wawakilishi pamoja na Madiwani kushirikiana kwa pamoja na vikundi hivyo ili viweze kupata nguvu pamoja na ari ya utendaji wa kazi zao za kutokomeza uhalifu.
"Kama tunavyofahamu Polisi Jamii ni suala la kujitolea na linalohitaji moyo, hawalipwi mshahara wala posho na si vibaya viongozi wao wakawachangia angalau fedha kidogo, huku wananchi kwa upande wao wakajitolea angalau kila nyumba shilingi 100 kwa siku, ili ziweze kuwasaidia katika kazi zao hizo ngumu za kila siku", alishauri Kamishana huyo.
Aidha aliwataka wananchi kuwafichua wahalifu katika maeneo yao, na kuachana na tabia ya kuoneana muhali kwani hali hiyo haitaweza kufanikisha azma ya kutokomeza uhalifu katika maeneo yao.
Pia alishauri kuwepo kwa kamati za ulinzi na usalama na ustawi wa jamii kwa lengo la kuzungumzia matatizo pamoja na kero zinazowakabili na kuzitafutia njia za kuzipatia ufumbuzi.
Mapema Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Kamishna Msaidizi wa Polisi Aziz Juma amevitanabahisha vikundi vya ulinzi vya Polisi Jamii, kuachana na tabia ya kuwapiga wahalifu wanapo wakamata kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.
"Kumpiga mtu ni kinyume cha sheria, mnapomkamata muhalifu mnatakiwa kwanza muhakikishie usalama wake, na kumfikisha katika vyombo vya sheria akiwa salama", alifahamisha Kamanda Aziz.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mkuu wa wilaya ya Mjini Luteni Kanali mstaafu Abdi Mahmoud Mzee, ambaye katika nasaha zake alisema maendeleo ya nchi pamoja na suala zima la ulinzi ni jukumu la wananchi wenyewe, ambao wao ndio wadau wakubwa wa kuifanya nchi iweze kuwa katika hali ya usalama na amani.
Wengine waliohudhuria ni Mbunge wa Jimbo la Jang'ombe Hussein Mustafa, Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Ali Salum, Madiwani wa Kwahani na Kwaalinato, pamoja na baadhi ya watendaji wa Jeshi la Polisi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment